Habari za Punde

China Yapongezwa Kwa Kuendeleza Utamaduni wa Kuiunga Mkono Zanzibar Kuimarisha Sekta Mbalimbali


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Balozi Mdogo wa China anayefanyia kazi zake Zanzibar.Mhe. Xie Xiuowu, akiwa na Katibu wa Kamati Kuu ya Chama Cha Kikomunisti na” Vice General Manager of China National Research Institute of Food Fermentation Industries Co.Ltd “ Bw. Dong Weihong, walipofika Ikulu kwa mazungumzo leo.

JAMHURI ya Watu wa China imepongezwa kwa kuendeleza utamaduni wake wa kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo kwa kuleta wataalamu kutoka nchini humo kuja kutoa mafunzo hapa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa pongezi hizo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Katibu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Dong Weihong ambaye pia ni Makamo Mkuu wa Taasisi ya ‘China National Research Institute of Food Fermentation Industries’ ya China.

Dk. Shein alieleza kuwa Jamhuri  ya Watu wa China imeanza kuleta wataalamu wake hapa Zanzibar tokea miaka ya 60 mara baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 hivyo, ujio wa wataalamu na wakufunzi kutoka nchi hiyo kuja kutoa mafunzo ya mapishi  na ukarimu yatakayoendeshwa na Taasisi hiyo ni muendelezo wa utamaduni huo.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa Jamhuri ya Watu wa China na Zanzibar zina historia ya muda mrefu katika kushirikiana kwa azma ya kuwaleta wataalamu na wakufunzi wake hapa Zanzibar kwani imeshawaleta wataalamu wake hapa Zanzibar katika sekta mbali mbali zikiwemo afya, kilimo, viwanda, elimu na nyenginezo.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar ina furahishwa na juhudi za nchi hiyo za kuendeleza uhusiano na ushirikiano wake katika kuendeleza na kuimarisha sekta za maendeleo.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa mashirikiano hayo ya pamoja kati ya Taasisi hiyo na Zanzibar katika kufikia uwamuzi wa kuleta wataalamu wake kwa mara ya tatu hapa Zanzibar kuja kutoa mafunzo ya mapishi, ukarimu pamoja na huduma nyengine za nyumbani ni jambo la busara.

Alieleza kuwa juhudi hizo ni hatua moja wapo za Jamhuri ya Watu wa China kuunga mkono mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuendeleza sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii kwani utaalamu huo wanaoutoa kwa jamii ya kizanzibari pia, ni kivutio kimoja wapo cha watalii kutoka nchini China na nchi nyenginezo.

Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa juhudi hizo zina manufaa makubwa hivi sasa na hata hapo baadae kwani ni kivutio kimoja wapo cha kupanua wigo katika masuala mazima ya vmapishi ya vyakula vya aina mbali mbali.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Jamhuri ya Watu wa China katika kuhakikisha sekta za maendeleo zinaimarika sambamba na kuimarisha udugu na urafiki uliopo.

“Ni jambo la kufurahisha sana kwani Jamhuri ya Watu wa China walianza kutusaidia kwa kutuletea wataalamu wa afya, kilimo, viwanda, elimu lakini leo inatuletea waatalamu wa mapishi na ukarimu kwa kweli ni jambo la kupongezwa sana”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa kufanyika mafunzo hayo hapa Zanzibar kunatoa ahueni na nafuu ya gharama za uendeshaji na utoaji nafasi kubwa zaidi kwa watendaji watakaopata fursa ya mafunzo hayo.

Pia, Rais Dk. Shein alieleza kuwa mafunzo hayo yataimarisha uhusiano na ushirikiano katika kuimarisha sekta ya elimu na utalii kwa kupitia Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar kiliopo Maruhubi ambacho hivi sasa kimeunganishwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Mapema Balozi mdogo wa China Xie Xiaowu alimueleza Dk. Shein kuwa Jamhuri ya Watu wa China inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na kuahidi kuendelea kutoa nafasi za masomo nchini humo sambamba na kuleta wakufunzi kuja kutoa mafunzo Zanzibar.

Balozi Xie Xiaowu alimueleza Rais Dk. Shein kuwa urafiki wa Jamahuri ya Watu wa China na Zanzibar ni wa miaka 55 hivi sasa, hivyo unaonesha wazi kuwa una historia kubwa na kuna kila sababu ya kuendelezwa na kudumishwa kwa nguvu zote.

Nae Katibu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Makamo Mkuu wa Taasisi ya ‘China National Research Institute of Food Fermentation Industries’ kutoka China Dong Weinhong amempongeza Dk. Shein kwa juhudi zake za kuhakikisha mafunzo hayo yanafanyika.

Kiongozi huyo alieleza kuwa juhudi hizo za Rais Dk. Shein ni lazima ziungwe mkono kwani zinaonesha wazi kuwa ana hamu na nia ya kwuasaidia wananchi wake katika sekta zote za maendeleo na kuahidi kuwa Taasisi hiyo itasimama bega kwa bega na yeye. Aliongeza kuwa hatua hiyo inazidi kujenga uhusiano na ushirikiano mwema kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Zanzibar.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza kesho Septemba 11, 2019 hadi Oktoba 10, 2019 ambayo yatawashirikisha watendaji 45 kutoka Taasisi za Serikali na Binafsi wakiwemo kutoka Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Baraza la Mapinduzi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Chuo Cha Utalii Maruhubi, Uwanja wa Ndege na Hoteli ya Verde.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.