STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 19.09.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.
Ali Mohamed Shein leo amefanya ziara ya kutembelea eneo litakalojengwa soko la
samaki, Malindi, ujenzi wa mradi wa hoteli ya Bwawani pamoja na kutembelea eneo linalotaka kujengwa
Ofisi za Benki ya Watu wa Zanzibar huku akieleza azma ya Serikali katika
kutekeleza miradi yake mipya iliyopangwa.
Katika ziara yake
hiyo, Dk. Shein alipata maelezo juu ya uendelezaji wa miradi hiyo muhimu na
kupongeza hatua zianazoendelea kuchukuliwa huku akisisitiza haja ya
kuharakishwa ili kumaliza kwa wakati uliopangwa sambamba na kuwepo kwa
mashirikiano ya pamoja kwa taasisi husika za Serikali.
Dk. Shein akiwa ameongozana
na viongozi mbali mbali, alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa
kwa wakati uliopangwa ikiwa ni pamoja na ukarabati wa Chelezo ili eneo hilo
liweze kuvutia.
Mapema Dk. Shein
alitembelea eneo litakalojengwa soko jipya la Samaki, Malindi na kupata maelezo
kutoka kwa uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi pamoja na
taasisi nyengine zikiwemo Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Mamlaka ya Maji
Zanzibar (ZAWA) na Mamlaka ya Mji Mkongwe Zanzibar.
Kwa upande wa Wizara
husika ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na
Uvuvi, Waziri wa Wizara hiyo Hamad Rashid alimuhakikishia Dk. Shein kuwa tayari
Bunge la Japan limeshatoa baraka zake kwa kuahidi kutoa fedha taslim kwa ajili
ya ujenzi wa mradi huo na kueleza kuwa fedha hizo ziko tayari.
Nae Mkurugenzi wa
Idara ya Uvuvi Mussa Aboud Jumbe alimueleza Rais hatua zilizofikiwa katika
ujenzi wa soko hilo linalojengwa kwa mashirikiano ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar pamoja na Serikali ya Japan
chini ya Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).
Akitoa maelezo
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa soko hilo linalotarajiwa kuaza ujenzi wake mapema
mwakani litakuwa la kisasa ambalo pia litakuwa na sehemu ya maegesho ya vyombo
vya uvuvi vikiwemo vinavyovua bahari kuu, maeneo maalum kwa ajili wavuvi na
wafanya biashara nyenginezo.
Aidha, Dk. Shein
alipita njia ya Ras Al Khaimah, Malindi Funguni na kupata maelezo juu ya diko
lisilo rasmi katika eneo hilo kutoka kwa uongozi wa Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Usafirishaji pamoja na Wizara ya Kilimo, Maliasili Mifugo na
Uvuvi.
Dk. Shein aliendelea
na safari yake iliyoelekea hadi hoteli ya Bwawani ambako alipata maelezo kwa
wakandarasi wanaoshughulikia mradi wa ujenzi wa Hoteli ya Bwawani ambapo alisisitiza
haja ya kufanyia haraka ujenzi wa mradi huo.
Akiwa katika eneo hilo,
Dk. Shein alipata maelezo kutoka kwa Msimamizi
wa ujenzi huo Syed Mansoor Hussain kutoka Kampuni ya “Stone Town Village Lmt” ambaye
alieleza kuwa ujenzi wa mradi huo utakuwa wa awamu tatu ambao tayari awamu ya
kwanza imeshaaza.
Alieleza kuwa awamu ya
kwanza itahusisha ujenzi wa ukumbi wa Salama, hoteli pamoja na eneo la hoteli
hiyo ambapo ujenzi wa awamu hiyo
unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka ujao.
Kwa upande wa awamu ya
pili ya ujenzi huo utahusisha maduka makubwa na madogo pamoja na mambo mengine
muhimu yaliyomo katika mradi huo.
Dk. Shein pia, alipata
fursa ya kutembelea eneo litakalojengwa Makao Makuu ya Benki ya Watu wa
Zanzibar hapo Malindi Mjini Zanzibar na kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa Benki
ya Watu wa Zanzibar PBZ, ambao ulimueleza kuwa ujenzi huo unatarajiwa kuanza
mwishoni mwa mwaka huu na unatarajiwa kugharimu Tsh. Bilioni 3.8 hadi kumalizika kwake.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment