Habari za Punde

Amchoma Kisu Kaka Ake Hatimae Kufariki Dunia Akikimbizwa Hospitalini.

Na Mwandishi Wetu Pemba. 

MTU mmoja Massoud Amour Seif (54) mkaazi wa Mtambile wilaya ya Mkoani Pemba, amefariki dunia baada ya kudaiwa kuchomwa kisu nje ya kituo cha Polisi cha Mtambile na ndugu yake wa damu, Kassim Amour Seif (43), baada ya kutokezea ugomvi wa wake zao.

Taarifa zinaeleza kuwa, wawili hao kabla ya mkasa huo, walianza kwa wake zao kugombana na kisha ugomvi huo kuhamia baina yao, na kupelekea marehemu kabla ya kufariki kupata majeraha na kupewa fomu ya Pf3 kwa ajili ya matibabu.

Imefahamika kuwa, baada ya kupata matibabu na kisha kwenda kituo cha Polisi kwa ajili ya maelezo ya kina, marehemu akiwa sambamba na mdogo wake, kisha walitakiwa warejee siku ya pili yake, na kujitokeza mkasa huo.

Mashuhuda wa tukio hilo wanaeleza kuwa, hatua chache kutoka kilipo kituo hicho cha Polisi, ndipo Kassim alipomrukia kaka yake na kumchoma kisu na kupoteza damu nyingi.

“Wakati Polisi wanamshughulika marehemu kwa tukio hilo, mpigaji kisu alichukua gari na kukimbilia eneo la barabara ya Wambaa, na mjeruhiwa kufarikia njiani akipelekwa hospitali”,alisema shuhuda huyo.

Aidha shuhuda Khamis Haji Omar, alisema tokea asubuhi ya tukio hilo, ugomvi wa wawili hao ulishaanza kwa muda mrefu, ikidaiwa kusababisha na watoto wao kuiibiana simu.

Nae shuhuda Mohamed Ali, alieleza kuwa baada ya kutokezea hali hiyo, iliosababishwa na watoto wao, ndipo wake zao nao walipoanza kutofahamiana na kisha kurukia na wanaume hao.

Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba, Sheihan Mohamed Sheihan alisema, kwa sasa wanaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo Kassim Amour Seif, na akipatikana atafikishwa mahakamani.

Alisema, kwa vile mtuhumiwa huyo baada ya kufanya tukio hilo alikimbia akitumia gari yenye namba za usajili Z 242 HI na kuelekea Wambaa, Jeshi lake lilivamia huko na baada ya kuona gari ya Polisi, mtuhumiwa aliamua kulitelekeza gari lake.

“Mtuhumiwa gari lake aliliawacha na kukimbia msituni, lakini sisi Jeshi la Polisi gari tunalo ambalo alilitumia Kassim, na sasa tumeshaweka mitego kila kona na akipatikana atajibu hoja’’,alifafanua.

Hata hivyo Kamanda huyo wa Polisi mkoani humo, amesema kwa sasa wanamshikilia kijana Mohamed Ali, ambae alikamatwa na pikipiki ikiwa na damu, akidaiwa kumsafirisha mtuhumiwa.

“Huyu kijana tunae na tunamuhoji, na tunamashaka nae kuwa ndie aliemsafirisha Kassim, ili kujihifadhi na hasa baada ya kulitekeleza gari lake, ili kuwakimbia Polisi’’,alifafanua.

Tukio hilo lilitokea Disemba 1 majira ya saa 12 :30 nje ya kituo cha Polisi cha Mtambile wilaya ya Mkoani mkoa wa Kusini Pemba, na likiwa la kwanza katika miaka ya hivi karibuni kuwahi kutokea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.