STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
26.10.2017

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa Uchumi wa Zanzibar unazidi
kuimarika siku hadi siku kutokana na uongozi uliopo kuwa na mashirikiano ya
pamoja katika kutekeleza mikakati iliyowekwa na Serikali.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar
alipokutana na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakati ilipowasilisha
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2016/2017, Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa
mwaka 2017/2018 na Utekelezaji wake kwa
kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba, 2017.
Dk. Shein alieleza kuridhishwa na hatua zinazoendelea
kuchukuliwa na uongozi wa Wizara hiyo katika kuhakikisha mapato yanaimarika na
nchi inaendelea kupata maendeleo endelevu na kutumia fursa hiyo kuzipongeza
juhudi hizo.
“Endeleeni na juhudi zenu, mmejitahidi sana na
kila mmmoja ametekeleza wajibu wake, na kwa vile mmefanya kazi wka pamoja
mmeona matokeo yake”alisema Dk. Shein.
Aliongeza kuwa leo Zanzibar inasifiwa duniani kote
kwa kuanzisha Penjeni jamii kwa wananchi wake waliokusudiwa, ambapo kila mwezi kiwango
cha fedha maalum kimetengwa kwa ajili ya malipo hayo.
Alieleza kuwa katika kipindi hichi Serikali
imetangaza kuondoa michango ya wazee kwa watoto wao skuli, kutokana na Setikali
kujipanga vyema kifedha ikiwa ni pamoja na kuendeleza juhudi zile zile
zilizochukuliwa katika ununuzi wa meli ya MV Mapinduzi II jambo ambalo
limewezekana.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza kwua Serikali
itahakikisha inapata mafanikio ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inaendelea kuyatekeleza
yale yote yaliyoasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
afya pamoja na elimu vinatolewa bure.
Pamoja na hayo, Rais aliuagiza uongozi wa Wizara
ya Fedha kulishughulikia suala la msongamano wa wananchi katika kupata huduma
za Benki jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wananchi kwa kipindi kirefu na
tayari ameshaawahi kulitoa agizo katika hotuba zake mbali mbali.
Dk. Shein alisisitiza kuwa licha ya changamoto
chache zilizopo katika sekta ya afya na elimu lakini bado Zanzibar imeweza
kupiga hatua kubwa katika sekta hizo ikilinganishwa na nchi nyenginezo za bara
la Afrika.
Alieleza kuwa suala zima la utegemezi wa Bajeti ya
Zanzibar imeweza kupata mafanikio na hivi sasa utegemezi umefikia asilimia 7.2
ikilinganishwa na wakati anaingia madarakani mwaka 2010 ambapo utegemezi
ulikuwa asilimia 32.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kufanywa utafiti na iwapo
Wizara itafanya utafiti itasaidia kwa kiasi kikubwa kupata majibu ambayo huwa
magumu kupatikana na ndio maana Serikali ikaunda Idara ya Mipango Sera na
Utafiti kwa kila Wizara kwa lengo la kupanga mipango ya maendeleo.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza Wizara hiyo pamoja na taasisi
zake zote kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata huku akisisitiza haja ya
kuviangalia viinua mgogo.
Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Dk. Khalid
Salum Mohamed alieleza kuwa uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika mwaka hadi
mwaka sambamba na kasi ya ukuaji uchumi kuimaika zaidi na kufikia asilimia 6.3
ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 5.2 kwa kipindi kama hicho cha
robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2016.
Aliongeza kuwa hali hiyo imetokana na kuimarika
zaidi kwa sekta ya huduma hususan katika sekta ndogo ndogo ya huduma za hoteli
na mikahawa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii walioingia nchini.
Dk. Khalid alieleza kuwa Wizara inaendelea na jitihada zake za
kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kusimamia vyema Sheria ikiwemo Sheria
mpya za Fedha za Umma na Ununuzi na Uondoshaji wa Mali za Serikali na kusimamia
matumizi ya fedha hizo za umma.
Wizara pia, itaendelea kufuatilia utekelezaji wa
Miradi ya maendeleo na kushauri hatua za kurekebisha pale zinapojitokeza
kasoro.
Waziri Khalid alieleza kuwa Wizara inashukuru sana
imani inayoendelea kupata kutoka kwa
Rais Dk. Shein pamoja na Makamo wa Pili Balozi Seif Ali Idd na kuongeza
kuwa miongozo ya Serikali imeendelea
kurahisiaha utekezaji wa majukumu ya Wizara.
Sambamba na hayo, uongozi huo ulieleza kuwa tayari
umeshaanza kulishugulikia tatizo la msongamano wa watu katika kupata huduma za Benki
kwa kuchukua hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za malipo
kwa njia za mitandao ya simu, pamoja na kukamilisha taratibu zitakazowesha
huduma hizo kutolewa na mawakala wa huduma za simu.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment