Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein Azungumza na Balozi wa Malawi Ikulu Zanzibar.STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                                                                   27.07.2018
---
RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya Malawi na Zanzibar una historia ya muda mrefu hivyo kuna haja ya kuuendeleza ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii.

Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa  Malawi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Bi Hawa Olga Ndilowe aliyefika Ikulu kwa ajili ya kuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Hawa Ndilowe kuwa Zanzibar na Malawi  zina mambo mengi ya kushirikiana kwa pamoja ambayo yanaweza kuleta mafanikio makubwa kwa pande zote mbili yakiwemo mashirikiano katika sekta ya utalii.

Dk. Shein alieleza kuwa  uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Malawi ni njia moja wapo kubwa itakayopelekea kuimarika zaidi kwa sekta ya utalii ambapo wananchi wa Malawi watapata fursa ya kuitembelea Zanzibar na wananchi wa Zanzibar nao watawatembelea ndugu zao wa Malawi.

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi Hawa kuwa Zanzibar na Malawi zote kwa pamoja zina mambo mengi ya kujifunza kwa kila upande ikiwa ni pamoja na namna ya kuendeleza na kuimarisha sekta ya utalii hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar imeanza kupata mafanikio makubwa katika sekta hiyo.

Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa mashirikiano katika sekta ya utalii yatazidisha na kuimarisha uhusiano huo wa kihistoria uliozishwa na waasisi wa nchi mbili hizo akiwemo Marehemu Mzee Abeid Amani karume ambaye alitembelea Malawi mnamo mwaka 1958 na Marehemu Dk. Kamuzu Banda alifika Zanzibar mnamo mwaka 1959.

Dk. Shein aliongeza kuwa mbali ya mashirikiano katika sekta za maendeleo yaliokuwepo wakati huo pia, viongozi hao waliweza kujenga urafiki kupitia vyama vyao vya siasa kikiwemo chama cha ASP kwa upande wa Zanzibar na Chama cha MCP cha Malawi.

Aliongeza kuwa, kwa upande wa sekta ya biashara pande hizo mbili zinaweza kuimarisha na kuendeleza sekta hiyo ambayo itaimarisha uchumi na kukuza uhusiano wa watu wake.

Akieleza kuhusu mashirikiano katika sekta ya elimu, Rais Dk. Shein alieleza kuwa ipo haja kwa kuendeleza mashirikiano kati ya vyuo vikuu vya nchi hiyo na vile vya Zanzibar kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) sambamba na kushirikiana katika sekta ya michezo na utamaduni hasa ikizingatiwa kuwa michezo hukuza urafiki na maelewano.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja ya kuendeleza mashirikiano katika kuwajengea uwezo wafanyakazi kwa pande zote mbili.

Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya mashirikiano ya sekta hizo mbili muhimu, nchi hizo zinaweza kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu, afya pamoja na kubadilishana utaalamu kwa vyuo vikuu hatua itakayopanua wigo wa kitaalamu na kimaendeleo kwa manufaa ya pande mbili hizo.

Nae Balozi wa Malawi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Hawa Olga Ndilowe alimueleza Dk. Shein kuwa Malawi itaendelea na dhamira yake ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kidugu uliopo kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar ambao umejengwa kwa muda mrefu.

Balozi Hawa alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa mashirikiano makubwa aliyoyapata hapa Zanzibar katika kipindi chake chote alichofanya kazi akiiwakilisha Malawi hapa Tanzania huku akisisitiza kuwa nchi hiyo itaendeleza ushirikiano wake na kukuza uhusiano wa kihistoria na kidugu uliopo.

Katika maelezo yake Balozi Hawa alimueleza Dk. Shein, haja ya kuendeleza ushirikiano katika sekta ya utalii kati ya pande mbili hizo hasa ikizingatiwa sekta hiyo ina umhimu mkubwa katika kukuza uchumi.

Alieleza kuwa kwa upande wake ameona kuna faida nyingi zinaweza kupatikana katika sekta ya biashara iwapo mashirikiano yataimarishwa zaidi ambapo tayari hivi sasa mafanikio yameanza kupatikana kati ya Malawi na Tanzania kutokana na makubalizo ambayo yameanza kufanyiwa kazi kwa sekta hiyo na sekta nyengienzo.

Aidha, Balozi Hawa alieleza kuwa mashirikiano katika sekta ya biashara  kati ya nchi yake na Tanzania yanaedelea vizuri na kueleza haja ya kuimarishwa kwa manufaa ya pande mbili hizo.

Aliongeza Malawi na Zanzibar zinaweza kushirikiana katika sekta kadhaa za maendeleo ikiwemo elimu, biashara, afya, kuwajengea uwezo wafanyakazi, utalii, michezo na utamaduni pamoja na sekta nyenginezo.

Balozi Hawa aliongeza kuwa Malawi imekuwa na mashirikiano na Tanzania katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu ambapo baadhi ya vyuo vikuu vya Tanzania kiikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam na vyo vikuu vyenginevyo vimenza kushirikiana.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.