Habari za Punde

ZSTC yatoa Mil 5 kuimarisha kitalu cha Mwanakombo

Mkurugenzi wa Masoko ZSTC  Salum Abdalla Tinde (wa pili kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya Kaskazini 'B' Rajab Ali Rajab  hundi ya Shilingi Milioni tano kwa ajili ya kuimarisha kitalu cha mikarafuu cha Mwanakombo

Na Maryam Kidiko / Maelezo .              
Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) limekabidhi Hundi ya Shilingi Milioni tano kwa Mkuu wa Wilaya  ya Kaskazini ‘B’ Rajab Ali Rajab ili kuimarisha Kitalu cha miche ya mikarafuu na mazao mengine ya viungo katika Wilaya hiyo .
Akikabidhi hundi hiyo, Mkurugenzi Masoko wa ZSTC Salum Abdalla Tinde,  kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo amesema Kitalu cha Mwanakombo kimekuwa cha mfano na hivyo kimewapa hamasa kutoa fedha hizo kukiimarisha zaidi.
Alisema kitalu cha Mwanakombo kimekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa zao la karafuu wa Wilaya Kaskazini ‘B’ kwa kutoa miche bora kwa Wakulima hao na kusaidia kuimarisha kilimo hicho na uchumi kwa jumla.
Mkurugenzi Masoko wa ZSTC aliahidi kuwa wataenelea kutoa misaada mbali mbali kwa wakulima wa zao la karafuu Unguja na Pemba ili kuzidisha uzalishaji na kutimiza lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuliimarisha zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Rajab Ali Rajab alisema ZSTC limekuwa likitoa ushirikiano mkubwa hasa katika kuimarisha zao la karafuu katika Wilaya yake na Wakulima wengi wamepiga hatua na kupata maendeleo makubwa.
Alilipongeza Shirika hilo kwa kuwapatia mikopo ya fedha na vifaa Wakulima wa karafuu hasa katika hatua za awali za msimu wa kuchuma na umekuwa ukiwasaidia kuendesha shuhuli mbali mbali kufanikisha 
Mkuu huyo wa Wilaya aliwaomba Wakulima wa karafuu wanaochukua mkopo kwa ajili ya kuchuma karafuu kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kujenga imani kwa Shirika na kujenga mazingira mazuri ya kukopeshwa msimu unaofuata.
“Nawaomba wale wote wanaokopeshwa kuirudisha mkopo kwa wakati ili kukuza pato la Taifa na kutimiza lengo lililokusudiwa,” alisisitiza Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Makame Mwadini Suleiman aliishukuru ZSTC kwa msaada wa fedha taslim shilingi milioni tano na aliahidi kuwa zitatumika katika kukiimarisha zaidi Kitalu cha Mwanakombo.
Alisema kuwa lengo lao mwaka huu ni kuwapatia wakulima miche ya mikarafuu ya kutosha na wamejipanga kuwahamasisha kuongeza mazao mengine ya viungo ya biashara yakiwemo pilipili hoho, pilipili manga na mdalasini.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.