Habari za Punde

Balozi Seif mgeni rasmi Mahafali ya 11 ya Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea Gwaride la Wahitimu wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar katika mahafali yaliyofanyika katika Ukumbi wa Dr. Ali Mohaed Shein uliopo ndani ya Viunga vya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA}kiliopo Tunguu Mkoa Kusini Unguja.

Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria na Utawala Bora Mh. Haroun Ali Suleiman Waziri wa Elimu Mh. Riziki Pembe Juma, Kushoto ya Balozi ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Bibi Fatma Said Ali,Waziri wa Vijana Balozi Ali Karume na Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Mh. Hassan Khatib.
 Baadhi ya Wahitimu wa Chuo cha Utawala wa Umma Tunguu wakiingia ndani ya ukumbi wa Dr. Ali Mohamed Shein SUZA kukamilisha mahafali yao ya 11.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihutubia kwenye Mahafali ya 11 ya Chuo cha Utawala wa Umma Tunguu Mkoa Kusini Unguja.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar Bibi Fatma Said Ali akitoa salamu wakati wa kuanza kwa Mahafali ya 11 ya Chuo hicho hapo Tunguu.
 Baadhi ya Wahitimu wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyokuwa yakifanyika kwenye Mahafali yao ya 11 kwenye Ukumbi wa SUZA
  Muhitimu Abass Bakari Yakoub akipokea zawadi ya Mwanafunzi Bora wa {DRM} kutoka kwa Mgeni Rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Muhitimu Maryam Said Omar akipokea zawadi ya Mwanafunzi Bora wa {DSS} kutoka kwa Mgeni Rasmi WA Mahafali yao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Taifa bado linahitaji kuwa  na Watumishi wenye ujuzi ili kwenda sambamba na mabadiliko mbali mbali ya sayansi  na Teknolojia itakayoweza kuzikabili changamoto tofauti zilizopo Ulimwenguni hivi sasa.
Alisema Watumishi hao wakiandaliwa vyema katika maadili bora ya Utumishi wa Umma uliojaa Ubunifu, weledi na uchungu wa Rasilmali za Taifa ndio watakaokuwa tayari kuibadilisha Zanzibar kufikia Maendeleo yanayokusudiwa na Jamii.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Wahitimu wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar wa ngazi na Fani mbali mbali za Elimu pamoja na Walimu na Wananchi kwenye Mahafali ya Kumi na Moja ya chuo hicho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa  Dr. Ali Mohamed Shein SUZA Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema kwa vile Mtumishi wa Umma ndio Rasilmali ya msingi na nguvu kazi ya Maendeleo ya Taifa lolole, Chuo cha Utawala wa Umma kina dhima ya kumuandaa na kumuendeleza Mtumishi wa Umma ili amudu kutekeleza majukumu aliyopangiwa kwa ueledi, uaminifu, upendo na Uzalendo.
Balozi Seif alisema Chuo hakina budi kujikita katika kufanya tafiti mbali mbali zitakazosaidia kuandaa Programu za mafunzo ya muda mrefu na mfupi zitakazokwenda sambamba na mahitaji ya Wanajamii ili kuisaidia Serikali kuwa na Watumishi Bora wanaotoa huduma kwa vigezo na  viwango kulingana na matarajio makubwa ya Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Uongozi wa Chuo hicho kuendelea kuongeza Uwezo wa kubadili Wanafunzi wengi zaidi lakini kwa kuzingatia vigezo na masharti yanayowekwa na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini pamoja na mahitaji ya sasa na baadae ili kufikia malengo ya Nchi iliyojiwekeza.
“ Tukumbuke kuwa Taifa linahitaji wasomi walioandaliwa vyema  na kushiba Maadili bora ya Utumishi wa Umma, Weledi wenye Uchungu wa Rasilmali za Nchi”. Alieleza Balozi Seif.
Alielezea faraja yake kuona jinsi Chuo kinavyoendelea kutanua wigo wake wa kutoa Mafunzo mafupi ya kujenga uwezo kwa Watumishi wa Umma ikiwemo kuijengea uwezo Idara husika kwa kuandaa Programu Maalum ya Mafunzo iliyotokana na ziara ya kujifunza uendeshaji katika vyuo mbali mbali vya Zanzibar na Tanzania Bara.
