Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiondoa kipazia kuashiria kuweka Jiwe la Msingi la Jengo Jipya la Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Maabara ya Vinasaba vya DNA, Maruhubi Zanzibar, ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali na Maabara ya Uchunguzi wa Vinasaba (DNA) kujidhatiti katika ubunifu
ili ziweze kutoa huduma bora na za kisasa zaidi, zitakazokwenda na wakati
uliopo,
Dk. Shein aliyasema
hayo katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali na Maabara ya Uchunguzi wa Vinasaba (DNA), lililopo Maruhubi, Mkoa wa
Mjini Magharibi ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 55 ya Mapinduzi ya
Januari 12, 1964.
Alisisitiza kuwa
uongozi wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Maabara ya Uchunguzi
wa Vinasaba (DNA), ni lazima uweze kujikita katika suala zima la ubunifu kwa
lengo la kwenda mbele zaidi na kupata mafanikio katika kutoa huduma za afya
zikiwemo zile za uchunguzi.
Alieleza kuwa ubunifu
ni jambo muhimu na kubainisha kuwa pale unapopewa cheo ni pazima uwe mbunifu,
badala ya kubaki ukitegemea mambo yaliobuniwa na wengine,
ikiwa ni pamoja na njia na mikakati
sahihi.
Alieleza haja ya Bodi
ya Wakala na Maabara hiyo kutoa msaada katika kuisaidia Maabara hiyo kubuni
mipango mbali mbali na kueleza kuwa kila siku kumekuwa kukibuniwa mambo mapya
duniani, hivyo ni vyema na wao wajiweke tayari katika mabadiliko hayo, kwa vile
tayari wamekuwa wakifanya kazi na wataalamu wengine wa Afrika Mashariki na
sehemu nyengine duniani.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa DNA ina mambo mengi inayoyafanya na sio kama inavyokuzwa hivi sasa na
baadhi ya watu, akibainisha kazi zinazofanywa Maabara hiyo husika ni za
kitaalamu ambazo zenye taratibu zake.
Alieleza kuwa Zanzibar
ina vifaa na mashine nyingi muhimu za utoaji huduma za afya kupitia Wizara ya
Afya ikiwa pamoja na mashine ya uchunguzi ya MRI ambayo ni muhimu katika huduma
za afya.
Dk. Shein alisema kuwa
Mapinduzi ni mabadiliko ikiwa ni pamoja na kupanga mipango ya maendeleo kwa
nchi na wananchi wake na ndio maana ASP
ilipaswa kufanya Mapinduzi kutokana na dhulma kubwa iliyokuwepo kwa muda mrefu
ambapo haki haikuwa ikitendeka kwa
Wazanzibari.
Aliongeza kuwa wakati
wa ukoloni palikuwa na ubaguzi mkubwa wa kutoa huduma za afya ambapo watu
waligawiwa kwa makundi katika kutoa
huduma hizo kulingana na uwezo na nasaba
zao.
Alisema kuwa kabla ya
Mapinduzi matibabu yalikuwa kwa ubaguzi na ndio maana mara tu baada ya
Mapinduzi mnamo Machi 3, 1965 Marehemu
Mzee Karume alitangaza matibabu bure ambapo hata hivyo kabla ya Mapinduzi Maabara
hiyo kazi zake zilifanywa kwa ubaguzi.
Pamoja na hayo, alisema
kuwa Maabara hiyo imepita katika mikondo migumu na ndio sababu Serikali ikaipa
kipaumbele tokea Awamu zilizopita na viongozi wengine waliofuata huku
akisisitiza kuwa na yeye kwa upande wake aliweza kutoa mchango wake wa kuimarishwa taasisi hiyo.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa Maabara ya Viwango, Maabara ya Vyakula na Vipodozi pamoja na
Maabara ya Mkemia Mkuu na Maabara ya
Uchunguzi wa Vinasaba (DNA) ni muhimu sana ambapo kila moja ina kazi zake na Sheria
na taratibu zake hivyo kazi zao haziingiliani.
