Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akisalimiana na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshuhulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Bw.Stephen B.Kargo alipofika Ikulu Mjini Unguja leo
Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akizungumza na mgeni wake Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshuhulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Bw.Stephen B.Kargo alipofika Ikulu Mjini Unguja leo
Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akifuatana na mgeni wake Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshuhulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Bw.Stephen B.Kargo baada ya mazungumzo yao alipofika Ikulu Mjini Unguja leo,[Picha na Ikulu.] 17/10 /2017.
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 17.10.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza haja kwa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kuendelea kuiunga mkono Zanzibar
katika kuimarisha sekta ya viwanda hatua ambayo itawasaidia hata vijana
kujipatia ajira pamoja na kukuza pato la taifa.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Stephen Kargbo
Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya
Viwanda (UNIDO).
Katika mazungumzo hayo, Dk.
Shein alimueleza Mwakilishi Mkaazi huyo kuwa kwa kutumia uzoefu na utaalamu wa
Shirika hilo, ni vyema likaishauri na kuisaidia Zanzibar katika kutekeleza azma
yake ya kuimarisha sekta ya viwanda hasa vidogo vidogo sekta ambayo iwapo
itatiliwa mkazo itasaidia kukwamua changamoto ya ajira kwa vijana.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kumueleza Mwakilishi huyo Mkaazi mikakati pamoja na malengo ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo Dira ya Maendeleo ya 2020, MKUZA III, katika
kupambana na umasikini sambamba na tatizo la ajira kwa vijana.
Dk. Shein alilipongeza
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa ambalo limekuwa na historia kubwa ya
mashirikiano kati yake na Zanzibar kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha sekta zake za maendeleo.
Aidha, Dk. Shein alieleza
haja ya kuungwa mkono wakulima wa zao la mwani kutokana na zao hilo kuwa na bei
ndogo jambo ambalo limekuwa likiwarejesha nyuma wakulima wa zao hilo
ambalo kwa upande wa Zanzibar nchi ya
tatu duniani kuzalisha zao hilo.
Kutokana na uzoefu wa
Shirika hilo, Dk. Shein alieleza haja kwa UNIDO kushirikiana na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Taasisi zake ili kuweza kusaidia mbinu na maarifa
katika kufanikisha sekta hiyo ya viwanda.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alimueleza Mwakilishi huyo kuwa katika kutekeleza Uchumi wa Bahari,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika hatua ya kuanzisha Kampuni ya
uvuvi, ambapo Serikali itaanza kwa kununua meli mbili za uvuvi, hatua ambayo
pia itatekeleza malengo ya Jumuiya ya nchi zilizopakana na Bahari ya Hindi
(IORA).
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa Serikali imekuwa ikiimarisha sekta ya utalii, ikiwa ni
mbadala wa sekta ya kilimo, sekta ambayo itapata mafanikio mazuri iwapo sekta
ya viwanda itaimarika zaidi kwani utalii umeweza kuchangia fedha za kigeni kwa
asilimia 80.
Nae Mwakilishi Mkaazi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO),
Stephen Kargbo alimueleza Dk. Shein kuwa kipaumbele kikubwa kilichowekwa na
Shirika hilo hivi sasa ni uimarishaji wa viwanda hasa kwa nchi za bara la
Afrika, na kuahidi kuiunga mkono
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta hiyo.
Katika maelezo yake
Mwakilishi huyo Mkaazi alimueleza Dk. Shein hatua na mikakati iliyowekwa na
Shirika hilo katika kusaidia sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya viwanda na
kueleza hatua zitakazochukuliwa na Shirika hilo kwa upande wa Zanzibar.
Aliongeza kuwa UNIDO ina
mipango kabambe katika kuiunga mkono Zanzibar ili iweze kupiga hatua katika
azma yake ya kuimarisha sekta ya viwanda.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alikutana na Balozi
wa Uganda nchini Tanzania Richard Mabonero, Ikulu mjini Zanzibar ambapo katika
mazungumzo yao viongozi hao walisisitiza haja ya kuendeleza na kuimarisha
uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo.
Katika maelezo yake Dk.
Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Uganda imekuwa na mashirikiano mazuri na
Tanzania hasa katika sekta ya elimu kwani nchi za Afrika Mashariki ikiwemo
Tanzania kabla ya kuwa na vyuo vyake vikuu Watanzania walio wengi wamepata
elimu yao ya juu kutoka Chuo Kikuu cha Makerere cha nchini humo.
Aidha, aliipokea rai ya
Balozi Mabonero ya Zanzibar kuisaidia nchi hiyo katika kuiimarisha lugha ya
Kiswahili kwa kuwapatia walimu huku Dk. Shein akisisitiza haja ya kuwepo kwa
mashirikiano katika kubadilishana uzoefu na utaalamu kati ya vyuo vikuu vya
Uganda na vyuo vikuu vya Zanzibar kikiwemo chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
(SUZA).
Dk. Shein alisema kuwa
kuwepo kwa usafiri wa ndege kati ya Uganda na Zanzibar kutaimarisha sekta ya
utalii kwa pande zote mbili huku Rais Dk. Shein akitumia fursa hiyo kumpongeza
Rais Yoweri Kaguta Museven kwa kufanikisha nchi yake kutoa mafuta na gesi.
Nae Balozi huyo wa
Uganda nchini Tanzania Richard Mabonero alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa
mafanikio makubwa yaliopataikana hapa Zanzibar na kueleza kuwa nchi yake
itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Tanzania
ikiwemo Zanzibar.
Balozi huyo alisisitiza
haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Zanzibar na Uganda hasa
katika usafiri wa ndege sambamba na kutoa ombi maalum la kutaka kusaidiwa
kukiendeleza na kukikuza Kiswahili nchini mwao kwa kupata wakufunzi kutoka
Zanzibar kwa kutambua kuwa Zanzibar ndio chimbuko la lugha ya Kiswahili.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment