Habari za Punde

Ugonjwa wa kisukari ni miongoni mwa magonjwa hatari Visiwani

Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mnazi mmoja katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kisukari duniani.
Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.

Na Ramadhani Ali/Maelezo   
              
Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud  Thabit Kombo amesema hadi sasa hakuna dawa yoyote  duniani iliyothibitishwa  kutibu ugonjwa  wa kisukari na amewashauri watu waliopata maradhi hayo wawe karibu na madaktari kupata miongozo  sahihi itakayowasaidia kuimarisha afya zao

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mnazi mmoja katika kilele cha kuadhimisha siku ya kisukari duniani, Waziri Mahmoud amesema ugonjwa huo  ni hatari  na ni miongoni mwa magonjwa  makuu matano  yanayoongoza kwa kuuwa watu wengi Zanzibar.

Amesema kwa kawaida ugonjwa wa kisukari huchelewa kujitokeza dalili zake na zinapojitokeza tatizo tayari linakuwa kubwa hivyo amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kama kuna dalili zozote wapate ushauri wa kitaalamu na hatimae kuepusha athari zaidi.

Ameongeza kuwa maradhi ya kisukari yanaweza kukingwa kwa asilimia 80 iwapo wananchi watajiepusha na vihatarishi vinavyopelekea kupata ugonjwa huo.

Ametaja changamoto inayojitokeza katika maradhi hayo hivi sasa ni kuwa watoto wadogo nao wamekuwa wakipata ugonjwa huo kwa kasi na kwa mujibu wa takwimu wastani wa watoto 230 wamesajiliwa katika hospitali ya Mnazi mmoja na Abdalla  Mzee na zaidi ya watoto 20 wamepoteza maisha kati ya mwaka 2010 hadi 2015. 

Amesema tatizo jengine lililojitokeza kwa mujibu wa vipimo vilivyo fanywa katika Wizara nane za Serikali imegundulika  kuwa idadi kubwa ya  wafanyakazi wanakabiliwa na tatizo la maradhi ya kisukari.

Amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi na kuwa na utaratibu mzuri wa vyakula kwani ni moja kati ya tiba nzuri ya maradhi ya kisukari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.