STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 01.09.2017
OFISI ya Mufti na viongozi wa dini hapa nchini
wametakiwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanikisha
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Zanzibar wa miaka mitano wa kupambana na vitendo
vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.
Hayo yameelezwa leo na
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed
Shein, katika hotuba yake ya Baraza la Idd el Hajj, aliyoitoa huko Fumba,
Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja katika eneo la nyumba
za mradi wa Makampuni ya Said Salim Bakhressa.
Hafla ambayo
ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Makamu Pili wa Rais Zanzibar Balozi
Seif Ali Idd na viongozi wengine wa dini na Serikali pamoja na wananchi.
Alhaj Dk. Shein alisema
kuwa Ofisi ya Mufti ni vyema iwe inavifuatilia kwa karibu vyuo vyote vya Qur-an
ikiwemo kuvijua mahali vilipo, walimu wanaofundisha katika vyuo hivyo pamoja na
kujua sifa zao.
Alieleza kuwa hatua hiyo
itasaidia kuwadhibiti walimu wachache wanaokiuka misingi na maadili mema wakati
wa utekelezaji wa majukumu yao na kutoa nasaha kwa Mashehe na Maimamu wote
kufanya juhudi za kuielimisha jamii juu ya Mpango huo kupitia mawaidha
wanayotoa misikitini na katika hotuba za sala ya Ijumaa.
Kadhalika, Dk. Shein
alieleza kuwa viongozi wa dini nyengine nao wana jukumu la kuwaelimisha wafuasi
wa dini zao na jamii nzima kwa jumla juu ya umuhimu wa kufuata maadili mema na
kuepuka vitendo viovu vya udhalilishaji wanawake na watoto.
Katika jitihada za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kupambana na vitendo vya udhalilishaji,
wiki iliyopita tarehe 26 Agosti, 2017, Dk. Shein alizindua Mpango Kazi wa
Zanzibar wa miaka 5 wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji dhidi
ya Wanawake na Watoto unaoanza mwaka huu hadi mwaka 2022.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa jamii kwa pamoja
ina wajibu wa kuchukua hatua kwa kushirikiana na Masheha pamoja na vikundi vya
ulinzi shirikishi na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha vitendo vya
vijana kuwasumbua wananchi hasa wanawake kwa kuwavamia na kuwanyanganya vitu vyao,
vinakomeshwa.
Aliongeza kuwa zipo
taarifa za kuongezeka kwa vitendo vya wizi wa mifugo, mazao pamoja na uchimbaji
ovyo wa mchanga katika maeneo yasioruhusiwa, vitendo ambavyo vinafanywa na
vijana waliokosa maadili bora na malezi mema vinahatarisha amani na usalama wa
wananchi na mali zao pamoja na uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wa ukusanyaji
wa mapato hapa nchini, Alhaj Dk. Shein ameendelea kusisitiza haja kwa wafanyabiashara
kutoa risiti na wananchi nao kudai risiti wakati wa kuuza na kununu bidhaa
kwani hivyo ndivyo ilivyo sheria.
Alisema kuwa Uislamu
umehimiza uadilifu katika biashara kwa hivyo utoaji wa risiti sahihi ni kitendo
cha kufanya uadilifu kati ya muuzaji na mnunuzi, na kutoa wito kwa Bodi ya Mapato Zanzibar
(ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu
ya umuhimu wa kutoa risiti kwa mauzo wanayoyafanya.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa Mikoa yote kwa juhudi
wanazozichukua katika kuijenga nchi yao, kuimarisha mshikamano pamoja na
kudumisha amani na utulivu hali ambayo aliiyona katika ziara yake hivi karibuni.
Aidha, aliwapongeza
viongozi walioshiriki katika kuifanikisha ziara hiyo katika Mikoa yote na
Wilaya za Unguja na Pemba kuanzia Agosti 12 hadi 26 kwa madumuni ya kuona na
kufahamu juhudi za utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka
2015-2020 na mipango mengine ya Maendeleo iliyopangwa kuwatumikia wananchi na
kuwaletea maendeleo.
Alhaj Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa vyombo vya habari kwa kufuatilia kwa karibu zaidi
ziara za Mikoa na kuwapa wananchi taarifa kwa wakati juu ya matukio mbali mbali
ya ziara za mikoa alizozifanya.
Alhaj Dk. Shein, alitoa
pongezi kwa uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi na Wilaya zake, taasisi na
vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi wote kwa jitihada zinazochukuliwa
katika kusimamia amani na utulivu.
Akitoa nasaha zake kwa
wananchi, Alhaj Dk. Shein alitaka jitihada hizo ziwe za kudumu na wananchi
waendelee kushirikiana na Serikali kwani jukumu la kusimamia amani na usalama
ni la kila raia mwema na sio viongozi wa serikali na vyombo vya ulinzi peke
yao.
Alisisitiza kuwa
Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar zote kwa pamoja zitaendelea kuhakikisha kuwa wananchi na mali zao
na wageni wanaoitembelea Tanzania wapo salama na wanaendelea kufanya shughuli
zao bila ya hofu.
“Bila ya amani hakuna
maendeleo, bila ya amani watu watashindwa hata kufanya ibada jambo ambalo
tumekuwa tukikumbusha kila tunapopata wasaa kutokana na umuhimu wake…tumuombe
Mwenyezi Mungu aendelee kutukirimu neema”,alisema Alhaj Shein.
Aidha, Alhaj Dk. Shein
alieleza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kudhibiti na kupambana
na uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya na kuwaomba wananchi
kuendelea kushirikiana na vyombo husika ili kuzidi kuwaokoa vijana
wanaoathirika na dawa za kulevya na ukimwi.
Alhaj Dk. Shein
alisisitiza haja ya kuongeza jitihada katika kupeana elimu sahihi juu ya
maambukizo ya virusi vya UKIMWI, kutoa huduma nzuri kwa walioathirika,
kukomesha unyanyapaa pamoja na kuzilinda haki za waathirika.
Aliongeza kuwa bado
tatizo la UKIMWI lipo ambapo Zanzibar hivi sasa ina watu 15,122 wanaoishi na
virusi vya UKIMWI, idadi ambayo inakadiriwa kuwa sawa na asilimia 1 ya idadi ya
Wazanzibari wote.
Mapema asubuhi aliungana
na Waumini wa dini ya Kiislamu katika
sala ya Idd el Hajj katika uwanja wa mpira Dimani, Wilaya ya Magharibi
‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi na baadae alikutana na kusalimiana na Mashekh
pamoja na viongozi mbali mbali katika ukumbi wa moja wapo ya nyumba za mradi wa
Makampuni ya Said Bakhressa na kumpongeza mfanyabiashara huyo kwa kukubali eneo
hilo kufanyika shughuli hizo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment