Habari za Punde

Kikao cha Kamati ya pamoja ya Serikali ya SMT na SMZ kuhusu masuala ya Muungano

 Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kati kati akikiongoza Kikao cha Kamati ya pamoja ya Serikali ya SMT na SMZ kuhusu masuala ya Muungano kilichofanyika katika ukumbi wa zamani wa Barazxa la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya pamoja kuhusu masuala ya Muungano kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya pamoja kuhusu masuala ya Muungano kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anayeshughulikia Mazingira na Muungano Mh. Januari Makamba  akiwasilisha Taarifa ya Maazimio ya Kikao cha  Mawaziri wa SMT na SMZ kwenye Mkutano huo.
 Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Juu wa Serikali zote mbili ile ya SMT na SMZ.

Kulia ya Mh. Samia ni Waziri Mkuu Mh. Mjaliwa Kassim Majaliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anayeshughulikia Mazingira na Muungano Mh. Januari Makamba .

Kushoto ya Mh. Samia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akizungumza na Wana Habari mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho cha Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ.

Picha na – OMPR – ZNZ

Na Othman Khamis, OMPR

Kikao cha kamati ya pamoja ya Viongozi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu masuala ya Muungano kimekutana chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan.

Wajumbe wa Kiko hicho ambao ni Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu , Watendaji na baadhi ya Wataalmu wa pande zote mbili za Tanzania walikutana katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Wawakilishi wa zamani uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Akiwasilisha Taarifa ya Maazimio ya Kikao cha  Mawaziri wa SMT na SMZ Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anayeshughulikia Mazingira na Muungano Mh. Januari Makamba  alisema kikao hicho kilijadili Agenda 10 na Mada Mbili.

Mh. Makamba alisema moja ya miongoni mwa  agenda  Kuu za Vikao hivyo ni ile ya chimbuko  la changamoto  za Muungano  ambazo baadhi  zilizokuwa  zikileta kero pande zote za Muungano tayari  zimeshapata ufumbuzi na nyengine ziko katika mchakato wa kuzitanzua.

Alisema ushiriki wa pamoja wa wataalamu na watendaji waandamizi wa pande mbili za Muungano katika vikao vya kujadili changamoto zinazolalamikiwa na sehemu zote husika kuanzia ngazi ya chini na kuwasilishwa kwa Makatibu Wakuu na hatimae Mawaziri wa pande hizo umesaidia kupunguza kero hizo.

Waziri Januari Makamba alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na usajili wa vyombo vya moto, Gharama za deni la Tanesco kwa Zeco, utumishi wa wafanyakazi wa Zanzibar kwa Taasisi za Muungano, uvuvi wa bahari kuu pamoja na Zanzibar kutofaidika na miradi iliyoanzishwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alieleza kwamba yapo baadhi ya masuala kimsingi yanayohitaji utaratibu wa kubadilishwa kwa baadhi ya Sheria kwenye Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na baadaye yaridhiwe na Baraza la Wawakilishi  akilitolea mfano lile la Uvuvi wa Bahari Kuu.

Akichangia kwenye kikao hicho Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Majaliwa Kassim  Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa kuandaa utaratubu mzuri wakati wa ujio wa Viongozi Wakuu wa Mataifa ya Nje wanaofanya ziara Nchini Tanzania na hatimae pia kufika Zanzibar.

Mh. Majaliwa alisema utaratibu huo ambao ulikuwa ukitumika siku za nyuma ni vyema ukawasilishwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili ipate fursa ya kujipanga mapema jinsi inavyoweza kufaidika na ujio wa Viongozi hao wa Kimataifa.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwaeleza wajumbe wa Kikao hicho kwamba katika azma ya kuhakikisha Muungano wa Tanzania unaimarika kwa pande zote mbili utaratibu wa Viongozi Wakuu wa Upande wa Tanzania Bara umeshaandaliwa wa kufanya ziara za kukagua miradi ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar.

Alisema wapo baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tayari wameshafanya ziara kama hizo hasa wale wanaohusika na Wizara za Muungano zenye Taasisi zake upande wa Zanzibar, akamtolea Mfano Waziri wa Mambo ya Ndani.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitahadharisha kwamba wapo baadhi ya watu wasioutakia mema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao tayari umeshatimiza miaka 53 sasa.

Balozi Seif alisema watu hao hutumia mapungufu na changamoto zilizopo katika baadhi ya kero za Muungano kwa kupotosha Wananchi kwa makusudi dhamira halisi na malengo la Muungano ambayo ni Umoja na Mshikamano wa Wananchi wa pande zote mbili.

Akikiahirisha Kikao hicho Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan alisema kitendo cha Serikali zote mbili kuwatumia Wataalamu wao katika ngazi ya msingi kwa kuzitafutia ufumbuzi changamoto za Muungano kimesaidia kuleta suluhu na ufumbuzi wa mambo mengi.

Hata hivyo Mh. Samia alisema kutokana na mabadiliko ya dunia yanayokwenda kwa kasi katika harakati za Kimaisha  katika mfumo wa teknologia ya Kisasa ya Habari na Mawasiliano changamoto za Muungano bado zitaendelea kuibuka nyengine.

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua iliyofikia ya kupitisha sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar baada ya Bunge  la Muungano kupitisha sheria ya kuiwezesha Zanzibar ijitegemee yenyewe katika masuala hayo.

Mh. Samia alieleza kwamba Wananchi wasingependa kuona suala la mafuta na Gesi asilia linarejea tena kwenye masulala yanayoleta kero ndani ya Muungano wa Tanzania.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.