Habiba Zarali ,Pemba.
WANANCHI kisiwani Pemba, wametakiwa kuendelea kubuni
miradi mbali mbali ya kimaendeleo inayoendana na mabadiliko ya tabia nchi, ili
miradi hiyo iweze kuwaletea tija na mafanikio wananchi hao .
Kauli
hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Luhaga Joelson Mpina, alipokuwa akikaguwa mradi wa kuvuna
maji ya mvua na mradi wa tuta la kuzuwia maji chumvi inayotekelezwa na mfuko wa
hifadhi ya jamii Tanzania (TASAF 3) kisiwani Pemba.
Akikaguwa
Tuta la kuzuwia maji ya mvua lenye ukubwa wa mita 200 lilioko Ndagoni Wilaya ya
Chake chake, Mpina aliwapongeza Tasaf 3 kuibuwa miradi inayoendana na
mabadiliko ya tabia nchi na mazingira na kusema itawawezesha wananchi kupambana na umaskini kwa kudhibiti
maji chumvi kutoingia katika mashamba hayo.
“
Mradi huu utawasaidia nyinyi wananchi wa Ndagoni kwa kuwaokolea mashamba
yenu na maji ya chumvi ambayo maji haya
kila uchao yanasogea katika makaazi yenu jambo ambalo linaleta athari
kubwa,”alisema.
Akikaguwa
mradi wa kuvuna maji ya mvua ulioko Kibokoni Vitongoji Wilaya ya Chake chake
Pemba, Mpina alisema bwawa hilo litaleta tija na mafanikio makubwa kwa wakulima
na wafugaji wa vitongoji.
“Kutokana
na ardhi hii ya Vitongoji mumefanya jambo la busara kubuni mradi huu kwani
kilimo na mifugo yenu itapata kunawiri kupitia bwawa hili”,alisema.
Alisema
miradi hiyo haina ubaguzi wa aina yoyote na dhamira yake ni kuhakikisha watu
wote wako sawa katika kipato chao, ili kila mmoja aweze kujikimu na maisha yake
ya kila siku.
Mapema
akitowa taarifa fupi ya mradi wa Tassaf 3, Kisiwani Pemba, Mratibu wa Tasaf 3, Mussa Saidi Kisenge,
alisema malengo ya mradi huo ni kuhakikisha unapomalizika wananchi wote wanaweza
kujitegemea wenyewe katika kujipatia kipato ndani ya maisha yao.
Alisema
miradi yote iliyotekelezwa imekamilika
na inafanya kazi kama ilivyokusudiwa na kuwaomba walengwa wa miradi hiyo
kujiekea malengo ya kujiekea akiba kama yalivyo malengo ya miradi hiyo.
“Miradi
hii kisiwani Pemba, inaendana na mahitaji husika ya wananchi wenyewe na eneo
husika kwani kila sehemu inahitaji mradi kulingana na eneo lilivyo,”alisema .
Kwa
upande wake Mkuu wa wilaya Chake chake, Salama Mbarouk Khatib, alisema lengo la
mradi huo ni kuhakikisha kaya maskini wanajipatia kipato na kuondokana na Umaskini.
Aliwataka
wananchi kushirikiana pamoja kwa kuwahimiza watoto wao kusoma pamoja na
kuwapeleka watoto Klinik ili azma ya Serikali ya watoto kusoma na kuhudhuria Klinik
iweze kufikiwa.
Hivyo
wananchi walio faidika na miradi hiyo waliishukuru Serikali ya Muungano kwa
kuona umuhimu wa kuwaletea wananchi miradi mbalimbali ambayo ni msaada katika
kuendesha maisha yao.
No comments:
Post a Comment