Habari za Punde

Waziri: Kuwatupa wazee kunaondoa baraka kukaribisha laana. Jumuiya ya Alfatah Charitable Association Yawaandalia Chakula Maalum Cha Eid El Fitry Wazee wa Sebleni na Welezo Zanzibar.

AZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo, akisalimiana na Mzee  Alphonce Kumenya anayeishi katika nyumba za wazee Welezo, alipofika katika tafrija iliyoandaliwa na  Jumuiya ya Al Fatah Charitable Association katika Ukumbi wa Wazee Sebleni mjini Zanzibar.
MKURUGENZI wa Jumuiya ya Al Fatah Charitable Association Sheikh Rashid Salum Mohammed, akimuandalia chakula mgeni rasmi Waziri wa Habari, Utalii, na Mambo ya Kale Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo, wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa na  jumuiya hiyo katika ukumbi wa Wazee Sebleni mjini Zanzibar.
WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo (Katikati), akila chakula katika tafrija waliyoandaliwa wazee wanaotunzwa  kwenye nyumba za Sebleni na Welezo. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara anaeshughulikia habari Dk. Saleh Yussuf Mnemo na kushuto ni Mwanasheria wa Al Fatah Masoud Salim Mohammed.
WAZEE wa Sebleni na Welezo wakila chakula cha mchana walichoandaliwa na  Jumuiya ya Al Fatah Charitable Association katika Ukumbi wa Wazee Sebleni mjini Zanzibar.
WAZEE wa Sebleni na Welezo wakila chakula cha mchana walichoandaliwa na  Jumuiya ya Al Fatah Charitable Association katika Ukumbi wa Wazee Sebleni mjini Zanzibar.
MSANII Kassim Yussuf (Ziro Kasorobo), akiwaburudisha wazee kwa utenzi baada ya kupata chakula cha mchana walichoandaliwa na Jumuiya ya Al Fatah Charitable Association katika ukumbi wa Wazee Sebleni mjini Zanzibar.
MKURUGENZI wa Jumuiya ya Al Fatah Charitable Association Sheikh Rashid Salum Mohammed, akitoa maelezo mafupi kuhusiana na shughuli zinazofanywa na jumuiya hiyo kwa jamii.
WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo, akizungumza na wazee wanaotunzwa katika nyumba za Sebleni na Welezo mjini Zanziba baada ya kula nao chakula cha mchana kilichoandaliwa na Jumuiya ya Al Fatah Charitable Association.
WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo, akisaidia kumpandisha gari mmoja kati ya wazee waanaoishi katika nyumba za Welezo, kwa ajili ya kurudi kwenye makaazi hayo baada ya hafla ya chakula iliyofanyika Sebleni.
Picha na Abdalla Omar  Maelezo – Zanzibar.

Na Salum Vuai, WHUMK
KUWATUNZA na kuwasaidia wazee, ni jambo linalopaswa kupewa nguvu kwa ajili ya kutengeneza nchi na jamii bora itakayoridhiwa na Mwenyezi Mungu.
Akizungumza katika tafrija ya chakula cha mchana kwa wazee wanaotunzwa kwenye nyumba za Sebleni na Welezo juzi sikukuu pili, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo, amesema ni wajibu wa jamii kuhakikisha Zanzibar haina mzee anayehangaika kwa kukosa matunzo.
Katika hafla hiyo iliyoandaliwa na jumuiya ya Kiislamu, Al Fatah Charitable Association na kufanyika kwenye nyumba za wazee Sebleni, Waziri huyo alisema, jamii inayowatupa wazee na kuwaacha wakisumbuka bila msaada na matunzo, inakaribisha laana kwa Mwenyezi Mungu na kufukuza baraka.
Waziri Kombo alisema, kwa kuujua umuhimu na mchango wa wazee katika ujenzi wa taifa, ndipo Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume, alipoamua kuwajengea nyumba za Sebleni Unguja na Limbani, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
“Nyumba hizi zimejengwa ili kuhakikisha wazee wetu ambao ndio sababu ya mafanikio na maendeleo tunayopata, wanaishi kwa amani na utulivu wa nafsi badala ya kutelekezwa na kujikuta katika mazingira magumu,” alieleza.
Aidha, aliisisitiza jamii kujua kwamba wazee ni wa wote, na pia mtu anapokua mzee, watoto wote wanakuwa wake, hivyo hakuna sababu ya wao kukosa uangalizi kutoka kwa vijana, ambao utawapa furaha na faraja ya nyoyo.
“Tunaambiwa Pepo iko chini ya nyayo za wazazi. Sisi ndio watoto wenu, na nyinyi ni wazee wetu. Tunaomba mridhike na haya tunayofanya kwenu na mtupe radhi zenu ili nasi turidhiwe na Mwenyezi Mungu,” aliwaambia wazee hao.
Aliipongeza Al Fatah kwa namna inavyowajali wazee, lakini akasema haitoshi tu kuwaandalia pilau na biriani, lakini pia wanahitaji jamii na familia zao kutumia muda wao kuwatembelea na kukaa pamoja nao na kuzungumzia mambo mbalimbali waliyopitia maishani, yakiwemo matamu na machungu.
Mbali na kuwatunza wazee, Waziri huyo aliishauri jumuiya hiyo kuandaa mpango maalumu wa kuwasaidia watoto yatima kwa kuwalea na kuwasomesha hadi elimu ya juu, ili nao watakapokua, warithi uwekezaji huo mzuri wa  kuwaangalia wenzao.
Aidha, alikubali kuwa mlezi wa jumuiya hiyo, akiahidi kufanya kila lililo ndani ya uwezo wake pamoja na serikali, kuhakikisha inastawi na kufikia malengo yake zaidi ya inavyotarajia, huku akiushauri uongozi kutovunjika moyo kwa changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo.
Kwa upande wake, Mshauri wa Waziri huyo Abdalla Mwinyi Khamis, alisema kuwatunza wazee ni sehemu ya utamaduni wa Wazanzibari kuvienzi vitu vya kale, hivyo kilichofanywa na Al Fatah ni kitendo kinachoakisi mila na desturi za Zanzibar.
“Wazee kukaa na watoto wao na kula pamoja, ni mila nzuri ya Wazanzibari inayohitaji kuendelezwa na kila mwananchi kwani kujumuika, mkala, kunywa na kuzungumza kuna raha ya aina ya pekee inayoweza kumtoa mtu machozi ya furaha,” alisema.
Mkurugenzi wa Al Fatah Charitable Association, Rashid Salum Mohammed, alisema jumuiya yake kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali wa ndani na nje, imekuwa ikifanya mengi kuisaidia juhudi za serikali katika kufikisha huduma za msingi kwa wanajamii wa Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa, kutokana na namna inavyofanya kazi kwa uaminifu na juhudi, jumuiya ya Al Fatah imekuwa ikiaminiwa na wahisani wengi na hivyo kuitumia kama njia ya kuifikia jamii inayohitaji kusaidiwa wakiwemo watoto yatima.
Miongoni mwa mambo wanayofanya ni pamoja na kuchimba visima katika maeneo ya  vijijini, kutoa vifaa kwa ajili ya watu wenye ulemavu na wazee.     

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.