Habari za Punde

MWANAMKE WA AFRIKA BADO ANAKABILIWA NA CHANGAMOTO NYINGI - WAZIRI UMMY MWALIMU

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Ally Mwalimu ( Mb) akitoa hutuba kwa niaba ya Kundi la Nchi za Afrika wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 60 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake ( CSW).Mkutano  huu  wa wiki mbili unawakusanya wawakilishi  kutoka serikali mbalimbali  duniani na Asasi za Kiraia ambapo   hujadiliana na kubalishana uzoefu na kuelimishana kuhusu hatua mbalimbali ambazo serikali zao zinachukua katika kuboresha  maisha ya mwanamke na mtoto wa kike.
Mhe. Waziri akiwa na mwenyeji wake,  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi,  Mhe. Waziri anaongoza ujumbe wa  Tanzania katika Mkutano huu muhimu kuhusu masuala ya  maendeleo ya wanawake.
Waziri wa Malawi akimpongeza Waziri  Ummy Mwalimu mara  baada ya hotuba yake aliyoitoa kwa niaba ya Kundi la Nchi za Afrika.
Mhe. Waziri Mwalimu akichangia majadiliano  ya Mawaziri yaliyofanyika mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa 60 wa Kamisheni kuhusu hali ya Wanawake.  Majadiliano hayo ya  Mawaziri yalihusu uimarishaji  wa mfumo ya kisheria na kisera kwaajili na utekelezaji wa usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Na Mwandishi Maalum, New York
Wakati mamia ya wanawake kutoka serikalini na Asasi za Kiraia wakiwa wanakutana hapa Umoja wa Mataifa kwa mkutano wao unaojadili hali yao katika maeneo mbalimbali.

Mamia mengine ya wanawake hususani  wale wa Afrika wanaendelea kukumbana na changamoto lukuki zinazowarudisha nyuma kimaendeleo.

Ni wanawake hao wanaoishi katika nchi zenye migogoro, vita visivyokwisha, wenyekukabiliwa na uhaba na ukosefu mkubwa wa chakula, maji safi na salama,  matatizo yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi,  ndio ambao Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Mhe. Ummy Ally Mwalimu (Mb) ameitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza kasi ya ushirikiano ili malengo mapya ya maendeleo endelevu (Agenda 2030)  yaweze kuwafikia.

Waziri  Mwalimu ametoa wito huo jana jumatatu,  wakati alipotoa hutuba kwa niaba ya nchi za Afrika katika siku ya  kwanza ya Mkutano wa  60 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya wanawake (CSW) ambao umeanza hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Changamoto hizo pamoja na nyinginezo nyingi zikiwamo kutopata fursa ya huduma za afya ya uzazi salama, elimu na usawa wa kijinsia zinamfanya mwanamke wa Afrika ashindwe kushindana na wanawake wenziwe hususani  wale walioko katika mataifa yaliyoendelea.

Waziri Mwalimu ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu wa wiki mbili,  alitoa hotuba hiyo kwa niaba ya nchi za Afrika kutokana na kwamba Tanzania kupitia Uwakilishi wake wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ni Mwenyekiti wa Kundi  la Nchi za Afrika kwa mwezi huu wa March.

Amewaeleza washiriki wa mkutano huo waliofurika katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwamba.

Ingawa pamekuwa na makubaliano na mapendekezo mengi kuanzia yale yaliyofikiwa huko Beijing, bado mwanamke anayeishi katika nchi zenye migogoro na vita barani Afrika ataendelea kuachwa nyuma na hivyo kukosa fursa ya kushindana na wenziwe.

“Ingawa  vita,   ukame wakutisha,  ukosefu wa chakula, ukosefu wa maji safi, ukichangia na ukosefu wa fursa za kiuchumi,  kijamii na kisiasa ni matatizo yanayowakabili watu maskini lakini mwanamke ndiye anayeathirika zaidi” akaeleza Waziri Mwalimiu

Na kuongeza kwamba Afrika inaendelea kutilia mkazo hoja ya kuwashirikisha wanawake katika majadiliano na utoaji wa maamuzi katika masuala yanayowagusa yakiwamo masuala yanayohusu mabadiliko ya tabian china usuluhishi wa migogoro.

Akaeleza kwamba, nchi zinazoendelea na zilizoendelea zinapashwa kuongeza kasi ya ushirikiano na ubia baina yao ili kufanikisha utekelezaji Agenda 2030), Makubaliano juu Mabadiliko ya Tabia nchi yaliyofikiwa huko Paris Ufaransa mwaka jana na makubaliano yaliyofikiwa na waafrika wenye kupitia Ajenda 2063, ili katika umoja wake dunia basi iweze kumwondoa mwanamke na jamii nzima kutoka hapa ilipofikia hali bora zaidi ya maisha.

Kama  hiyo haitoshi Waziri amesema, Afrika inaamini pia katika uwezeshwaji wa Sekta binafsi, kupanua wigo wa ujasiliamali kama njia moja wapo ya kukuza uchumi endelevu, usawa wa kijamii,  usawa wa jinsia, ulinzi wa mazingira na uwezeshaji wa mwanamke.

Mada kuu ya Mkutano wa 60 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake, ni “Uwezeshaji wa Wanawake na uhusiano wake na Ajenda 2030

Awali akizungumza mwanzoni mwa mkutano huu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki   Moon amasema tangu alipoingia madarakani mwaka 2006 amejitahidi kuongeza nafasi za viongozi wanawake katika Idara za Sekreatarieti ya Umoja wa Mataifa.

Akitilia msisitizo hoja na haja ya kupanua wigo wa wanawake kushika nafasi katika ngazi za juu za maamumizi, Ban Ki Moon amesema, ingawa nchi nyingi zimejitahidi sana kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za juu za uongozi bado kuna Nchi Tano ambazo hazina wanawake katika Mabunge yao ili hali Nchi nyingine 7 hazina mawaziri wanawake katika serikali zao.

Naye Rais wa Baraza Kuu la 70 la Umoja wa Mataifa Bw Monges Lykketoft, akizungumza wakati wa mkutano huo,  pamoja na kusisitiza umuhimu wa utekelezaji wa Agenda 2030 ambayo ameitaja kuwa ni pamoja na kuendelea kupigia chapuo la kutaka Katibu Mkuu ajaye wa Umoja wa Mataifa awe  Mwanamke.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.