STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
27.11.2017

SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China imeahidi kuendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo ukiwemo
ukamilishaji ujenzi wa jengo jipya la abiria la uwanja wa ndege wa Abeid Amani
Karume pamoja na ujenzi wa bandari mpya ya Mpigaduri ili kukuza uchumi wa
Zanzibar.
Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania Mhe.
Wang Ke, aliyasema hayo leo wakati alipofika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya
kujitambulisha pamoja na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein.
Katika mazungumzo
hayo, Balozi Wang Ke alimueleza Dk. Shein kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China itahakikisha inatoa ushirikiano katika kutekeleza miradi hiyo mikubwa
katika taratibu zote zilizopangwa kwa lengo la kuendeleza na kukuza uhusiano na
ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Jamhuri ya Watu wa China.
Balozi huyo alimueleza
Dk. Shein kuwa nchi yake itahakikisha mradi wa ujenzi wa jengo la abiria katika
uwanja wa ndege wa Kimatifa wa Zanzibar unakamilika katika kipindi kifupi
kijacho huku akisisitiza kuwa mradi wa ujenzi wa bandari ya Mpigaduri nao
utatekelezwa kama ulivyopangwa.
Aidha, Balozi Wang Ke,
alimuhakikishia Dk. Shein kuwa China itaendelea kuisaidia na kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake ikiwa ni pamoja na kuahidi kuleta wawekezaji
kwa ajili ya kujenga viwanda vinavyotokana na rasilimali za bahari kwa lengo la
kukuza sekta ya uvuvi na sekta ya viwanda hapa nchini.
Pamoja na hayo, Balozi
huyo alimuhakikishia Dk. Shein kuwa mara baada ya kumalizika kwa miradi hiyo
nchi yake itakuwa tayari kuunga mkono katika kuanzisha miradi mipya mengine
mikubwa hapa Zanzibar kwa siku za usoni kwa ajili ya kuimarisha uchumi na
maendeleo endelevu hapa Zanzibar.
Pia, Balozi huyo
alitumia fursa hiyo, kumpsa salamu Dk. Shein zinazotoka kwa Rais wa Jamhuri ya
Watu wa China Rais Xi Jinping, zinazompongeza Rais Dk. Shein pamoja na wananchi
wa Zanzibar huku akiahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta mbali
mbali za maendeleo.
Balozi Wang Ke,
alipongeza mashirikiano yaliopo katika kuimarisha sekta ya afya ambapo nchi
yake imesaidia ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee huko Pemba, kuendelea kuleta
Madaktari kwa awamu kutoka nchini humo na kuahidi kuendeleza mashirikiano
katika sekta za elimu, kilimo, uvuvi, miundombinu,viwanda na nyenginezo.
Nae Rais Dk. Shein kwa
upande wake alimpongeza Balozi Wang Ke pamoja na nchi yake na kusisitiza kuwa
Zanzibar itaendelea kufuata misingi iliyowekwa na waasisi wa nchi hizo akiwemo marehemu
Maotse Tung, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume ambao bado juhudi zao zinathaminiwa.
Dk. Shein alisema kuwa
ni miaka 54 tokea Zanzibar na China zianzishe ushirikiano na uhusiano wao wa
kihistoria Zanzibar ambapo mafanikio makubwa yameweza kupatikana huku akieleza
kuwa kukamilika kwa jengo hilo la abiria katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Zanzibar kutaimarisha uchumi na kukuza sekta ya utalii.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alisema kuwa China
imekutoa mchango mkubwa katika kufanikisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya
afya, viwanda, kikiwemo kiwanda cha sukari, elimu, michezo, kilimo cha mpunga na
kueleza haja ya kwa nchi hiyo kuanzisha viwanda vitakavyotokana na rasilimali
ya bahari hapa Zanzibar.
Aliipongeza Serikali
ya China chini ya kiongozi wake Rais Xi Jinping kwa kuendelea kuisaidia na
kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo na
kuipongeza nchi hiyo kwa mafanikio inayoendelea kuyapata.
Wakati huo huo, Rais Dk. Shein
alikutana na Balozi wa Tanzania nchini
Misri Jenerali Issa Suleiman Nassor na Balozi Tanzania nchini Zambia Mhe.
Abrahman Kaniki, waliofika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kuaga.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein aliwasisitiza Mabalozi hao kulipa kipaumbele suala zima la
uchumi wa kidiplomasia hasa kwa vile Tanzania ikiwemo Zanzibar imejikita katika
kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda.
Pia, alitilia mkazo
makubaliano ya mkutano wa Jumuiya ya
Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA) uliofanyika mjini Jakata Indonesia
mnamo mwezi Machi mwaka huu ambao ulisisitiza juu ya uchumi wa Bahari ikiwa ni
pamoja na kuanzisha viwanda vinavyotokana na rasilimali za bahari kwa nchi
wanachama ambapo Zanzibar nayo imo katika mikakati ya kuelekea huko.
Aidha, Dk. Shein aliwasisitiza
viongozi hao kuchukua juhudi za makusudi za kuwavutia wawekezaji ili kuja
kuekeza Tanzania sambamba na kuitangaza Tanzania ikiwemo Zanzibar kiutalii
kutokana na vivutio vingi vilivyopo pamoja na kuyashajiisha Makampuni ya ndege
likiwemo Shirika la ndege la Misri ‘Egytian Air’ kufanya safari zake na
Zanzibar kwa lengo la kukuza sekta hiyo ya utalii.
Nao Mabalozi hao,
waliahidi kutekeleza vyema kazi zao watakapokuwa vituoni mwao na kusisitiza kuwa
watahakikisha wanatoa mchango wao mkubwa katika kuitangaza Tanzania kiutalii,
kuwavutia wawekezaji, kuimarisha na kukuza uhusiano na ushirikirikiano kupitia
Reli ya TAZARA ambayo ipo kati ya Tanzania na Zambia.
Dk.Shein pia, alikutana na Jaji
Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis ambaye alifika Ikulu mjini Zanzibar kwa
ajili ya kujitambulisha pamoja na kufanya nae mazungumzo.
Katika mazungumzo hayo,
Dk. Shein alieleza kuwa anafarajika na utendaji kazi wa mihimili yote mitatu mikuu ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo inafanya kazi ikiwa
huru na kwa mujibu wa Katiba zote za Serikali hizo tena kwa mashirikiano
makubwa ambapo alisisitiza haja ya kuimarishwa kwa pande zote mbili.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment