Habari za Punde

Balozi Seif aipongeza Serikali ya China alipozungumza na Balozi mdogo aliyepo Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaolon Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Xie Xiaolon wa pili kutoka Kushoto pamoja na Mtapta wake akibadilishana mawazo na Balozi Seif  kuhusu Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara yanayotarajiwa kufanyika Wiki ijayo katika Mji wa Nanning Nchini China.

Picha na – OMPR – ZNZ



Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa upendeleo wake wa kuiteuwa Tanzania pekee kati ya Nchi za Afrika ya Mashariki kushiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa 15 wa Biashara {China –Asean Expo 2018} unaotarajiwa kufanyika katika Mji wa Nanning ndani ya Jimbo la Guangxi.
Alitoa pongezi hizo wakati alipokuwa akizungumza na Balozi mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaolon Ofisini kwa Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema Tanzania na Zanzibar kwa ujumla zitaendelea kuiona China kama Taifa Rafiki lenye dhamira na muelekeo wa dhati wa kuunga mkono harakati za maendeleo na kiuchumi Nchini Tanzania kasi inayoleta faraja kwa Serikali zote mbili za Tanzania pamoja na Wananchi wote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi huyo mdogo wa China aliyepo Zanzibar kwamba taarifa za hivi punde kutoka kwa maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afika Mashariki ya Tanzania walioko Nchini China zinaeleza kwamba matayarisho ya maonyesho hayo yanakamilika vyema.
Balozi Seif alisema banda la Tanzania litakalojumuisha Wafanyabiashara, Wawekezaji na Wajasiri amali linakamilisha taratibu zote ili liweze kufunguliwa rasmi Tarehe 11 Septemba ambapo ufunguzi rasmi wa Maonyesho hayo utafuatia siku ya Pili ya Tarehe 12 Septemba.
Alimuhakikishia Bwana Xie Xiaolon kwamba uhusiano wa Tanzania na China utazidi kuimarika kufuatia mikakati ya Taifa hilo la Bara la Asia kutoa upendeleo maalum kwa kuunga mkono kasi ya kiuchumi ya Mataifa ya Bara la Afrika, Tanzania ikiwa miongoni mwa Nchi za Bara hilo zinazoendelea kufaidika na neema hiyo.
Mapema Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaolon alisema suala la China kulipa upendeleo Bara la Afrika linazingatiwa vyema na Serikali ya Nchi hiyo katika mpango wake wa mageuzi ya Kiuchumi yaliyolenga kwenda sambamba na kusaidia ufufuaji wa Uchumi wa Afrika.
Bwana Xie Xiaolon alisema yapo mafanikio makubwa yaliyokwisha patikana kupitia mpango huo ikiwemo misaada ya kiuchumi inayokwenda sambamba na ongezeko la Makampuni na Taasisi za Uwekezaji kufungua milango katika Mataifa mengi Barani Afrika.
Alielezea faraja yake kutokana na tukio la Wiki hii la utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya uvuvi kati ya china na Tanzania lililofanyika Mjini Beijing Nchini China.
Tukio hilo lililofanywa na Waziri wa Kilimo. Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Seriali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Rashid Ali Juma kwa upande wa Tanzania na Naibu Waziri wa Kilimo wa China Bwana Qu Dongyu lilishuhudiwa na Waziri Mkuu wa Tanzania  Mh. Kassim Majaliwa na Waziri wa Kilimo wa China Bwana Han Chanfu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.