Habari za Punde

Viongozi wa Dini Wanaharakati wa ukatili na Udhalilishaji watakiwa kuunga mkono juhudi za Serikali kupiga vita vitendo hivyo.

Na.Takdir Suweid.Maelezo Zanzibar.
Viongozi wa Dini na Wanaharakati wa kupiga vita vitendo vya Udhalilishaji wameombwa kutekeleza kwa vitendo mikakati iliowekwa na Serikali ya kupiga vita vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto ili iweze kufanikiwa.
Wito huo umetolewa huko Tawi la Ccm Muungano na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mjini Haji Lila Haji wakati alipokuwa akizungumza na Viongozi wa Matawi,Wadi na Jimbo la Amani ikiwa ni shamrashara za Juma la wiki ya Wazazi.
Amesema Serikali imeweka Sheria na Mikakati madhubuti kupinga vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto lakini mikakati hiyo haitoweza kufanikiwa iwapo hakutokuwa na mashirikiano ya kutosha baina a Serikali na Taasisi hizo.
Amefahamisha kuwa Viongozi wa Dini na Wananharakati wanamchango mkubwa katika jamii hivyo hakuna budi kutumia nafsi zao kuunga mkono mikakati iliowekwa na Serikali ya kupiga vita vitendo hivyo.
Aidha amewakumbusha Wazazi na Walezi kushirikiana na kuwalea watoto wao katika misingi ya Maadili mema na kuondokana na vishawishi vya kujiingiza katika utumiaji wa Dawa za kulevya,Bangi na Uhasharati.
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mjini Salama Rajab Kaboyonga amesema wamefanya ziara Majimbo yote ya Wilaya hiyo ili kuwakumbusha wazazi juu ya kuwalea watoto wao katika maadili mema ya kizanzibar.
Nao baadhi ya Viongozi hao wameupongeza uongozi wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Mjini kwa kufanya ziara hiyo kwani imeweza kuwasaidia katika kuelezea masuambala mbalimbali yanayowakabili katika maeneo yao ikiwemo ya udhalilishaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.