Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Afunga Mkutano wa Mawaziri wa SADC Jijini Dar es Salaam leo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihutubia wakati wa ufungaji wa Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za SADC wanaohusika na masuala ya Teknolojia ya Habari, Mawasiliano, Uchukuzi na Hali ya Hewa.uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ujenzi imara wa Miundombinu katika ukuaji wa Uchumi kwa Mataifa ya Jumuiya Maendeleo ya Uchumi ya Kusini mwa Bara la Afrika {SADC} ndio njia pekee ya kuimarisha Biashara kupitia Mfumo wa kisasa wa Habari na Mawasiliano {TEHAMA}.
Alisema mfumo wa Kidunia wa maendeleo ya Kibiashara tayari umeshabadilika mazingira yanayolazimisha  Mataifa ya SADC kwenda na wakati kwa lengo la kujiendesha yenyewe ili kuepuka kutegemea nguvu za nje ambazo wakati mwengine zinaambatana na masharti yasiyostahiki hususan Kiutamadunia.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiufunga Mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya Maendeleo ya Uchumi ya Mataifa ya Kusini mwa Bara la Afrika {SADC} uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere { JNICC } Jijini Dar es salaam.
Mkutano huo wa Kimataifa ambao pia ulijumuisha Wataalamu wa Taasisi za Mataifa ya {SADC} na Sekta Binafsi  ulikuwa akijadili masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano { TEHAMA}, Uchukuzi  pamoja na mabadiliko ya Hali ya Hewa.
Alisema Mfumo huo wa TEHAMA lioyoifanya  Duniani kuwa kiganja kutoka Kijiji unaendelea kurahisisha harakati za Kiuchumi na Biashara baina ya Mataifa yanayoshirikiana katika kuwasilisha huduma muhimu kwa Jamii husika.
Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na hatua kubwa iliyochukuliwa na Viongozi wa Mataifa ya SADC katika ngazi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wataalamu wao kufanya kazi pamoja katika kuimarisha  masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ndani ya Mataifa yao.
Alieleza kwamba uimarishaji wa mfumo huo wa Kisasa ndani ya Ukanda wa Mataifa ya Kusini mwa Bara la Afrika utasaidia kuimarisha chachu ya Maendeleo itakayokwenda sambamba na ukuaji wa ongezeko la fursa ya Ajira kwa Wananchi wake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaomba Viongozi na Wananchi wa Mataifa ya Afrika   hasa wale wa Jumuiya ya SADC  kuwa na tahadhari ya  kuzipalilia vurugu zilizotokea Nchini Afrika ya Kusini ambazo kuendelea kwake zinaweza kuwaathiri Waafrika walio wengi.
Balozi Seif alisema Rais wa Nchi hiyo Bwana Cyril Ramaphosa ameshawaomba radhi Waafrika wote kwa hitilafu iliyojitokeza Nchini mwake ya kupigwa kwa Wageni wa Mataifa mbali mbali wakiwemo wake wa Waafrika ambao wamo  Nchini humo kuendesha Maisha yao.
Alisema si jambo jema kuona Waafrika wenyewe wanafikia hatua ya kuhitilafiana kwa sababu ya fursa za ajira na kusahau udugu wao unaowaunganisha kutokana na kuingiliana kidamu, Silka na Utamaduni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Wajumbe wa Mkutano huo unaozungumzia masuala ya Tehama na zile Sekta nyengine kwamba Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kama Mwenyekiti wa SADC kipindi hichi itaendelea kushirikiana na kila mwanachama wa jumuiya hiyo katika masuala ya Maendeleo ya Uchumi.
Balozi Seif alisema wakati miundombinu katika Sekta ya Uchumi na Maendeleo inaendelea kuimarishwa fursa zozote za ajira zitakazojitokeza zinaweza kufaidisha Wananchama wa Jumuiya hiyo ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Kusini mwa Bara la Afrika {SADC}.
Mapema Waziri wa Kazi, Usafiri na Mawasiliano wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhandisi Isak Aloyce Kamwelwe alisema Mkutano huo umefuatia ule wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Sadc.
Mhandisi Kamwekwe ambae ni Mwenyekiti wa Mkutano huo alisema utaratibu uliowekwa na Uongozi wa Jumuiya hiyo umeeleza wazi kwamba Mikutanoyote inayohusu mienendo ya Jumuiya ya Sadc hufanyika katika Nchi Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya Kusini Mwa Afrika.
Alisema Wajumbe wa Mkutano huo wameongelea zaidi katika masuala ya Ushirikiano katika Ujenzi wa Njia za Reli, Mawasiliano pamoja na Mfumo wa Habari na Mawasiliano {TEHAMA}.
Alieleza kwamba inafurahisha kuona  Uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika {ADB} pamoja na Benki ya Afrika ya Kusini umesema uko tayari kuunga mkono muenendo mzima wa masuala yanayohusu Jumuiya ya Maendeleo ya SADC hasa katika Mfumo wa Kisasa wa TEHAMA uliolenga kutanua fursa za Ajira kwa Wanachama wake.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo wa Mkutano wa Mawaziri wa SADC Mhandisi Isak Kamwelwe alifahamisha kwamba suala la Biashara katika Mipaka ya Mataifa Wanachama wa SADC bado linaendelea kuwa changamoto na kuleta kero inayopunguza mwenendo wa Biashara.
Alisema Wajumbe wa Mkutano huo kutoka Mataifa 16 Wanachama wa SADC walipendekeza kuondoshwa kwa changamoto hizo za Vikwazo vya Biashara katika  Mipaka baina ya Nchi na Nchi.
Mapema Mjumbe kutoka Ubalozi wa Msumbiji Nchini Tanzania Bibi Tone tene alisema matokeo ya tabia Nchi yanayojitokeza Ulimwenguni yakaathiri pia mfumo wa mazingira kwa Nchi Wanachama linapaswa kushughulikiwa kwa pamojan.
Sekta ya Habari na Mawasiliano, Uchukuzi na Hali ya Hewa ni  muendelezo wa Mikutano mbali mbali ya SADC iliyopangwa kufanyika ndani ya kipindi cha  Mwaka Mmoja baada ya Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Bara la Afrika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.