Balozi Seif alisema kitendo cha kutoa mafunzo kwa Watumishi Wastaafu  watarajiwa pamoja na watumishi wapya ni ishara tosha ya namna Chuo kinavyopiga hatua ya kutekeleza majukumu yake ya msingi ya maandalizi ya Watumishi Wastaafu.
Alisema wakati umefika sasa wa kukithamini na kukiheshimu Chuo cha Utawala wa Umma na kukitumia ipasavyo kama alivyosema Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ywa Mwaka 1964 Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kutukuza chake Mtu mpaka asahau cha mwenzake.
Alieleza kwamba Taasisi za Umma na hata zile binafsi wajenge Utamaduni wa kukitumia Chuo cha Utawala wa Umma katika kuwaendeleza Watendaji wao chenye Walimu waliobobea wenye uwezo wa kuwabadilisha wanafunzi wao Kimaadili, Kitaaluma, Kifrikra, Kimawazo na Utendaji .
Kwa upande wa Wahitimu hao, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha kuitumia Taaluma wanapokwenda eneo lolote ili kubadilisha utendaji kazi wa mazoea kwenda kwenye Utumishi wenye kuzingatia uweledi, tija na utoaji huduma wa wakati kwa Wananchi.
Alisema Taifa linafurahia siku muhimu na adhimu ya ongezeko la Wataalamu wa fani mbali mbali wanaoingia kwenye tanuri la uwajibikaji utakaotegemewa katika kuleta mabadiloko ya Maendeleo endelevu Nchini.
Mapema Mkurugenzi wa Chuo cha Utawala wa Umma Dr. Mwinyi Talib Haji Alisema Chuo hicho ni Taasisi inayojitegemea na kupewa dhamana ya kutoa Mafunzo yanayohusiana na masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Nchini.
Dr. Mwinyi alisema Watumishi wa Umma ni Rasilmali muhimu inayopaswa kuenziwa kwa kupatia nyenzo ya kuwajibika Kitaaluma ambayo ni Elimu inayohusiana na Fani yao.
Alisema Chuo kimepata maendeleo makubwa tokea kuasisiwa kwake kwa kuzalisha Wahitimu wenye hadhi ya kukubalika katika ajira za Taasisi tofauti ambapo kwa sasa tayari kinawanafunzi 1,510 wanaoendelea kupata mafunzo katika fani tofauti.
Dr. Mwinyi alifahamisha kwamba Mwaka huu Chuo hicho kimezalisha Wahitimu wapatao 746 wa Ngazi ya Stashahada na Cheti katika fani mbali mbali sambamba na Wafanyakazi 2,675 wa Taasisi za Umma waliopatiwa Mafunzo.
Mkurugenzi huyo wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar alieleza kwamba Uongozi huo tayari umeshafungua Tawi lake Kisiwani Pemba linaloendelea kuwafinyanga Wanafunzi 235 hivi sasa.
Licha ya Mafanikio hayo Dr. Mwinyi alieleza kwamba zipo changamoto zinazokikabili chuo hicho akizitaja baadhi kuwa ni pamoja na uhaba wa Ofisi za Watendaji na Uzio unaotia hofu ya kuvamiwa na wahalifu hasa nyakati za Usiku.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kuzungumza na Wahitimu hao Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar Mh. Haroun Ali Suleiman alitoa wito kwa Viongozi na Wafanyakazi wa Taasisi za Umma kujipangia utaratibu wa kupata mafunzo ya Kazi chuoni hapo.
Waziri Haroun alisema Chuo kimebarikiwa kuwa na Walimu wenye uwezo mkubwa wa kutoa mafunzo yenye muelekeo wa kumuwezesha Manafunzi kufikia ngazi ya Stashahada kwa hivi sasa.
Kabla ya Mwaka 2007 Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar kilikuwa kikitoa Mafunzo kwa Watumishi wa Kada ya Chini, lakini kwa sasa kinadahili Wanafunzi wa ngazi ya Shahada ya Kwanza katika Kada tofauti zikiwemo Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka, Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia na Usimamizi wa Rasilmali Watu.
Wengine ni Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari, Uongozi wa Biashara, ununuzi na Ugavi, Mipango ya Maendeleo, Utawala wa Serikali za Mitaa, Uhazili, Uongozi wa Elimu na Utawala pamoja na Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.