Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Azungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Ikulu Zanzibar.

Rais Dk. Shein alikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna wa Polisi Diwani Athumani aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kujitambulisha kwa Rais.
Katika mazungumzo kati yake na kiongozi huyo, Rais Dk. Shein alieleza umuhimu wa kuendeleza mashirikiano kati ya (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA).
Rais Dk. Shein alieleza kuwa licha ya taasisi hizo kwa kila moja kufanya kazi zake lakini bado zote zina kazi ya kupambana na kudhibiti rushwa na kusisitiza kuwa kupambana na rushwa na kusimamia maadili ya viongozi ni mambo ya msingi katika utawala bora ambapo iwapo yakifanywa vizuri yatawasaidia wananchi.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)  Kamishna wa Polisi Diwani Athumani alieleza kuwa suala la rushwa ni changamoto kubwa ambayo si kwa Tanzania tu bali ni dunia nzima.
Alisema kuwa rushwa inawagusa moja kwa moja wananchi wa kada zote hasa katika eneo la maendeleo hivyo mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika kupambana nayo.
Alisisitiza kuwa kumekuwepo mashirikiano makubwa kati ya Taasisi hiyo na ile ya Zanzibar ambapo miongoni mwa maeneo wanayoendelea kushirikiana ni pamoja na utoaji mafunzo na kubadilishana uzoefu.
Rais Dk. John Pombe Magufuli alimteua Kamishna wa Polisi Diwani Athumani kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mnamo Septemba 6, 2018 ambapo anachukua nafasi ya Kamishna wa Polisi Valentino Mlowola ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.