Habari za Punde

Derby ya Zanzibar Heroes na Kilimanjaro Stars yawa gumzo Kenya. Hapatoshi kesho

Kikosi cha Zanzibar Heroes kilichoanza dhidi ya Rwanda


Na Abubakar Khatib Kisandu, Machakos Kenya.
Ndugu wa wawili wa Tanzania kesho Alhamis watakutana 

katika Soka kwenye Mashindano ya kuwania ubingwa wa 

Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati 

(CECAFA SENIOR CHALLENGECUP), kati ya timu ya Taifa 

ya Zanzibar “Zanzibar Heroes” dhidi ya Tanzania bara 

“Kilimajanjaro Stars” mchezo utakaopigwa majira ya saa 

8:00 za mchana katika Uwanja wa Kenyatta uliopo 

Machakos nchini Kenya.

Huu ni mchezo wa pili kwa kila timu kufuatia Heroes jana 

kushinda mabao 3-1 dhidi ya Rwanda wakati Kilimanjaro 

Stars walitoka sare ya 0-0 dhidi ya Libya katika mchezo wao 

wa awali, hivyo mechi hiyo ni muhimu kwa kila upande 

kupata alama tatu ili kujiwekea matumaini ya kucheza nusu 

fainali ambapo katika kundi lao A kuna timu 5 zinalazimika 

timu 2 kwenda hatua hiyo.

Katika kundi hilo A Kenya wanaongoza wakiwa na pointi nne baada ya kuifunga Rwanda mabao 2-0, kisha wakatoka 0-0 na Libya wakati Zanzibar Heros wakishika nafasi ya pili kwa alama zake tatu  huku Libya wakishika nafasi ya tatu kwa alama zao mbili ambapo Kilimanjaro Stars wakishika nafasi ya nne kwa point yao moja na Rwanda hawana alama wakikamata nafasi ya 5. 
Kilimanjaro Stars imetwaa mara tatu tu taji hilo, 1974, 1994 na mwaka 2010 wakati Zanzibar wenyewe walitwaa taji hilo mara moja tu mwaka 1995.

Uganda ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara sita, Ethiopia mara nne na Tanzania bara mara tatu.
Uganda, The Cranes pia ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo baada ya kutwaa taji la michuano hiyo mwaka 2015 nchini Ethiopia wakiwafunga Rwanda 1-0 kwenye fainali mjini Addis Ababa, wakati mwaka jana michuano hiyo haikufanyika kwa sababu ya kukosa nchi mwenyeji.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.