Habari za Punde

Balozi Seif Akabidhi Madawati Skuli ya Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi akijiandaa kumkabidhi madawati 111 Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Kitope Mwalimu Suleiman Juma Makame yaliyotolewa mchango na Kampuni ya Mitandao ya Mawasiliano ya simu za Mkononi ya Tigo.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Nd, Issa Juma akitoa Takwimu za kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa Skuli zilizomo ndani ya Wilaya hiyo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Madawati kwa Skuli ya Kitope ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi.
Kushoto ya Nd. Issa ni Mwakilishi wa Jimbo la Kitope Balozi Seif, Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Bahati Ali Abeid na Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi.
Baadhi ya Madeski aliyoyakabidhi Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif kwa Skuli ya Kitope yaliyotolewa mchango na Kampuni ya Mitandao ya Mawasiliano ya simu za Mkononi ya Tigo.(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na Othman Khamis. OMPR.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema matokeo mazuri ya ufaulu wa wanafunzi wa Jimbo la Mahonda na Wilaya nzima ya Kaskazini “B” kwa ujumla utatoa sura nzuri  kwa wafanuzi hao kuwa na uwezo kamili wa     Kitaaluma utakaowawezesha kuendelea na masomo yao ya darasa la 13.

Alisema utaratibu wa kutoa Viongozi Waandamizi ndani ya Jimbo na Wilaya hiyo unawezekana kabisa iwapo wanafunzi wenyewe kwa msaada wa walimu wao watajitahidi katika kutafuta elimu kwa bidii.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi Madawati 61 kwa ajili ya kusaidia kupunguza uhaba wa Vikalio kwenye Skuli za Msingi na Sekondari za Kitope.

Madawati hayo 61 ni miongoni mwa Madawati 111 yaliyotolewa mchango na Kampuni ya Mtandao wa Simu za Mkononi Tanzania ya Tigo kwa ajili ya Jimbo la Mwakilishi wa Mahonda yakiwa na thamani ya Shilingi Milioni 20,500,000/- hafla iliyokwenda sambamba na Balozi Seif kukabidhi mchele na fedha Taslimu kwa wanafunzi walioanza kambi wakijiandaa kwa mitihani yao ya Kitaifa hapo baadae.

Hata hivyo Balozi Seif alitanabahisha kwamba kazi za usimamizi wa wanafunzi katika kutafuta Elimu si vyema wakaachiwa Walimu pekee, bali mchango wa Wazazi na walezi unahitajika katika kufanikisha suala hilo muhimu.

Alisema licha ya kwamba ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao unahitajika kufikia hatua ya asilimia 60% lakini mchango wa Viongozi wa Jimbo hilo bado unahitajika zaidi katika kuhakikisha mazingira mazuri ya wanafunzi hao katika kutafuta Elimu yanapatikana.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda alifahamisha kwamba katika kuunga mkono jitihada za Wal;imu na Wanafunzi hao za kuimarisha miundombinu ya Skuli hiyo aliahidi kuchangia Mashine ya Fotokopi muda mfupi ujao ili kuwaondoshea usumbufu wanataaluma hao wakati wanapojiandaa kufanya Mitihani yao ya Taifa.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini”B” Nd. Issa Juma alitahadharisha kwamba  matokeo ya mitihani ya Darasa la 12 { Form IV } bado hayaridhishi ndani ya Wilaya hiyo jambo ambalo jitihada za makusudi zinalazimika kuchukuliwa kati ya Wazazi, Walimu na wahusika wenyewe Wanafunzi.

Nd. Issa alisema utafiti uliofanywa na Wataalamu wa Elimu kuhusu ufaulu wa Wanafunzi ndani ya Wilaya hiyo umebaini kuporomoka kwa viwango vya ufaulu vya wanafunzi katika skuli nyingi za Wilaya ya Kaskazini “B” hasa katika Mitihani ya Darasa la 12.

Aliwataka wafunzi hao wa Skuli ya Kitope pamoja na zile zilizomo ndani ya Wilaya yake kumsifu Mwakilishi wao wa Jimbo la Mahonda pamoja na Viongozi wenzake kwa kuunga mkono sekta hiyo muhimu ya Elimu kwa maendeleo ya Taifa.

Akigusia changamoto ya vikalio Maskulini Mkuu huyo wa Wilaya ya Kaskazini “B” alizipongeza jitihada za makusudi zinazochukuliwa na Viongozi wa Jimbo la Mahonda katika kuimarisha Sekta ya Elimu. 

Alisema skuli za Wilaya hiyo kwa sasa zimepunguza changamoto kubwa ya uhaba wa vikalio kutokana na jitihada kubwa inayoendelea kuchukuliwa na Viongozi mbali mbali pamoja na Serikali Kuu katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo la muda mrefu.

Hata hivyo Nd. Issa alitahadharisha kwamba skuli hizo zinaweza kuendelea kupata changamoto ya vikalio vipatavyo elfu 2,068 baada ya kumalizika kwa miradi ya ujenzi wa majengo mengine mapya ya Skuli yanayoanzishwa na wenyewe Wananchi kwa njia za kujitegemea.

Wakati huo huo Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Maabara la Skuli ya Sekondari ya Kitope na kuridhika na hatua iliyofikiwa.

Balozi Seif aliwahi kufanya ziara ya kukagua jengo hilo mnamo Tarehe 28 Septemba na kushawishika kusaidia uwezeshaji wa fedha kumaliza jengo hilo kwa lengo la kuwaondoshea usumbufu wanafunzi wa Sekondari wa Skuli ya Kitope wanaoupata hasa wakati wa mitihani yao.

Ujenzi huo wa Maabara ya Skuli ya Sekondari ya Kitope unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 13.7 una muelekeo wa kumalizika kwa wakati kama ilivyopangwa katika kipindi cha wiki mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.