Akieleza juuu ya kazi
za Maabara ya Uchunguzi wa Vinasaba (DNA), Rais Dk. Shein alisema kuwa katika
uchunguzi unaofanywa katika Maabara hiyo hatimae kesi zinazoletwa zinakwenda
Mahakamani, hivyo taasisi hizo ni lazima ziwe na watu wenye taaluma kubwa na kuwataka kuwa makini katika utendaji wao
wa kazi.
Alieleza kuwa wale
wanaoshutumiwa ndio watakaokuja katika Maabara hizo wakiwemo wale waliofanya
matokeo mbali mbali maovu wakiwemo waliobaka, hivyo umakini lazima uwepo ili
kuweza kupata ukweli juu ya uchunguzi utakaofanywa.
Alisema kuwa Wizara ya
Afya imefanya mambo makubwa katika Awamu ya Saba, chini ya uongozi wake ikiwa
ni pamoja na kuwepo kwa huduma ya Benki ya Damu ambayo hapo nyuma haikuwepo.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa wakati anaingia madarakani, Novemba 3 mwaka 2010 Serikali ilikuwa
inakusanya TZ Shilingi Bilioni 13.5 kwa mwezi lakini hivi sasa fedha
zinazokusanywa na Serikali ni TZ Shilingi Bilioni 65 kwa mwezi.
Alisema kuwa licha ya Zanzibar
kuwa nchi masikini lakini imeweza kufanya mambo mengi makubwa ambayo kuna nchi
nyengine haziwezi kufanya kama ilivyofanya Zanzibar.
Dk. Shein alizitaka
Maabara zote tano za hapa Zanzibar waanzishe Jumuiya yao ya Maabara kama ilivyo
kwa nchi nyengine hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ina wataalamu watu wengi.
Alisema kuwa iwapo
watafanya hivyo itasaidia hasa katika kufanya kazi zao huku akiwataka kuunda Jumuiya zao za Kitaalamu ili awe na
nguvu za Kitaalamu na kuweza kushiriki mambo kadhaa duniani kwani tayari Zanzibar
imekuwa ikijulikana.
Alisema kuwa Zanzibar
inajiuza kwa jina lake, na kuwataka kuitumia nafasi hiyo kuendelea kuijenga
nchi, Mapinduzi na Muungano kwani Mapinduzi yameleta Muungano ambao umeleta
nguvu kwa wananchi wake.
Alisisitiza kuwa ni
lazima wafanyakazi wajikite kwenye uzalendo kama walivyokuwa wakifanya kazi wao
katika Wizara hiyo na kusisitiza kuwa lengo ni kwenda kwenye taaluma za kisasa zaidi
ili kuweza kutoa huduma za kitaalamu zinazokwenda na wakati uliopo.
Aidha, alieleza kuwa
fani hiyo ya uchunguzi wa mambo ya jamii hukumu yake haiishii hapa duniani bali
yanaishia kwa Mwenyezi Mungu hivyo, aliwataka wafanyakazi wa Maabara hiyo
kufanya kazi kwa umakini, kuwa waadilifu na wakweli pale wanapotoa matokea.
Aliongeza kuwa kazi
hiyo ni kazi ambayo matokeo yake hayaishii hapa ni kazi ambayo ina lawama hivyo
aliwataka kufanya kazi vizuri ili matokeo yawe mazuri na kwani wananchi wote wa
Zanzibar wanaitegemea sana Maabara hiyo iwasaidie katika uchunguzi wa DNA.
Nae Kaimu Waziri wa
Afya Rashid Ali Juma, alisema kuwa jengo hilo linakidhi nafasi ya vyumba vya
maabara pamoja na nafasi na kueleza kufarajika kwa kupata jengo hilo ambalo
litandoa changamoto ya nafasi na kuwafanya watendaji kufanya kazi kwa ufanisi.
Watafanya kazi ya
kutoka huduma ya uchukungu zi kitaifa na kimafaita, ni shemu ambayo imeanza 1908
ambapo hivi sasa itatizomiza 111.
