Habari za Punde

Zanzibar Yaadhimisha Siku ya Uoni Duniani.

Mtaalamu wa macho kutoka China Dkt. Zhao Wei akimpima macho Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo kwenye maadhimisho ya siku ya uoni Duniani yaliyofanyika kitaifa kituo cha Afya cha Magogoni, Mjini Zanzibar.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima macho kwenye maadhimisho ya siku ya uoni Duniani yaliyofanyika Kituo cha Afya Magogoni wakiendelea kuangaliwa macho.
Mratibu wa huduma za macho Zanzibar Dkt. Rajab Mohammed Hilal akisoma risala ya kitego cha matibabu ya macho kwenye maadhimisho ya siku ya uoni Duniani yaliyofanyika Kituo cha Afya Magogoni, Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na wananchi na wafanyakazi wa Kituo cha Afya Magogoni kwenye maadhimisho ya siku ya uoni Duniani yaliyofanyika katika Kituo hicho.
Mwakilishi wa Shirika la Sightsaver Tanzania Andrew Kilewela akibadiliishana mawazo na Mratibu wa Mradi wa Afya ya macho Zanzibar Dkt. Fatma Juma Omar wakati wa maadhimisho ya siku ya uoni Duniani katika Kituo cha Afya Magogoni.


Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo amewataka wananchi kuendelea kuvitumia vituo vya  afya vilivyo  karibu  nao vinavyotoa huduma  za macho katika jamii ili kupambana na upofu usiowalazima.

Amesema vituo vingi vya Afya hivi sasa vimewekewa huduma muhimu za uchunguzi wa maradhi mbali mbali, ikiwemo uchunguzi wa macho, na hakuna haja ya wananchi kukimbilia Hospitali Kuu ya Mnazimmoja.

Waziri Mahmoud ameeleza hayo katika maadhimisho ya siku ya uoni Dunini yaliyofanyika Kitaifa kituo cha Afya Magogoni Wilaya ya Magharibi B.

Amesema  madaktari wanapohisi tatizo ni kubwa na haiwezekani kupata matibabu katika vituo vidogo wanaamua kumpeleka mgonjwa Hospitali Kuu hivyo hakuna haja ya kuwa na wasiwasi na viituo hivyo.

Amesema tatizo la uoni limekuwa kubwa duniani kote na inakisiwa hivi sasa  kuna watu wasioona wapatao milioni 285 na asilimia 37 kati yao hawaoni kabisa.

Kwa upande wa Zanzibar amesema inakisiwa kuwa na watu 10,000 ambao wanamatatizo ya uoni na asilimia 50 kati ya hao hawaoni kabisa kutokana na sababu mbali mbali.

Waziri wa Afya ameongeza kuwa wataalamu wa maradhi ya tiba ya macho nchini kwa kushirikiana na Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) pamoja na taasisi mbali mbali duniiani wako katika mikakati ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya maradhi ya macho.

Hata hivyo amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya inajitahidi kuendeleza huduma za matibabu ya macho katika nyanja zote katika vijiji mbali mbali Unguja na Pemba kupitia Kitengo chake cha Afya ya msingi ya matibabu ya macho vijijini.

Amewataka wananchi kufanya juhudi kuepuka maradhi ambayo yanapelekea matatizo ya macho na kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara kwani ni moja ya tiba ya kujiepusha na maradhi mengi.

Aidha alilishukuru Shirika la Kimataifa la Sightsaver kwa ushirikiano wake wa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na misaada ya kitaalamu na dawa wanazosaidia kitengo cha matibabu ya macho.

Katika risala ya wafanyakazi wa Kitengo cha matibabu ya macho iliyosomwa na Mratibu wa Kitengo hicho Dkt. Rajab Mohammed Hilal wamesema wanakabiliwa na udogo wa nafasi ya kutekeleza katika kitengo hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.