STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 1.11.2016

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza umuhimu wa viongozi katika Ofisi na Idara za
Serikali kuwa na utaratibu wa kufanya mikutano mara kwa mara na watendaji wao ili kuzungumza na
kujadili masuala yao ya kazi.
Dk. Shein aliyasema kuwa
hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kujua matatizo ya watendaji wao pamoja
na kukaa kwa pamoja kwa lengo la kujadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo
kwa haraka na hatimae kuweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar katika kikao maalum kati yake na uongozi wa
Ofisi ya Rais, na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wakati ilipowasilisha
Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa kipindi cha
Julai hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016-2017 ya Ofisi hiyo.
Katika maelezo yake, Dk.
Shein alisema kuwa ni jukumu kwa kila mkuu wa Idara kuwa na utaratibu huo kwani
utasaidia kwa kiasi kikubwa kupata maamuzi ya haraka sambamba na kuweza kufanya
kazi kwa pamoja hatua ambayo pia, hupunguza mivutano na hujenga mafahamiano
makubwa.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kuwa kukaa pamoja kati ya kiongozi na watendaji wake kunasaidia kwa
kiasi kikubwa kufikia muwafaka katika kujadili masuala mbali mbali ya
kiutendaji hali ambayo huzidisha mshikamano na kujenga udugu miongoni mwao.
Alisema kuwa hata
vikao vya taarifa za Mpango Kazi wa
Mawizara vinavyofanyika Ikulu Zanzibar vimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa
katika kuyapatia ufumbuzi wa haraka masuala mbali mbali ambayo yameweza
kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Alisisitiza kuwa hatua
hiyo haitopunguza ama kuondoa heshima kwa kiongozi na badala yake itazidi
kujenga heshima na mashirikiano ya karibu miongonimwao badala ya watendaji
kumuogopa kiongozi wao.
Hatua hiyo imekuja
baada ya uongozi wa Ofisi ya Faragha ya
Rais kuwa na utaratibu wa kukutana mara kwa mara na watendaji na kujadili
masuala mbali mbali ya kazi zao ambao ulipongezwa katika kikao hicho.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi
na watendaji wote wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa utendaji
wao wa kazi sambamba na kazi nzuri ya uwasilishaji na utekelezaji wa Mpango Kazi uliofanywa na Ofisi hiyo.
Nae Katibu Mkuu
Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee nae
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Ofisi hiyo na kuwataka viongozi na
watendaji wake kuwa kioo kwa watendaji na viongozi wa Wizara nyengine za
Serikali sambamba na kuionesha vyema taswira ya Rais.
Kwa upande wao,
Washauri wa Rais walitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi na watendaji wa
Ofisi hiyo kwa kuendeleza ushirikiano na mshikamano katika utendaji wa kazi zao
huku wakieleza umuhimu wa ziara za Pemba kwa viongozi wa Ofisi hiyo.
Mapema Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi Gavu akisoma taarifa ya Mpango Kazi wa Ofisi hiyo, na
kusema kuwa Ofisi ya Rais imedhamiria kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar ili
waishi kwa amani, mshikamano na upendo miongoni mwao.
Alisema kuwa dhamira
hiyo itafikiwa kwa kuhakikisha kwamba kunakuwa na mawasiliano ya karibu baina
ya wananchi na Mheshimiwa Rais, hali ambayo itaifanya jamii kuwa na imani na
Serikali yao na itapelekea kuimarika kwa amani, umoja na mshikamano.
Aidha, alisema kuwa
Ofisi itahakikisha kuwa Zanzibar inanufaika na uhusiano wa Jumuiya za Kikanda
na Kimataifa kama ilivyosisitizwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi 2015-2020.
Alieleza kuwa Ofisi
hiyo itahakikisha kuwa Idara inayoshughulikia masuala ya Diaspora inaimarishwa
kwa kuwa na watendaji wenye uwezo na kuweka mazingira mazuri kutendea kazi
ambapo pia uongozi wa Ofisi hiyo ulieleza juhudi zinazochukuliwa katika ujenzi
na ukarabati wa majengo ya Ikulu.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment