Ø Chauza
kama njugu
Ø Kuingia
Ulaya, Japan na Marekani kuanzia wiki
ijayo
Na:
Ali O. Ali
Kile
kitabu cha ‘PAKA WA BINTI HATIBU’
ambacho kilikuwa kikisubiriwa kwa hamu na shauku kubwa hatimaye kimeingia
mitaani tayari kufikisha ujumbe na kutoa burudani kwa jamii iliyokusudiwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii,
mtunzi wa kitabu hicho Mhadhiri Yussuf Hamad, wa Chuo kikuu cha London, SOAS
nchini Uingereza, amethibitisha kupokea taarifa na ithibati rasmi kutoka kwa
mchapishaji wa kazi hiyo, The Jomo Kenyatta Foundation Educational
Publishers ya Nairobi nchini Kenya.
“Ninaweza kukuthibitishia ndugu mwandishi
pamoja na kuwathibitishia wapenzi, washabiki na wasomaji wangu kwa ujumla kuwa
kitabu hivi sasa kipo madukani na kinapatikana kwa bei nafuu kabisa.’ Alisema
Bwana Yussuf.
Kitabu cha Paka wa Binti hatibu, kilitarajiwa
kutoka mapema mwezi Novemba mwaka jana lakini kutokana na matatizo ya kiufundi,
kitabu hicho kilichelewa kutoka hadi mwezi Machi mwaka huu ambapo kinapatikana
maduka yote ya vitabu hasa hasa katika duka la The Jomo Kenyatta Book Distribution Center, iliyopo Kijabe
Street, jijini Nairobi.
Akitoa ufafanuzi juu ya namna gani kitabu hicho
kinaweza kuwafikia walengwa nchini Tanzania na nchi nyengine za Ulaya, Afisa wa
shirika hilo la Uchapishaji Bibi Anne alisema;
“Kwa sasa kitabu kinapatikana hapa Nairobi.
Lakini tumekuwa tukipata ‘order’ kutoka sehemu za Ulaya kama vile Uingereza, Japani na Marekani na ijapokuwa tulikuwa
hatujajipanga kwa hilo tunatafuta utaratibu wa kukifikisha huko pia muda si
mrefu. Hadi sasa kuna order ya kopi 100 ambazo zimeagiziwa kutumwa Uingereza.
Tunajaribu kutafuta njia za kuwafikia wasomaji wetu wa huko na muda si mrefu
tutaweza kuwafikia.’
Alipoulizwa kuhusu vipi kitabu kitawafikia
wasomaji waliopo Tanzania na visiwani Zanzibar, Bibi Anne alisema;
“ Kwa sasa hatuna wakala nchini Tanzania.
Isipokuwa wateja walioko Tanzania wanaweza kuwasiliana na kampuni ya Dar es
Salaam Printers Limited ambao wataweza kuagizia vitabu hivyo na kuwafikishia
Watanzania. Tunawashauri wateja wetu walioko huko kufanya mawasiliano na
kampuni hiyo ili waweze kukipata kitabu hicho”
Wakati huo huo, Kampuni binafsi ya uchapishaji
na usambazaji ya JC PRESS iliyoko jijini
London nchini Uingereza, imeeleza nia yake ya kutaka kuwasiliana na kampuni ya
Jomo Kenyatta Foundation ili kuweza kushirikiana katika kukisambaza kitabu
hicho kwa urahisi katika nchi za Ulaya na hususan kwa njia ya mauzo mtandaoni
ambayo ni rahisi katika nchi nyingi za Ulaya na Marekani. Kwani kufanya hivyo kutarahisisha kupatikana
kwa kitabu hiki kwa wepesi zaidi hasa ukizingatia kuwa ni kitabu ambacho
kimevuta na kugusa hisia za wasomaji wengi.
Aidha, naye mkuu wa Idara ya masomo ya Kiafrika
wa chuo kikuu cha London SOAS, Bibi Alena Rettova amesema kuwa Idara yake
imejipanga kukifanyia kitabu hicho uzinduzi rasmi baada ya mapumziko ya pasaka.
Kitabu cha Paka wa Binti Hatibu ni kazi ya
kwanza ya mwandishi Yussuf Shoka HAMAD kutoka Visiwani Zanzibar. Kitabu hicho
kina hadithi fupi saba ambazo zimebeba dhima na dhamira mbali mbali za kijamii.
Alipoulizwa kuhusu ubora wa kazi yake hiyo ya awali Bwana Hamad alisema;
‘Hii ni kazi yangu ya kwanza kuchapishwa.
Ninazo kazi nyingine nyingi hivi sasa. Lakini hii ni ya kwanza. Na kama mjuavyo
Waswahili husema; ‘Kipya kinyemi, ingawa kidonda!’ Naamini nimejitahidi kadiri
niwezavyo kuifanya kazi hii iwe na bora mlioutarajia. Ila kama mnavyofahamu,
kazi ya Binadamu haiachi kuwa na makosa. Kwa vile ni kazi ya mwanzo, basi
makosa madogo madogo ya hapa na pale yanaweza kujitokeza. Mimi si malaika. Ni binaadamu
mwenye mapungufu. Ila, pamoja na hayo, nawaahidi makubwa wasomaji wangu
watakaokisoma kitabu hiki.”
PICHA NA MAELEZO
Gamba la Kitabu cha PAKA WA BINTI HATIBU: Kulia
anaonekana Binti Hatibu na Paka wake. Kushoto ni wageni waliomtembelea ili
kujua kadhia ya Paka huyo!
Mwandishi wa ‘PAKA WA BINTI HATIBU’ Bwana Yussuf Shoka
HAMAD akiwa ofisini kwake SOAS, jijini London mapema wiki hii
No comments:
Post a Comment