RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Rais wa Djbout Mhe.Ismail Omar Guelleh alipofika katika Ikulu ya Djbout leo akiwa katika ziara ya kiserikali na ujumbe wake
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akifuatana na Rais wa Djbout Mhe.Ismail Omar Guelleh alipofika katika Ikulu ya Djbout leo akiwa katika ziara ya kiserikali na ujumbe wake,Picha na Ikulu.07/05/2017
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Djibouti 7.05.2017

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya
Djibouti Ismail Omar Guelleh ambapo katika mazungumzo hayo viongozi hao
wamekubaliana kuanzisha uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo hasa katika
sekta za maendeleo na uchumi.
Viongozi walifanya
mazungumzo katika ukumbi wa Ikulu ya Djibouti ambapo Rais Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa Rais Guelleh kwa mwaliko wake huo
nchini mwake.
Katika mazungumzo hayo viongozi
hao kwa kauli moja walieleza haja ya kuanzisha uhusiano na ushirikiano katika
sekta mbali mbali za maendeleo na uchumi kwa manufaa ya pande mbili hizo.
Rais wa Djibouti Ismail
Omar Guelleh kwa upande wake alimuhakikishia Dk. Shein kuwa nchi yake iko
tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta za mawasiliano, utalii,
uwekezaji pamoja na usafiri na usafirishaji sambamba na utayari wa kujifunza
mambo mbali mbali kutoka Zanzibar ikiwemo sekta ya utalii.
Rais Guelleh, alieleza
kuwa nchi yake inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na
Tanzania ambao una historia nzuri na kueleza kuwa Djibout iko tayari kujifunza mbinu
zilizotumika na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii.
Ambapo pia, kiongozi
huyo alieleza utayari wa kushirikiana na Zanzibar kutokana na mafanikio
waliyoyapata na njia sambamba na mikakati waliyoitumia katika kufikia mafanikio
waliyoyapata na mikakati waliyoitumia kufikia mafanikio waliyonayo hasa katika
suala zima la uimarishaji wa bandari, mawasiliano na vitega uchumi.
Kiongozi huyo wa
Djibouti alimkaribisha Dk. Shein pamoja na ujumbe wake nchini humo huku
akisisitiza kuwa Tanzania na Djibouti zina ukaribu mkubwa na zimekuwa
zikishirikiana katika kupambana na uharamia wa baharini kupitia Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) na Mamlaka ya
Serikali ya Kimaendeleo (IGAD).
Aidha, Rais Guelleh alitumia
fursa hiyo kumueleza Dk. Shein mafanikio yaliyopatikana nchini mwake hasa
kutokana na uimarishaji wa bandari, mawasiliano na kueleza azma ya nchi yake
hivi sasa kujikita katika sekta ya utalii kutokana na baadhi ya vivutio
vilivyopo ikiwemo Ziwa Assal ambalo chimbuko lake ni Bonde la Ufa pamoja na
mambo mengineyo.
Hivyo kiongozi huyo
alimueleza Dk Shein kuwa pande hizo mbili zina mengi ya kujifunza kwa pamoja
kwani kila upande umeweza kupata mafanikio yake.
Kwa upande wake Rais Dk.
Shein, alitumia fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa Rais Guelleh kwa
mualiko wake huo aliompa pamoja na mapokezi makubwa aliyoyapata yeye na ujumbe
aliofuatana nao na kueleza kuwa ziara hiyo itakuwa ndio kichocheo kikubwa cha
mashirikiano kati ya Zanzibar na Djibouti.
Dk. Shein alimueleza Rais
Guelleh kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Djibouti hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo wa
kiuchumi inategemea sekta ambazo Zanzibar nayo imeamua kwa makusudi
kuziimarisha ili ziweze kuimarisha uchumi na kuleta tija.
Alizitaja miongoni mwa
sekta hizo ambazo Djibouti imepata mafanikio ni uendeshaji wa Bandari,mawasiliano
na Maeneo Huru ya Kiuchumi ambayo yamekuwa ndio kichocheo kikubwa cha uchumi wa
nchi hiyo.
Aidha, Dk. Shein alieleza
kuwa ziara hiyo ni kielelezo cha urafiki, heshima na udugu baina ya Serikali
zote mbili pamoja na wananchi wake ambapo itasaidia sana kuimarisha uhusiano na
kuibua maeneo mapya ya ushirikiano.
Katika maelezo yake, Dk.
Shein alimueleza Rais Guelleh kuwa Zanzibar katika ziara hiyo ina hamu kubwa ya
kufahamu maendeleo makubwa yaliyofikiwa na Djibouti tokea mwaka 1977 ilipopata
uhuru wake kutoka kwa Koloni la Kifaransa.
Dk. Shein alieleza kuwa
ana hamu kubwa kuona maendeleo yaliofikiwa na nchi hiyo katika sekta muhimu za
kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya bandari, kuendeleza maeneo Huru,
mawasiliano, uvuvi, viwanda, usafiri na usafirishaji, afya, elimu na sekta zote
muhimu za utoaji wa huduma kwa wananchi wa nchi hiyo.
Alipongeza juhudi kubwa
zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya nchi hiyo chini ya uongozi wa Rais
Guelleh ambazo zimepelekea Djibouti kuwa ni mfano mzuri kwa nchi za Afrika
ambazo zinatafuta maendeleo ya haraka, demokrasia pamoja na kuimarisha hali ya
utulivu na usalama wa nchi.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kumueleza Rais wa Djibouti mafanikio yaliopatikana kwa upande wa kisiasa
na kimaendeleo na kupelekea kuimarika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ambao ni Muungano wa mfano kwa bara la Afrika na kutoa salamu za Rais wa
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa kiongozi huyo.
Aidha, Dk. Shein
alimuhakikishia Rais huyo utayari wa Zanzibar kushirikiana na Djibouti na kutoa
uweledi wake katika sekta ya utalii kwa nchi hiyo kutokana na Zanzibar kupata
mafanikio makubwa katika sekta ya Utalii.
Pamoja na hayo, Dk.
Sheuin alimuelkeza Rais huyi wa Djibout hatua zinazoendelea kuchukuliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake ikiwa ni pamoja
na ujenzi wa Bandari mpya ya Mpiga Duri, mradi ambao utasaidia kwa kiasi
kikubwa kuongeza uingizaji wa mizigo na makontena na kuipunguzia mzigo Bandari
ya Malindi.
Aidha, alieleza azma ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuifanya Zanzibar kuwa na uchumi wa kati
ifikapo mwaka 2020, huku akitumia fursa hiyo kumualika kiongozi uyo wa Djibouti
kutembelea Zanzibar kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa pande mbili hizo.
Dk. Shein yupo nchini
Djibouti kwa ziara ya siku tatu kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Ismail
Omar Guelleh.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment