Na. Irene B.
Serikali imeridhia kufuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 ambayo yamepoteza sifa na imeamua yagawiwe kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na mifugo.
Uamuzi huo umefikiwa leo (Jumatatu, Septemba 23, 2019) kweye kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa mara baada ya kikao hicho, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Mawaziri wa kisekta wakiongozwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi walichambua na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi nchini iliyowasilishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha leo.
“Mawaziri walichambua na kubaini kuwa vijiji vyenye migogoro ni 975 na siyo 366 kama ilivyotangazwa awali, Baraza limeamua kwamba vijiji 920 vitabaki ndani ya hifadhi, mipaka irejewe upya, vipatiwe vyeti vya ardhi vya kijiji pamoja na kupangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi,” amesema na kuongeza kuwa orodha ya vijiji hivyo itatangazwa baadaye.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeridhia Misitu ya Hifadhi saba yenye ukubwa wa ekari 46,715 iliyopoteza sifa itolewe kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na mifugo ili kuwaondolea kero za uhaba wa ardhi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeridhia kumega hifadhi za misitu 14 kwa ajili ya kilimo na mifugo na kufuta mashamba 16 yasiyoendelezwa ili yapangiwe matumizi ya kilimo na mifugo.
“Vijiji 55 vilivyobaki vinaendelea kufanyiwa tathmini ya kina maeneo yaliyobaki ndani ya hifadhi na kuwasilisha mapendekezo yake kwa ajili ya uamuzi. Uchambuzi na taarifa itatolewa,” amesema na kuongeza kuwa orodha ya maeneo ya vijiji, mapori ya wanyama, misitu na mashamba yaliyofutwa itatangwa baadaye.
Pia amesema Baraza limeamua ardhi ya mita 500 zilizotengwa kama buffer zone (eneo kinga) kwenye maeneo ya vijiji vinavyopakana na hifadhi za wanyama ziachiwe vijiji husika na wananchi wasiondolewe kwenye maeneo hayo.
Ameyataja maamuzi mengine yaliyofikiwa kwenye kikao hicho kuwa ni Ofisi ya Makamu wa Rais imetakiwa ikamilishe mwongozo utakaobainisha matumizi ya ardhi ndani ya hifadhi ya mita 60 za mito, vyanzo vya maji, maziwa na bahari.
Maamuzi mengine ni kuzitaka Wizara na taasisi zote za Serikali zilinde maeneo yao kwa kuweka alama za kudumu zinazoonekana; na kwamba wananchi hawaruhusiwi kuvamia maeneo mapya na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya uvamizi wowote kuanzia leo.
Januari, mwaka huu, Rais Magufuli alitoa maagizo kwa Mawaziri nane wa sekta zinazohusika na matumizi ya ardhi wachambue na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi nchini.
Maagizo hayo yalikuwa ni pamoja na: Kutoviondoa vijiji na vitongoji 366 vilivyomo ndani ya hifadhi; Kubainisha maeneo ya hifadhi ambayo yamepoteza sifa ili yaweze kugawiwa kwa wananchi kwa shughuli za ufugaji na kilimo na kuhakiki na kurekebisha mipaka baina ya hifadhi za misitu, wanyama na makazi.
Mengine ni kumega baadhi ya hifadhi za Taifa, mapori tengefu na misitu, kuwagawia wafugaji na wakulima; Kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi; Kupitia upya Sheria ya Vyanzo vya Maji inayozungumzia uhifadhi ndani ya mita 60; Kuwasilisha mapendekezo ya kufutwa mashamba yasiyoendelezwa na kugawa kwa wananchi kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo na kuendelea kulinda na kuhifadhi maeneo ya hifadhi za misitu, wanyamapori na vyanzo vya maji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, SEPTEMBA 23, 2019.
No comments:
Post a Comment