Habari za Punde

Serikali imo katika hatua za mwisho ujenzi wa Barabara - Kinyasini

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                               7.10.2017
---
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa imo katika hatua za kuendelea kukamilisha taratibu zilizobaki ili kuanza ujenzi wa barabara ya Bububu-Kinyasini hadi Mkokotoni, ujenzi ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo katika hotuba yake wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bandamaji, Mkoa wa Kaskazini Unguja, pamoja na waumini wa dini ya Kislamu waliofika kijiji hapo kwa ajili ya ufunguzi wa msikiti wa Saeed Al Bawady, ambapo Dk. Shein alikuwa mgeni rasmi.

Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein alisema kuwa ndani ya kipindi cha wiki mbili Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inategemea kukamilisha hatua ya utiaji saini wa mikataba na Wakandarasi.

Dk. Shein alieleza kuwa hivi sasa tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshalipa fidia katika Shehia nyingi ambazo barabara hiyo inapita na imo katika matayarisho ya kulipa wahusika katika Shehia 5 tu zilizobaki ambazo ni Kinyasini, Chaani Masingini, Mkwajuni, Kivunge na Mkokotoni.

Aliongeza kuwa matayarisho ya kulipa fidia kwa Shehia hizo zilizobakia yanakwenda vizuri kwa lengo la kurahisisha ujenzi wa barabara hiyo muhimu.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa ujenzi wa barabara ya Bububu-Kinyasini hadi Mkokotoni utaanzia huko maeneo ya Chuini, Wilaya ya Magharibi ‘A’, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akiwa katika ziara zake za kuitembelea Mikoa na Wilaya zote za Unguja na Pemba mnamo mwezi wa Agosti mwaka huu, mara baada ya kuweka jiwe la jiwe la msingi katika Mradi wa Soko la Kinyasini, Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa Mkoa huo azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuijenga barabara hiyo ambapo kumalizika kwake kutasaidia kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Mkoa huo.

Kukamilika kwa ujenzi huo kutawasaidia wananchi wa Mkoa huo wa Kaskazini Unguja pamoja na mikoa jirani kupata kufaidika na huduma ya miundombinu bora ya barabara kwa ajili ya usafiri sambamba na kuwasaidia katika shughuli zao za maendeleo zikiwemo za kilimo, biashara pamoja na kuimarisha sekta ya utalii.

Sambamba na hayo, katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa Mkandarasi atakaejenga barabara hiyo ndiye atakaejenga barabara tatu nyengine ambazo ni barabara ya Matemwe hadi Muyuni, Pale Kiongele hadi Mkwajuni na Fuoni hadi Kombeni.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.