Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Azindua Mpango Kumaliza Kipindupindu Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizindua Kitabu cha Mpango wa Kumaliza Kipindupindu Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar kulia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi na kushoto Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed, wakishuhudia Uzinduzi huo uliofanyika leo.10-9-2019.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alisema serikali inawajibu wa kuwatunza na kusimamia Afya za wananchi, kwa kuhakikisha wanaondokana na maradhi mbalimbali, ikiwemo kipindupindu.

Dk. Shein amesema hayo katika Uzinduzi wa Mpango shirikishi wa kutokomeza Kipindupindu, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakili, kikwajuni Jijini Zanzibar.

Alisema katika kufanikisha azma hiyo Serikali inaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha huduma za maji safi na salama yanapatikana kwa uhakika nchini kote.

Alisema wananchi wa Zanzibar wanahitaji kupata maji yalio safi na salama ili kuondokana na kadhia ya ugonjwa wa kipindupindu, akibainisha chanzo cha ugonjwa huo kuwa kinatokana na uchafu wa mazingira, sambamba na matumizi ya maji yasio salama.


Alisema Serikali kwa kushirkiana na washirika wa maendeleo hivi sasa imekuwa ikitekeleza miradi mbali mbali ya upatikanaji wa maji safi na salama, ili kuimarisha afya za wananchi wake.

Aidha, alisema Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa misingi ya maji ya mvua na miundombinu ya maji machafu ili kuyawezesha maji ya mvua kupita, sambamba na ujenzi wa vyoo na karo katika makazi ya wananchi.

Dk. Shein, alisema kupitia Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), Serikali imeanzisha shahada ya kwanza ya Afya ya Mazingira, kwa lengo la kupata wataalamu wengi zaidi, hivyo kulijengea uwezo Taifa katika kukabiliana na maradhi mbalimbali.

Akielezea utekelezaji wa mpango huo, Dk. Shein aliwataka watendaji wanaohusika na utekelezaji wa Mpango huo kuelekeza nguvu zao katika utoaji wa elimu kwa wananchi kupitia mikutano.

Alisema sio sahihi kwa watendaji wa mpango huo kufurahia juhudi za washirika wa maendeleo juu ya hatua yao ya kutoa fedha na kubainisha kuwa fedha hizo zipo kwa ajili ya kufanyiwa kazi, hivyo akawataka kuepuka kufanya semina nyingi ziziso na lazima.

“Nyenzo zitakuwepo kusaidia, lakini sisi wenyewe ni lazima tutekeleze”, alisema.

Aidha aliitaka Wizara ya Afya na Wizara nyengine zinazohusika na mpango huo kuongeza nguvu katika kuwafikia wananchi majumbani na katika maeneo ya skuli za msingi na Sekondari, ili kuhamasisha usafi wa mazingira.

Alisema mradi uliozinduliwa ndio jibu sahihi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu, hivyo akasisitiza haja kwa taasisi zote na jamii kushirikiana kufanikisha mpango huo.

Alisema ili kufanikisha na kupatia ufanisi mpango huo, wananchi wanawajibu mkubwa wa kutoa ushirikiano, kwa kigezo kuwa ufanisi wa mradi huo utataegemea zaidi mchango wao na dhamira ya dhati badala ya fedha.

Alisema ugonjwa wa kipindupindu, kama ilivyo kwa ugonjwa wa Malaria na Ukimwi yanaweza kuondoka kabisa, hivyo akawataka wananachi kuunga mkono juhudi za Serikali.

“Kila mmoja lazima awajibike kwa kufuata mipango iliyowekwa…………kama tulivyofanikiwa kudhibiti maradhi ya malaria na ukimwi, ni dhahiri kuwa tunaweza kupambana na cholera”, alisema.

Dk. Shein aliwapongeza washirika wa maendeleo na mashrika ya Kimataifa kwa mchango wao wenye lengo la  kuunga mkono juhudi za serikali katika kutokomeza ugonjwa wa Kipindupindu nchini.