Maabara kwa kipndi
kirefu ilifanya kazi zake katika chumba kimoja katika Wizara ya Afya, na baadae
kuhamishwa na kupatiwa nafasi ya muda katika jengo la Living stone pamoja na kuwa
na watumishi wachache na hivi sasa idadi ya watumishi imeongezeka .
Mnamo mwaka 1964
ilihamishiwa Wizara ya Afya ambyo ipo hadi hivi sasa ambapo ilipandishwa hadhi
ya kuwa Idara kamili pamoja na kupatiwa jengo huko Mwanakweekwe ambapo miongoni
mwa kazi zake ni uchunguzi wa vyakula, dawa za kuevya, sumu na pombe.
Alieleza kuwa hatua
hiyo ni mafanikio makubwa ambayo yamepatikana katika uongozi wake ikiwa ni pamoja na kupitishwa Sheria namba 10
ya mwaka 2011 na kutoka Idara hadi kuwa Wakala
ambayo ndiyo matuda mema katika sekta ya afya.
Waziri Rashid alisisistiza
kuwa hiyo ni Taasisi muhimu katika nyanja za kiuchimi na kijamiii, ambayo ina
kazi ya kufanya uchunguzi na kutoa matokea kwa jamiii na hiyo ni sehemu ya
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM hasa katika kuimarisha uchunguzi kwa
wananchi.
Katika maelezo yake,
Waziri huyo alimuomba Rais Dk. Shein kuendelea na utamaduni wake wa kuzilea taaasisi hizo ili Maabara hiyo iendelee
na kazi zake za uchunguzi na kusisitiza imani yake katika kuhakikisha huduma
muhimu zinatolewa.
Kaimu Waziri huyo wa
Afya alitumia fursa hiyo kuwapongeza wafanyakazi kwa taaluma zao walizonazo
pamoja na kuupongeza uogozi wa Idara hiyo sambamba na kupongeza mashirikiano
makubwa yaliopo kati ya watendaji wa Wakala huyo.
Mapema , Katibu Mkuu
Wizara ya Afya Asha Ali Abdalla alisema kuwa
kuwepo kwa mashine za uchunguzi wa vinasaba kutapelekea pamoja na mambo mengine
kupatikana kwa ushahidi wa kitaalamu utakaowezesha kutatuwa utata wa kesi
nyingi hasa zinazohusu udhalilishaji wa kijinsia pamoja na kihalifu.
Alisema kuwa hatua
hiyo itasaidia kufanya tafiti za magonjwa mbali mbali na pia, kuwezesha
kutambuwa miili ya wahanga pale inapotokea ajali na wahanga kushindikana kutambuliwa
kwa sura.
Katibu Mkuu huyo
alisema kuwa mpaka hatua zilizofikiwa za ujenzi wa jengo hilo mradi huo wa
Kuimarisha Maabara ya Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali umegharimu jumla ya TZ Shilingi
Bilioni 2.8.
Alisema kuwa jengo
hilo limejenga na Mkandarasi mzalendo kutoka Zanzibar anaeitwa (Millenium
Engineering Company) ambae amejitahidi kulijenga kwa kiwango kilichohitajika na
amefanya kazi hiyo chini ya usimamizi wa Wataalamu Wahandisi na Wasarifu wa
Majengo wa Wizara ya Afya.
Sambamba na hayo,
Katibu Asha alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa jitihada kubwa aliyoionesha
katika kufanikisha kuwepo kwa jengo hilo la Maabara ya Wakala wa Mkemia Mkuu wa
Serikali “Tusingelifika hapa kama si nia yako safi na ya dhati pamoja na azma
ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha huduma za maabara za
uchunguzi ili kuleta maendeleo chanya kwa wananchi na Zanzibar kwa
jumla”,alisema Katibu Asha.
Mapema Dk. Shein
alitembelea jengo hilo na kupata maelezo juu ya shughuli zinazofanywa katika
Maabara hiyo ya uchunguzi ya DNA pamoja na kupata maelezo juu ya utendaji kazi
wa vifaa vilivyomo ambavyo ni vya kisasa.
No comments:
Post a Comment