Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Akli Iddi Azungumza na Ujumbe wa Wawekezaji Kutoka Misri.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akizungumza na Ujumbe wa Viongozi  Wanane wa Taasisi za Uwekezaji kutoka Nchini Misri hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Kiongozi wa Ujumbe wa Viongozi  Wanane wa Taasisi za Uwekezaji kutoka Nchini Misri Bwana Amgad Hassoun  wa Pili kutoka Kulia akimueleza Balozi Seif  maeneo ambayo Kampuni za Misri zinaweza kuwekeza Miradi yao Visiwani Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Zanzibar inaweza kuimarika zaidi kiuchumi, Maendeleo na Ustawi wa Jamii endapo uwekezaji katika Sekta ya Utalii, ujenzi wa Miji Mipya ya Nyumba za Makaazi ya Wananchi wa kawaida, Uvuvi, pamoja na Mifugo itajengewa miundombinu imara katika utekelezaji wake.
Hayo yamejiri kufuatia Kikao cha pamoja kati ya Ujumbe wa Wawekezaji  Wanane kutoka Nchini Misri ukiongozwa na Bwana Amgad Hassoun ulipozungumza na Ujumbe wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ukiongoza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Vuga Mjini Zanzibar.
Mmoja wa Viongozi wa Ujumbe huo kutoka Misri Profesa Hossam El – Borombaly alisema zipo Taasisi na Makampuni ya Uwekezaji Nchini Misri yenye uwezo wa  kuwekeza katika Sekta za Uvuvi, Miji Mipya, Mifugo na Miradi ya Utalii lakini kinachohitajika ni namna ya kuitekeleza kupitia Mikopo ya Benki zilizojitolea kusimamia Miradi hiyo.
Profesa Hossam alisema ujenzi wa Miji ya Kisasa ambayo Misri imeshakuwa  na uzoefu mkubwa inaweza kustawisha Wananchi wa Kipato cha chini kwa kupata  Makaazi bora sambamba na upatikanaji wa Ofisi zenye hadhi inayokubalika Kimataifa.
Alieleza kwamba mradi huo unazingatia hali halisi ya Kimazingira hasa ikitiliwa maanani mfumo wa misimu ya hali ya hewa kama ule wa masika wakati mwengine huambatana na mvua kubwa zinazosababisha mafuriko na kuleta Maafa.
Alisema Sekta ya Uvuvi kwa upande wake inaweza kutoa ajira kubwa  kwa vile Zanzibar imebarikiwa kuzunguukwa na Bahari pande zote baraka ambayo uwezo wa kuvuliwa Tani 1,000 za samaki unawezekana kabisa.
Naye kiongozi wa Ujumbe huo Bwana Amgad Hassoun alisema upo uwezekano mkubwa wa Kamapuni ya Taasisi za kusafirisha Watalii za Misri kuwa kiunganishi cha safari za Watalii kutoka Nchi za Bara la Asia ambao wameonyesha nia ya kutaka kutembelea Visiwa vya Zanzibar.
Bwana Amgad alisema utafiti umebaini kwamba Watalii wengi kutoka Nchi za Kazakistan, Ubakistan pamoja na Pakistan wameonyesha shauku na tayari wanapenda kuitembelea Zanzibar  baada ya kupata sifa ya ukarimu wa Watu wake unaozingatia Mila na Utamaduni wake.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Mali Asili, Mifugo na Uvuvi Mh. Rashid Ali Juma ambae aliwahi kuwa Waziri anayesimamia Sekta ya Utalii aliueleza Ujumbe wa Wawekezaji hao kutoka Nchini Misri kwamba, Wawekezaji wenye nia ya kutaka kuanzisha Miradi yao Zanzibar wanapaswa kuzingatia Utamaduni na Mila za Watu wake.
Mh. Rashid alisema hatua hiyo inasaidia na kuharakisha kukamilisha kwa haraka malengo ya Wawekezaji hao yanayokwenda sambamba na utayari wa Wananchi wa maeneo yatakayohusika na Miradi hiyo ya uwekezaji.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza Ujumbe huo wa Misri kwamba Zanzibar bado ina maeneo mengi ya uwekezaji yanayopaswa kuchangamkiwa na Makampuni na Taasisi za Uwekezaji kutoka Nchini Misri.
Balozi Seif  aliwaomba Viongozi wa Ujumbe huo kuangalia maeneo ambayo wanaweza kujitokeza kuwekeza na kuwataka  kuainisha  Miradi watakayoilenga kuanzisha katika maombi watakayotuma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.