Maulid Khamis Ahmed alipokutana na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni
Na Zuhura Juma, PEMBA
“MTAJI wa masikini ni nguvu zake mwenyewe’’
Huu ni
msemo maarufu sana uliotumika zama za karne nyingi nyuma, ambapo mpaka sasa
unaendelea kutumika.
Sio
kama kila mwenye nguvu ameshajiwekea mtaji wake, hapana…, lakini msemo huu,
hutumika pale unapojikuta unajituma kufanya jambo ambalo litaweza kukukwamua na
hali ngumu ya maisha.
Maana hivi
sasa vijana wengi wameamua wakijiajiri wenyewe katika nyanja tofauti, kwa ajili
ya kujitafutia riziki ili kuona nao wanapata maisha bora
Kama
mwandishi wa makala hii alipokutana mjasiriamali maarufu katika mji wa Wete,
ambae hujishughulisha na mambo mbali mbali yanayomkwamua na umasikini, ikiwemo
ya uchukuaji picha (shooting).
Ni
kijana mtanashati mwenye umri wa miaka 28, mkaazi wa Utaani Wete ndani ya
kisiwa cha marashi ya karafuu cha Pemba, ambapo ni miaka saba sasa tokea kuanza
kazi ya uchukuaji picha.
Ni
Maulid Khamis Ahmed (LIDI) aliyevutika na fani ya uchukuaji picha za video,
ambayo kwa sasa ni shughuli yake kubwa inayompatia kipato.
“Fani
hii ndio shughuli yangu kubwa ambayo inanipatia tija kwa ajili ya kuendesha
maisha yangu”, alidakiza mjasiriamali huyo.
Lidi
alijikita katika kazi hiyo baada ya kushindwa kuendendelea na masomo ya chuo
kikuu mwaka 2009.
“Nilipomaliza
kidatu cha sita mwaka 2009 skuli ya Utaani, sikupata kuendelea na Chuo kikuu,
kutokana na familia yangu kuwa na uwezo mdogo kifedha, hapo niliamua nitafute
kitu chakufanya”, alieleza Lidi.
Kabla
ya kujiingiza katika kazi hiyo, Lidi alijiunga katika chama cha malezi bora
‘Umati’ tawi la Pemba, ambapo alikaa hapo na kutoa elimu kwa vijana wenzao kuhusiana na Ukimwi
pamoja na malezi bora.
Huku
akiwa yumo katika chama chicho, hakukaa kujipweteka (kutulia) tu, bali
aliutumia muda wake mwengine kwenda kujifunza uchukuaji wa picha za ‘movie ’
hapo hapo mjini Wete
.
Ilipofika
mwaka 2013 alianza kujichimbia kuisomea kazi ya kupiga picha kwa siku 90,
aliielewa vyema ingawa aliamua kujiendeleza na kujichukulia umaarufu ndani na
nje ya mji wa Wete.
“Sikukaa
tu nikajituliza Umati, bali niliamua nikajifunza uchukuaji wa picha na sasa
nashukuru maana huitwa sehemu mbali mbali katika shughuli kama za harusi”,
alieleza
Aliwataja
walimu waliomfundisha fani hiyo kuwa ni Sultan Ali Yussuf (Chani) na Saleh Mkubwa
Mjaa (Tizo), wote wakiwa wakaazi wa Wete Pemba, ambao aliwashukuru sana kwa
elimu waliyompa
“Baada
ya kuijua kazi hiyo, sikuwa mchoyo nikaona jambo la msingi nifundishe vijana
wenzangu, ninao wanafunzi wawili ambae ni Bashir Talib Khamis na Seif Bomoa”,
alieleza huku akitabasamu.
Huku
ukiwa uso wake unaonesha furaha kaka huyo, kwa sasa ameanzisha kampuni yake alioipa
jina la ‘MSUO VIDEO PRODUCTION WETE PEMBA’ yenye makao makuu yake Chupa la soda mjini Wete,
ambapo amewaajiri na wanafunzi wake.
Anasema
ingawa hutegemeana na mwenye shughuli kama ya harusi au maulidi, lakini
hujipatia kati ya shilingi 80,000 hadi shilingi 100,000 ambapo bei hiyo inaweza
kubadilika.
