Na. Suleiman Juma
MKURUGENZI wa Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima
Zanzibar, Bi Mashavu Ahmad Fakih amesema Walimu wa Vituo vya Elimu Mbadala
wanahitaji kujengewa uwezo ili waweze kuwa wabunifu katika shughuli mbalimbali
ikiwa ni pamoja na uandaaji wa zana kulingana na mazingira ambapo wataweza
kufanikisha dhana nzima ya ufundishaji na ujifunzaji.
Alieleza hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalumu kwa
walimu wa Kituo cha Elimu Mbadala Mtemani Wingwi Pemba.
Alisema, mafunzo watakayopatiwa yatawajengea uwezo walimu
hao kuandaa zana za kufundishia na kujifunzia na kuweza kwenda sambamba na
mtaala husika, pamoja na kuongeza ubunifu wa vitu vipya katika kukidhi
mahitaji.
“Mafunzo haya yataweza kubuni mbinu na kuandaa zana husika
katika suala zima la ufundishaji, lakini vilevile itakuwezesheni kufundisha kwa
mujibu wa mtaala tulionao” alieleza.
Sambamba na hilo alisema kuwa, walimu ni viongozi hivyo
wanapaswa kujua mbinu mpya za uongozi, utawala, na uendeshaji na kuongeza uwezo
katika masuala ya uratibu na usimamizi.
Alisema, mafunzo ya walimu hujikita katika masuala ya muhimu
ambayo ni utendaji kazi na matatizo kazini kwani walimu hukutana na matatizo
mengi yanayokwamisha wepesi na ufanisi
wa mwalimu kiutendaji hasa katika ufundishaji.
“Mafunzo yatawezesha kukabiliana na mahitaji na mabadiliko
yote katika mazingira ya ufundishaji yatakayojitokeza, kwaiyo yatakupeni upeo
mzima wa kuona tumefikwa na changamoto hii tuweze kuitatua kwa kiasi gani”
aliongeza.
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Divisheni Elimu
Mbadala na Watu Wazima Bi Halima Tawakal Hairallah aliwataka walimu hao
kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili waweze kufundisha kwa wepesi na ufanisi.
Wakitoa michango yao baadhi ya walimu wa kituo hicho
walimshukuru Mkurugenzi huyo kwa kuwaandalia mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia
kazi.
No comments:
Post a Comment