Habari za Punde

Mkutano wa Tisa wa Jukwaa la Biashara Zanzibar.Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni.

Na Ali Issa  Maelezo.
Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Balozi Amina Salum Ali amesema Baraza la Biashara la Taifa kwa ushirikiano na Serikali na sekta Binafsi ni njia moja wapo rahisi ya kuwasaidia Vijana kupata ajira na kuweza kujinasua na hali ngumu ya kiuchumi.
Ameyasema hayo leo huko Wizarani kwake Migombani  wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Jukwaa la Tisa la Biashara la Zanzibar litalofanyika siku ya Jumamosi tarehe 24-11-2018 huko  katika ukumbi wa Sheikhe Idrissa Abdullwakili chini ya Mwenyekiti wake  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein.
Amesema kumekuwa na kundi kubwa la vijana wasio na ajira linalotokana na soko la ajira kuwa dogo Serikalini  hivyo muundo wa baraza hilo ni kuwasaidia vijana  ili waweze kujiajiri na kuzalisha kipato chao na familia zao.
Aidha Balozi Amina amesema  kumekuwa na fursa nyingi za kuwafanya vijana kujiajiri wenyewe katika Nyanja mbalimbali za kimaendeleo lakini vijana hushindwa kukosa mitaji,nyezo,masoko na pembejeo za kilimo.
Hata hivyo alisema  iwapo  yakizingatiwa hayo kutaweza  kuwasaidia vijana kwani hakuna sababu ya  wao kushindwa kukimu maisha yao ya kila siku .
“Kuna fursa nyingi sana za kufanikiwa vijana wetu kimaisha yakiwemo mambo mbali mbali kama vile soko la utalii, kilimo, uvuvi, viwanda na biashara,” alisema Balozi Amina.
Aidha Waziri huyo alisema kuwa Serikali imetunga Sheria namba 10 ya mwaka 2017 ilianzisha muundo wa majadiliano ya kibiashara baina ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Sambamba na hayo alisema kuwa jukwaa la tisa litajadili kwa pamoja fursa za ajira ambazo zinaweza kupatikana katika sekta za kiuchumi zikiwemo Utalii,Viwanda ,Kilimo na Uvuvi ili kuweza kuhamasisha na kuchochea shughuli za kiuchumi hapa Zanzibar.
Mwisho
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.