Pamoja
na kujikita katika fani hiyo, alivutika zaidi pale alipokuwa anachukua picha za
uigizaji wa filamu huko Wete.
“Nilipoanza
kuchukua picha za filamu, fani hii ilizidi kunivutia sana, kwani zimeweza kutoka
na nyengine zinaendelea”, alisimulia.
Lidi
baada ya kazi ya kupiga picha za video kumuingia magegoni, sasa ameshatanua
mbawa zake, na kuaminiwa hadi kushuti hata michezo ya kuigiza.
“Kila
nikichukua picha za harusi, maulidi, sherehe za kuzaliwa au mikutano, ndio
napata umaarufu na fani imenikaa hasa moyoni na niko ‘fiti’, alijigamba.
Filamu
ambazo aliweza kuzishuti ni pamoja na ‘NENO SAMAHANI, SABABU MAISHA YANGU, UCHUNGU
WA MWANA KWA MZAZI, TAMIMA NA THE STRESS (MAWAZO)’ ambazo tayari zimeshatoka
na cd zake kuuzwa.
Filamu
nyengine ambayo anaendelea nayo kuishuti
kwa muda huu ni pamoja na ‘PENZI LA MUUNGANO’ ambapo waandaji wa mchezo
huo ni waigizaji kutoka vikundi tofauti vya mji wa Wete.
Lidi
anaeleza kuwa kuna tofauti ya kushuti filamu za mikutano au harusi, kwani
filamu unatumia aina ya picha nzima ‘long short, au kipiande ‘medium na za
ukaribu mno ‘close up’, ambapo mikutano na harusi unapiga picha nzima ‘long
short’.
Tabu
anayoipata Lidi wakati wa kushuti mchezo wa kuigiza ni ukaidi kwa wasanii
wakati wa kuongoza na kuchelewa kufika kwenye maeneo (location) wanayotumia.
“Wasanii
baadhi yao wanakuwa wakaidi wakati wa kuongoza, kwani unapomwambia fanya hivi…..
yeye anaona kama unamuhangaisha”, alieleza.
Kushuti
mchezo mmoja wenye sehemu mbili (part one na two) huchukua muda wa wiki mbili
ingawa inategemea wepesi wa wasanii au mpiga picha mwenyewe.
Utaalamu
kwa vile ni jambo la lazima popote, nae Lidi anasema, unatumika katika kushuti
mchezo au jambo jengine, ikiwa ni pamoja na kuangalia kamera mara kwa mara.
Jengine
la msingi anaona ni kuangalia kila wakati aina ya picha ili usiirudie kwa
mtendo moja, kufahamu kipande au sehemu wanayoigiza wanapokuwa jukwaani (sini)
na kupiga shoti kila sini.
Kijana
huyo anasema wakati mzuri wa kushuti mchezo ni muda wa asubuhi kabla ya jua
kuwa kali, au jioni jua linapoanza kuzama taratibu.
“Au
inategemea muongozo wa sini unazotaka kuzishuti kwa sababu pengine wanapenda
kipande kionekane jua kali au mvua”, anaeleza.
Yeye
anaposhuti michezo lazima aandae muongozo (script), kwani humsaidia na
kumrahisishia kazi yake hiyo bila ya matatizo.
Anafahamisha
kuwa, anaporudi kushuti mchezo (filamu) huhifadhi kazi yake katika kompiyuta,
ambapo pia humo ndimo anapotengenezea kazi yake hiyo.
Pamoja
na hayo, lidi hakuacha kusema tatizo analoliona kwa wasanii wakati wa kushuti,
kuwa ni pale wanapoongea vile walivyopangiwa mwanzo na
wakati wa kushuti kubadilisha maongezi.
Lidi
anasema kushuti mchezo hadi kumalizika ni wastani ni shilingi 800,000 (ahilingi
laki nane) ingawa kwa Pemba ni kinyume chake kwani yeye hulipwa chini ya kiwango
hicho.
Kuna
mafanikio mbali mbali aliyoyapata Maulid katika fani hiyo ikiwa ni pamoja na
kupata fedha za kujikimu na maisha, kupata umaarufu, kutembea sehemu tofauti
nje ya Zanzibar ikiwemo Tanga, Dar-es-salaam, Arusha na Nairobi.
