Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Watoto Yaadhimishwa Zanzibar.

Washindi wa Pili wa Mashindano ya Qswida kwa Mwaka 2019 Mdrasatul Muuminina ya Mtaa wa Mpendae wakifanya vitu vyao wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi zao iliyofanyika katika Viwanja vya kufurahisha Watoto Kariakoo.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akizungumza katika Hafla ya kukabidhizawadi kwa washindi wa mashindano ya Qaswida yaliyoandaliwa na Bahari F.M Redio.
Mkurugenzi Mkuu wa Bahari F.M Redio Nd. Hassan Abdulla Mitawi akiwakaribisha wageni mbali mbali katika hafla ya mashindano ya Qaswida yaliyofanyika ndani ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Baadhi ya washiriki wa mashindano ya Qaswida kutoka Madrasa mbali mbali za Unguja wakifuatilia hafla ya kukabidhiwa zawadi washindi wa mashindano hayo.
Mke wa Makamu wa Pili wa Raius wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akiakabidhi Cheti kwa washindi wa Qaswida Bora kwa mwaka 2019 iliyochukuliwa na Madrasatul Darsu ya Mtaa wa Mkele.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha akiwakabidhi zawadi washindi wa Tatu wa Mashindano Madrasat Afnania ya Mwanyanya Wilaya ya Magharibi “A”.
Mama Asha akiwakabidhi zawadi washindi wa Pili wa mashindano hayo MadrasatHidayatul Muuminina ya Mtaa wa Mpendae Wilaya ya Mjini.

Mama Asha akimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Bahari F.M Nd. Hassan Abdullah Mitawi kutokana na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na edio hiyo katika kutoa Elimu kwa Uma.

Na.OthmanKhamis.OMPR.
Wazazi Nchini wameaswa kuacha tabia ya kuwafanya Watoto wao wa Kike kuwa vitega uchumi wa kujipatia mapato kwa kuweka Mahari makubwa ambayo husababisha vikwazo kwa Vijana wa Kiume wanaofikia wakati wa kutaka kufunga ndoa.
Nasaha hizo zimetolewa na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi  katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa Mashindano ya Qaswida yaliyoandaliwa na Bahari F.M Redio hafla iliyofanyika katika Uwanja wa kufurahishia Watoto Kariakoo.
Mama Asha Suleiman Iddi alisema Wazazi wengi Nchini wamekuwa na mfumo wa kulazimisha mahari makubwa pale Watoto wao wa Kike wanapochumbiwa jambo ambalo ni hatari kwa kukaribisha vitendo vya udhalilishaji vinavyoibua ubakaji katika Jamii.
Alitahadharisha kuachwa kwa tamaa hiyo ambapo mbali ya kwenda kinyume na malengo hasa ya uwepo wa ndoa kwa mujibu wa mfumo na Taratibu za Dini lakini pia haileti taswira njema katika maisha ya kila siku ya Jamii.
Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizishukuru Madrasa zote zilizojitokeza kushiriki kwenye Mashindano hayo na kuipongeza Bahari F.M Redio  kwa kuendesha zoezi hilo muhimu.
Alisema katika kuiunga mkono Bahari F.M Redio alikubali kuwa mlezi na ameahidi kujitolewa kusaidia maendeleo ya Mpango huo ili uwe wa kudumu kwa vile unawagusa moja kwa moja Wananchi.
Akisoma Risala Mwakilishi wa Bahari F.M. Redio Mwashaban Seif Ali alisema Mashindano hayo yameanza kuonyesha maelekeo wa kukubalika ndani ya Jamii kutokana na ongezeko kubwa la Washiriki kutoka Madrasa 10 Mwaka 2018 na kufikia hadi Madrasa 20 kwa Mwaka 2019.
Mwashaban alisema zoezi hilo lililoshirikisha Madrasa 20 kutoka Mikoa yote ya Kisiwa cha Unguja  lilitoa fursa kwa Majaji ambao ni Wasikilizaji wa Bahari F.M kutoa maamuzi kwa kupiga kura kupitia njia ya Simu.
Alisema lengo la mfumo huo wa mashindano uliojumuisha wasikilizaji kutoka Mikoa ya Unguja, Pemba na baadhi ya Tanzania Bara ulilenga kuwakumbusha wana Jamii umuhimu wa Ramadhani, kuheshimu Mwezi wa Ramadhani, Utukufu wa Quran pamoja na miongozo yake.
Aidha alisisitiza kwamba mfumo huo pia ulikwenda sambamba na kuihamasisha Jamii katika jitihada za kumcha Mwenyezi Muungu pamoja na kuunga mkono Serikali Kuu katika mkakati wake wa kupiga vita vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimekithiri hapa Nchini.
Mwashamba alifahamisha kwamba pamoja na kutengwa shilingi Milioni 2,200,000/- kwa ajili ya mpango huo lakini zipo changamoto zilizojitokeza katika kuendesha zoezi hilo ikiwemo Rasilmali Fedha.
Alieleza kwamba changamoto hiyo imesababisha zoezi hilo tokea kuasisiwa kwake Mwaka uliopita wa 2018 limethubutu kufanywa upande Mmoja tu wa Visiwa vya Zanzibar uliopo Unguja.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Bahari F.M Radio Ndugu Hassan Abdulla Mitawi amewaahidi Wasikilizaji wa Redio Bahari F.M  kuendeleza sifa zote zinazonogesha maisha ya Jamii kupitia Matangazo yake ya kila siku.
Nd. Mitawi alisema Watendaji wa chombo hicho cha Habari watazingatia kufikisha ujumbe kwa Jamii katika kuhamasisha masuala ya Uzalendo, kulinda Amani na Umoja ili Jamii iendelee kufaidi hazina hiyo inayokosekana katika Baadhi ya Mataifa Duniani.
Katika kuendelea kushajiisha Mashindano hayo Mama Asha akajitolea kusaidia Kompyuta Mbili, moja kwa Bahari F.M na nyengine kwa Mshindi wa kwanza pamoja na zawadi ya Fedha Taslim Shilingi Laki 800,000/- kwa Madrasa Nne zilizoshinda kwenye Mashindano hayo muhimu katika Jamii.
Katika mashindano hayo yaliyoshirikisha Madraa 20 za Unguja mshindi wa Nne ilikuwa Madrasat Mabanat ya Mtaa wa Kwaalamsha iliyojizolea shilingi Laki 300,000/-, Juzuu na misahafu wakati mshindi wa Tatu ilikuwa Madrasat Afnania ya Mwanyanya iliyopata kitita cha shilingi Laki 500,000/-. Juzuu na misahafu.
Mshindi wa pili wa mashindano hayo ni Hidayatul Muuminina ya  Mtaa wa Mpendae ambayo Mwaka uliopita ilichukuwa mshindi wa kwanza ikajipatia shingi Laki 700,000/-. Misahafu pamoja na juzuu.
Mabingwa wa mashindano hayo mwaka 2019 ni Madrasa Shamsia ya Mtaa wa Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja iliyoibuka na kitita cha Shilingi Milioni 1,000,000/- Taslim, Juzuu, Misahafu, Cheti pamoja na Kompyuta.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.