Habari za Punde

Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wanawake na Watoto Mh.Maudline Castico Akagua Ujenzi wa Skuli ya Maandalizi Shehia ya Kipange.


WAZIRI wa Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Zanzibar. Mh.Maudline  Castico(wakwanza kushoto) akikagua jengo lenye madarasa matatu ya kusomea katika shehia ya Kipange Wilaya ya Micheweni.


WAZIRI wa Kazi Uwezeshaji Wazee,Wanawake na Watoto Zanzibar.Mh. Maudline Castico (wakwanza kulia) akizungumza na wananchi ya shehia ya Kipange Wilaya ya Micheweni mara baada ya kukagua ujenzi wa banda lenye madarasa matatu Skuli ya maandalizi Kipange.

Na Mwandishi wetu Pemba
WAZIRI wa Kazi Uwezeshaji Wanawake na Watoto Mh.Maudline Castico amewataka wazazi kisiwani Pemba kushirikiana na walimu katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma vizuri na kufaulu.

Alisema hayo wakati alipofika kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa matatu ya maandalizi katika kijiji cha Kipange Konde wilaya ya Micheweni.
Alisema, ufaulu wa wanafunzi unakwenda sambamba na upatikanaji wa ushirikiano wa dhati kati ya wazazi na walimu.

“Ili mtoto aweze kufanikiwa vizuri kielimu hatuna budi kuwa sambamba na mwalimu, mwalimu ndiye anaefahamu maendeleo ya mwanafunzi” alisema.
Sambamba na hilo aliwataka wazazi hao kufuatilia kwa karibu nyendo za watoto ili kudhibiti mporomoko wa maadili ikiwemo udhalilishaji wa watoto.

Aliongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa vitendo vya udhalilishaji ni vyema wazazi wakajenga mazoea ya kuwafahamu watu ambao wanakua karibu na watoto wao ili kuchukua hatua mapema.

Aidha waziri Castico aliwataka akina baba kuona wanawake wana daraja kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu hivyo wanapaswa kuenziwa badala ya kuwanyanyasa.

Alisema bila ya msaada , nguvu na imani ya mwanamke wanaume wasingeweza kupata mafanikio waliyonayo sasa hivyo ni lazima waoneshe shukurani kwao na kuwatunza na kuwapa heshima inayostahiki.

Mapema wakisoma risala mbele ya mgeni rasmi wazazi hao walieleza kuwa ujenzi wa madarasa hayo ulianza mwishoni mwa mwaka 2017 kufuatia changamoto ya masafa kwa wanafunzi wa maandalizi kutoka kijiji cha Kipange hadi mji wa Konde.

Walibainisha kuwa katika msimu wa mvua za masika watoto wa kijiji hicho hupata shida kutokana na hali ya barabara kujaa maji hali inayopelekea kushindwa kufika skuli mapema.
Walisema ujenzi huo ambao unatokana na nguvu ya umoja wa wananchi wa kijiji hicho na serikali hadi kufikia hatua ya kuezeka umegharimu jumla ya Tsh 4,870,500/=

Aidha waliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi waMh. Rais Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuendelea kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu, maji na barabara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.