Kila
penye mafanikio hapakosi kuwa na matatizo, Lidi anakabiliwa na changamoto ya
upungufu wa vifaa vya kufanyia kazi, jambo ambalo linamkwaza katika kazi yake.
Changamoto
nyengine inayomkabili ni kukosa usafiri wa kwenda katika shughuli yenyewe,
ambapo hutembea masafa marefu mpaka kufika sehemu yenye shughuli
.
“Sehemu
nyengine hazina usafiri hivyo hulazimika kupiga mguu, pia ni unaweza kupata
mtetemo (shoti) wakati wa kupanga vifaa na wakati mwengine kugombana na wateja
kwa malipo”, alieleza Lidi.
“Mtu
anakwita ukamchukulie picha katika shughuli yake, lakini cha kushangaza wakati
wa malipo wanakuwa wagumu mno, jambo ambalo linarejesha nyuma’’,alifafanua.
Katika
siku aliyokuwa hatoisahau maishani yake kwenye fani hiyo, ni pale alipopata hitilafu
‘short’ ya umeme katika Ukumbi wa Jamhuri Wete wakati wa kupanga, ambapo
alipata majeraha ya kuungua ingawa sio sana.
Kijana
huyo alitoa hisia zake kuwa, malengo yake ya baadae ni kukikuza zaidi kipaji
chake hicho na kuona kwamba anapata maisha mazuri ya baadae.
Pamoja
na kazi ya uchukuaji picha, Lidi pia ni mjasiriamali, muigizaji wa filamu za Kiswahili na muelimishaji rika katika chama cha malezi
bora ‘Umati’ tawi la Pemba.
Alitoa
wito kwa vijana wenzake kuwa, waweze kujiajiri wenyewe bila ya kutegemea
serikali, kwani haina uwezo wa kuajiri watu wote nchini.
Muigizaji
Rabia Suleiman Salum mkaazi wa Jadida Wete anasema Lidi ni mpiga picha mzuri,
ambaye wanampenda sana katika kikundi chao cha uigizaji cha ‘Msuo Group’
Bashir
Talib Khamis ambae ni mwanafunzi wa Lidi alimsifu mwalimu wake kwa ushirikiano
anaouonesha wakati alipokuwa akiwafundisha na hata sasa katika utendaji wa kazi
zao.
“Mwalimu
wetu yuko vizuri sana, katufundisha kwa nia njema kabisa na sasa ametuajiri
katika kampuni yake ya MSUO tunafanyakazi kwa pamoja” alisifu Bashiri.
Mmoja
wa mwalimu aliyemsomesha Lidi, Sultani Ali Yussuf (Chani) anasema kijana huyo
alimsomesha fani ya uchukuaji picha kwa muda mdogo sana, ambapo kwa sasa
anafanya shughuli zake bila kuongozwa.
“Lidi
ni kijana mzuri sana, mstahamilivu na mimi mpaka sasa nikiwa na kazi yangu
naweza kumtuma na wala hakatai, hilo nimejivunia kama mwalimu”, alijinadi
mwalimu huyo.
Chani
aliiomba serikali iwaangalie vijana wanaojitolea kama Lidi na kuwawezesha kwa
kuanzisha taasisi ambazo zitaweza kuwakwamua na umasikini kwa kupewa mikopo.
Lidi ni
mzaliwa wa Mtambwe Kele shehia ya Mtambwe Kaskazini Wilaya ya Wete Pemba, akiwa
mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya watu wanne.
Amepata
elimu yake ya msingi katika skuli ya Uondwe Mtambwe na kufaulu michepuo, ambapo
alijiunga katika skuli ya sekondari Utaani na kumaliza kidatu cha sita.
Alipofika
umri wa miaka 31, Lidi alilihama jumba la upweke, na kufunga ndoa na mwandani
wake kutoka wilaya ya Mkoani, na leo Allah ameshampa mtoto mmoja wa kike.
Kwa
sasa anaishi mtaa wa Kipangani mji maarufu kwa halua, wa Wete na anasema hulala
jicho moja na la pili kusikiliza wapi kuna shuguli za kupiga picha za video ili
nae mkono uwende kinywani.
No comments:
Post a Comment