Na Mbaraka Kambona,
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame
Nyanduga amesema kuwa jukumu la usimamizi na utetezi wa masuala ya haki za
binadamu sio jukumu la Serikali, Asasi za kiraia wala mtu binafsi, ni jukumu la
watu wote.
Nyanduga aliyasema hayo jana alipokuwa akifunga mkutano wa siku tatu wa
wadau wa haki za binadamu uliofanyika jijini Dar es Salaam kujadili mapendekezo
ya tathimini ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu.
Katika mkutano huo, Nyanduga alisema kuwa haki za binadamu zinamuhusu kila
mmoja wetu, hivyo ni muhimu kwa tume na asasi za kiraia kushirikiana kwani wote
wanafanya kazi moja ya kujenga taifa lenye kuheshimu haki za binadamu.
“Tume haichagui nani wa kushirikiana nae kwa kuwa masuala ya haki za
binadamu sio miliki ya serikali, asasi za kiraia wala mtu binafsi, bali ni
jukumu letu sote” alisema.
Aliongeza kuwa: “ni muhimu tukashirikiana sisi wote kwa kuwa lengo letu ni
kujenga taifa lenye kuheshimu haki za binadamu”
Aidha, Nyanduga alisema baada ya kumalizika kwa mkutano huo ni muhimu kwa
tume na asasi za kiraia kukaa pamoja ili kuyapitia vizuri mapendekezo hayo
ambayo wamekubaliana na kuandaa taarifa ambayo wataiwasilisha serikalini kwa ajili
ya kuishawishi serikali iweze kuyakubali mapendekezo hayo ambayo awali
iliyakataa.
Awali, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),
Onesmo Olengurumwa, aliwataka wanahabari kutumia fursa waliyoipata katika
mkutano huo kuelimisha jamii kuhusu mchakato mzima wa tathimini ya utekelezaji
wa masuala ya haki za binadamu.
“Mkutano huu umekuwa ni fursa kwenu wanahabari kujua namna mchakato wa tathimini ya
utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu unavyokuwa kwa kuwa hamkuwepo Geneva,
lakini kupitia mkutano huu mumeweza kuelewa, hivyo naomba mtumie fursa hii
kuelimisha jamii kuhusu mchakato huo”, alisema Olengurumwa
Olengurumwa aliipongeza tume kama taasisi ya kitaifa inayosimamia masuala
ya haki za binadamu kwa ushirikiano wao mkubwa ambao wamekuwa wakiendelea
kuutoa kwa asasi za kiraia na aliiomba
taasisi hiyo kuendelea kufanya hivyo kwani ndio njia pekee itakayosaidia kupiga
hatua kubwa katika masuala ya usimamizi wa haki za binadamu kama nchi.
Itakumbukwa kuwa Juni 27-29 mwaka huu, wadau wa haki za binadamu walikutana
jijini Dar es Salaam kujadili mapendekezo ya tathmini ya utekelezaji wa masuala
ya haki za binadamu nchini ili kupanga mikakati ya kuweza kuishawishi serikali
kuyakubali mapendekezo iliyokataa katika mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu
uliofanyika Geneva Mei, mwaka huu.
katika Mkutano huo mapendekezo ya jumla yalikuwa 227, serikali ilikubali
mapendekezo 130 na kuyakataa 72 na 25
iliyaweka pembeni.
No comments:
Post a Comment