Habari za Punde

Balozi Seif ziarani India, China

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiagana na Viongozi wa Serikali kwenye uwanja wa ndege wa Zanzibar kwa ajili ya safari yake ya uchunguzi wa Kawaida wa Afya yake Nchini India na Baadaye kuelekea Jamuhuri ya Watu wa China kwa Ziara rasmi ya Kiserikali ya Siku Tano.

Wa kwanza aliyempa mkono ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Moh’d Mahmoud, Meya wa Manispaa ya Mjini Mstahiki Khatib Abdulrahman Khatib, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Zubeir Ali Maulid, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Mh. Said Hassan Said na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga
Meya wa Manispaa ya Mjini Mstahiki Khatib Abdulrahman Khatib  kati kati akimtakia safari njema Balozi Seif  wakati akiondoka uwanja wa Ndege wa Zanzibar katika safari  yake ya Uchunguzi wa kawaida wa Afya yake pamoja na Ziara rasmi Nchini India na China.

Wa kwanza kutoka Kulia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed  Mahmoud.

Picha na – OPMR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameondoka Zanzibar leo mchana kupitia Mjini Dar es salaam kuelekea Nchini India kwa safari ya uchunguzi wa kawaida wa Afya yake.

Mara baada ya kukamilisha shughuli ya uchunguzi wa afya yake Balozi Seif anatarajiwa kufanya ziara ya Kiserikali  ya Siku Nne Nchini China atakayofuatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mh. Mohamed Ahmed Salum.

Wengine atakaofuatana nao ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Nd. Khamis Mussa Omar, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Nd. Asha Ali Abdulla.

Akiwa Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar atapata fursa ya kutembelea Benki ya Kimataifa ya Exim na kufanya mazungumzo na Uongozi wa juu wa Benki hiyo yenye mafungamano na Zanzibar hasa katika Miradi mbali mbali ya Kimaendeleo.

Pia katika ziara hiyo Balozi Seif  atatembelea Makamo Makuu ya Kampuni ya Kimataifa ya Mitandao ya kisasa ya Mawasiliano ya ZTE  na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Kampuni hiyo inayosimamia  Mradi wa Mawasialiano  Serikalini { E. Government }.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ujumbe aliofuatana nao atamalizia ziara yake ya Kiserikali Dubai ambapo atapata fursa ya kufanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Biashara pamoja na kukutana na baadhi ya Viongozi wa Makampuni na Taasisi za Kibiashara watakaoonyesha nia ya kutaka kufungua milango ya Uwekezaji Miradi yao ya Kiuchumi na Biashara Visiwani Zanzibar.

Balozi Seif na Ujumbe wake anatarajiwa kurejea Zanzibar mnamo Tarehe 26 Disemba   2016  kuendelea kutekeleza  majukumu yake ya Taifa kama kawaida. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.