Habari za Punde

Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Wampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Kwa Kuendelea Kuwathamini na Kuwatekelezea Ahadi Alizowaahidi.


WANANCHI wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein kwa kuendelea kuwathamini na kuwatekelezea ahadi alizowaahidi ikiwa ni pamoja na kuwatengenezea barabara yao inayotoka Bububu hadi Mkokotoni.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Alhaj Dk. Shein, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Vuai Mwinyi katika futari maalum aliyowaandalia wananchi pamoja na viongozi mbali mbali wa dini, vyama vya siasa na serikali wa Mkoa huo, hafla  iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu ndogo ya Mkokotoni iliyopo katika Mkoa huo.

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein nae aliungana pamoja na wananchi pamoja na viongozi mbali mbali wa Mkoa huo katika futari hiyo maalum.

Wananchi hao wa Mkoa wa Kaskazini Unguja walizipongeza juhudi za Rais Dk. Shein na kueleza jinsi wanavyothamini maendeleo yote aliyowapelekea pamoja na juhudi zake za kuwatengenezea barabara hiyo ambayo kwa maelezo ya Mkuu huyo wa Mkoa ujenzi wake utaanza rasmi hivi leo.

Barabara hiyo  yenye urefu wa kilomita 31 inajengwa na Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi na Uhandisi wa Majengo (CCECC) kutoka nchini China.

Walieleza kuwa mshikamano mkubwa umepatikana ndani ya Mkoa huo kutokana na uongozi wa Rais Dk. Shein ikiwa pamoja na kuendelea kuwepo kwa amani, utulivu, umoja na mshikanao.

Wananchi hao wa Mkoa wa Kaskazini Unguja walieleza kuridhika kwao kwa amani pamoja na mashirikiano makubwa yaliopo katika Mkoa huo ambayo yamepelekea kuendelea kupata mafanikio katika nyanja zote za maendeleo na za kijamii.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa niaba ya Rais Dk. Shein aliwapongeza wananchi wa Mkoa huo kwa kuitikia mwaliko wa Rais na kuungana nae pamoja katika futari hiyo maalum aliyowaandalia.

Walimpongeza kwa juhudi zake kubwa kwa kuviimarisha vijiji vikubwa vitatu vya Mkoa huo vikiwemo Mgonjoni, Mbuyumaji na Mlilile ambapo kwa upande wa kijiji cha Mgonjoni tayari huduma za maji, umeme, skuli na kituo  cha afya zimeshawafikia.

Akieleza kwa upande wa kijiji cha Mgonjoni alisema kuwa tayari skuli pamoja na kituo cha afya vimeshajengwa pamoja na huduma za maji na  kinachosubiriwa hivi sasa ni bajeti ya mwaka huu inayoanza mwezi wa Julai kwa ajili ya kumalizia barabara yao ambayo imebaki asilimia 20 kumaliza. katika kijiji hicho.

Akielezea kuhusu kijiji cha Mbuyumaji, Mkuu huyo wa Mkoa alieleza kuwa tayari huduma zote muhimu za maendeleo alizoagiza kufikishiwa wananchi wa kijiji hicho zinaendelea kupelekwa ambapo asilimia 95 ya ujenzi wa skuli ya kijiji hicho imefikiwa na asilimi 90 ya matengezo ya hospitali nayo imefikiwa.

Kwa upande wa kijiji cha Mlilile ambacho Dk. Shein alikitembelea wakati wa ziara yake katika Mkoa huo, alieleza kuwa tayari yale  yote aliyoelekeza kufanywa katika kijiji chicho yametekelezwa ikiwemo ujenzi wa skuli, kituo cha afya pamoja huduma za maji na umeme.

Aidha, walieleza kuwa mradi wa Maji katika Mkoa huo unaendelea vizuri na tayari mradi huo wameshakabidhiwa na wataalamu kutoka china na hatua iliyoendelea hivi sasa ni ya usambazaji na kueleza kuwa si muda mrefu tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi na wananchi waweze kupata huduma hiyo.

Wakitoa neno la shukurani wananchi hao wa Mkoa wa Kaskaznini walimpongeza, walimshukuru na kumuombea dua Rais Dk. Shein kwa mema yote aliyowafanyia ikiwemo futari hiyo adhimu aliyowaandalia.

Alhaj Dk. Shein atahitimisha utaratibu na utamaduni wake aliojiwekea wa kufutari pamoja na wananchi wa Mikoa yote ya Unguja na Pemba ambapo hapo kesho anatarajia kufutari pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na viongozi mbali mbali katika viwanja vya Ikulu Mjini Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.