Akigusi Historia ya Ugonjwa wa kipindupindu duniani Dk. Shein alisema wataalamu wanaeleza kuwa ugonjwa huo ulianza kujitokeza na kutambulika yapata miaka 1,019 iliyopita.

Alisema hapa Zanzibar mripuko wa kwanza wa ugonjwa huo mdogo uliwasibu wananchi wa kisiwa cha Tumbatu mwanzoni mwa mwaka 1978, wakati mripuko wa pili ambao ulikuwa mkubwa ulitokea mwezi Machi, 1978, ambapo watu wengi mjini na mashamba waliathirika.

Alisema uzinduzi wa mpango wa kutokomeza maradhi ya kipindupindu una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya sekta ya Afya na nchi kwa ujumla, kwa kuzingatia kuwa ugonjwa huo unaathari nyingi za kiuchumi na kijamii.

Katika uzinduzi huo, Dk. Shein alipata fursa ya kukata utepe wa vitabu vya mpango na kuvigawa kwa Mawaziri mbali mbali wanaohusika.

Mapema, Waziri wa Wizara ya Afya, Mhe.Hamad Rashid Mohammed alisema ufanisi na ufumbuzi wa kuwepo ugonjwa wa kipindupindu nchini, utatokana na mchango wa wananchi, hususan katika suala zima la kudumisha usafi wa mazingira, miili yao pamoja na makaazi.

Alisema ugonjwa huo kama ilivyo kuwa kwa ugonjwa wa Kichocho na Malaria unaweza kuondoka nchini, hivyo akawataka wananachi kuunga mkono juhudi za serikali ilio chini ya Uongozi wa Dk. Shein.

Aliwataka wananchi kushirikiana, akibainisha kuwa utatuzi wa kuwe po kw a ugonjwa huo hakuhitaji fedha, bali dhamira za kweli.

“Cholera iko ndani ya uwezo wetu, haitaki uchawi, inataka usafi na nia njema”, alisema.
Hamad alisema ili Taifa liweze kufaidika kiuchumi kutokana an sekta ya Utalii, kuna umuhimu wa kuzingatia usafi wa mazingira na usalama wa nchi, kwa kigezo kuwa hakuna watalii wataozuru nchini bila ya kuwepo mambo hayo.

Nae, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Asha Ali Abdalla, akitowa maelezo yakitaalamu juu ya mpango huo, alisema kuwa ni mpango wa miaka kumi kuazi (2018-2027), utakaohusisha Wizara na sekta mbali mbali katika utekelezaji wake.

Alisema kimsingi ugonjwa wa kipindupindu umebainika kujitokeza mara kwa mara hapa nchini, mara baada ya kumalizika kwa mvua za msimu, zikiwemo za Vuli na Masika, hivyo kuleta athari kubwa kwa jamii, ikiwemo vifo.

Alisema mpango huo unalenga kuondosha kabisa vimelea vinavyosababisha ugonjwa huo kwa kusimamia sheria na miongozo inayosimamia usafi wa mazingira na chakula.

Aidha, alisema mpango unalenga kuwepo hatua za haraka zitachukuliwa mara ugonjwa huo utakapojitokeza pamoja na kupanua wigo na ufanisi, huduma za kinga na upatikanaji wa maji safi na salama.

Nao, washirika wa maendeleo kutoka mashirika ya WHO, UNICEF na KOIKA ,walieleza kuwa kipindupindu ni maradhi yanayoaithri zaidi jamii ya watu maskini katika maeneo mbalimbali ya mkusanyiko, ikiwemo kambi za wakimbizi.

Walisema kuna haja katika utekelezaji wa mpango huo kuwepo mashirikiano ya pamoja kati ya taasisi na wananchi, sambamba na kutilia mkazo uimarishaji wa afya kupitia usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji safi na salama.

Sambamba na hayo, walisema katika kukabiliana na ugonjwa huo, kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo vyoo katika makaazi ya watu pamoja na kuwepo kampeni maalum kuanzia ngazi za skuli za msingi ,kusimamia usafi wa mwili, ikiwemo kunawa mikono kabla ya kula.

AbdiShamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.