Habari za Punde

Balozi Seif Atembelea Eneo Linalolalamikiwa na Wananchi wa Jimbo la Welezo Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi akilikagua eneo liliopo Mtofaani kwenye Makutano ya Bara bara za Hawaii na Masingi ambalo liliombwa na Wananchi kwa shughuli za Kijamii lakini kwa sasa kuna tetezi ya kumilikiwa na Mtu mwengine.
Balozi Seif akipata ufafanuzi kutoka kwa Mwenyekiti wa Tawi la Mofaani Bwana Iddi Sultan kuhusiana na utata wa eneo hilo linalomilikiwa na mtu binafsi hivi sasa.
 Balozi Seif  kushoto akiwa nyuma ya Ukuta wa Matofali uliojengwa kati kati ya eneo hilo akijaribu kuangalia upande wa Pili wa eneo hilo lenye utata wa umiliki.Aliyepo upande wa Kulia ni Mwakilishi wa Jimbo la Welezo Mhe. Hassan Khamis Hafid.
Eneo la wazi liliopo Makutano ya Bara bara ya kuelekea Msingini na Hawaii  liliopo Mashariki mwa Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Sehemu hilo.
Ukuta wa matofali uliojengwa kati kati ya Eneo la wazi liliopo Makutano ya Bara bara ya kuelekea Msingini na Hawaii  lenye kuleta utata wa umiliki wake.
(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na. Othman Khamis OMPR. 
Wananchi wa Shehia ya Mtofaani Masingini ndani ya Jimbo la Welezo wameiomba Serikali Kuu kufikiria maombi yao ya kutaka kupewa eneo lililokuwa likimilikiwa na Kikosi cha Kuzuia Magendo { KMKM } kwa ajili ya kulitumia kwa shughuli zao za Kijamii.
Wamesema eneo hilo ni sehemu pekee iliyowazi kwa shughuli za Kijamii katika shehia ya Mtofaani ambalo linaweza kuwasaidia kwa ujenzi wa Soko,huduma za Afya, Skuli na Michezo ili kuwaondoshea usumbufu Watoto na Wananchi kufuata huduma hizo katika Masafa marefu. 
Wananchi hao walipaza sauti zao mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika kukagua eneo hilo baada ya kupokea kilio chao wanacholalamikia eneo hilo kumilikiwa na Mtu aliyetambulika kwa jina Moja tu la Zahor ambae kwa sasa ameshaamua kulizunguushia Ukuta eneo lote.
Walieleza kwamba muda mrefu uliopita  Kamati ya Maendeleo ya Eneo hilo kupitia Sheha wa Shehia hiyo iliwahi kupeleka maombi yao ili kupatia eneo hilo lakini jitihada hizo hazikufanikiwa na badala yake kushuhudia ugawaji wa Viwanja uliopelekea kuwavunja moyo.
Walifahamisha kupigwa kwao na mshangao na butwaa pale Vijana wa eneo hilo walipozuiwa na Mtu huyo liyejitambulisha kulimiliki eneo hilo kutofanya shughuli yoyote ya Michezo na Burdani katika Vipindi vya  Siku Kuu za Iddi.
Akijibu hoja na kutoa ufafanuzi wa Kilio cha Wananchi hao wa Shehia ya Mtofaani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwaahidi kwamba atamuagiza Waziri anayehusika na masuala ya Ardhi pamoja na Maofisa wake kwa kushirikiana na Uongozi wa  Kikosi cha KMKM kufanya uchunguzi wa kina kutambua uhalali halisi wa Mmiliki wa Eneo hilo.
Balozi Seif  ameamua kuchukuwa hatua hizo ili kupata Taarifa na Ripoti sahihi itakayobainisha Mmiliki halali wa sehemu hiyo ili Serikali Kuu itakapokuja chukuwa maamuzi isije ikaonea upande wowote.
Eneo hilo la ardhi zamani likitumiwa kwa shughuli za ufyatuaji Matofali lililojengwa ukuta wa matofali kati kati yake likiwa mashariki mwa Msikiti Mkuu wa Ijumaa uliopo Mtofaani makutano ya Bara bara za  Masingini  na Hawaii linakadiriwa kuwa na ukubwa wa eka Nne.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.