Habari za Punde

Wizara ya Afya Zanzibar Yasaini Mkubaliano na Kampuni ya Utafiti wa Madawa ya Novartis.

Mkuu wa Kampuni ya Novartis Kanda ya East & Southern Africa Dkt. Nathan Mulure s kushoto wakitiliana saini ya Mkataba wa Maridhiano na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bi. Asha Abdallah kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya Zanzibar na Kampuni ya Novartis Social Business iliyoko Switzerland kwa lengo la kuanzisha Programu itakayotekelezwa kupitia huduma ya Simu ya Mkononi kupitia Mtandao wa Vodacom.Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Hotel ya Verde Mtoni Zanzibar.
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 26.09.2018
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana saini Mkataba wa maridhiano na Kampuni ya Madawa ya Norvatis iliyoko Switzerland kwa lengo la kuanzisha Programu itakayotekelezwa kupitia vituo vya afya ya msingi Zanzibar.
Program hiyo itawezesha kujua taarifa za hali ya matumizi na uwepo wa Dawa Vituoni kote nchini kupitia huduma ya mtandao wa Simu ya Mkononi ya VODACOM.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo huko Hoteli ya Varde Mtoni, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman amesema mfumo huo utawezesha pia kujua taarifa za Maradhi mbali mbali zinazoendelea katika sehemu zote za utoaji wa huduma ya afya ya msingi kupitia vituo vya afya nchini.
Amesema lengo la kuingia makubailiano hayo ni kuendeleza juhudi za Serikali katika kuinua hali ya utoaji wa huduma bora za afya kwa wazanzibari wote.
Amesema majukumu hayo yanakwenda sambamba na uanzishwaji wa Mkakati wa Afya Mtandao (E-Health Strategy- 2014-2016) kwa maendeleo mapya ya kupeana taarifa na mafunzo mbalimbali kupitia Teknolojia ya Mawasiliano.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Vodacom Afrika Mashariki Stephen Kinuthia amesema Mradi huo utakuwa unatumia nyenzo mbalimbali katika kupeleka taarifa, nyenzo kuu ikiwa na matumizi ya simu kubwa za Mkononi (Tablet) na mtandao wa simu uliounganishwa na Computer na hivyo kuunganishwa na Vituo vyote vya Afya ya Msingi.

Amesema mradi huo utakaojumuisha jumla ya Vituo 190 vya Unguja na Pemba,    umekuwa ukitumika katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Kenya, Nigeria, Afrika kusini, Cameroon na Ghana.
Mwakilishi wa Ubalozi wa Switzerland nchini Romana Tedeschi amesema Switzaland na Tanzania zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu katika mambo mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya toka miaka ya 1960.
Amesema wataendeleza kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhakikisha Wananchi wanapa huduma za afya za kiwango cha hali ya juu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Abdulla amesema Wizara itahakikisha usimamizi mzuri wa Vifaa vitakavyotolewa kupitia mradi huo vinatunzwa vyema ili kutimiza lengo lililokusudiwa.
Amesema Wizara itaunda Kikundi kazi maalum cha mipango kitakachoratibu shughuli zote za mradi kwa muda wote mradi utakaofanya kazi.
Mradi huo wa miaka miwili unatarajiwa kugharimu takriban Bilioni moja za kitanzania kwa ajili ya kuweka mfumo huo, kununulia Vifaa na mafunzo kwa watendaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.