Habari za Punde

Kadi ya Mpiga Kura Haitatumika Kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Dkt. Mahera ameeleza kwamba zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linaendelea kwa sasa katika mikoa ya Tabora, Katavi na Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma ambako uboreshaji utafanyika kuanzia tarehe 14 Oktoba hadi tarehe 20 Oktoba mwaka huu.Ameongeza kwamba zoezi hilo litaendelea kwenye mikoa ya Songwe, Dodoma na Singida kuanzia tarehe 26 Oktoba hadi tarehe 01 Novemba 2019.
Na. Idara ya Habari-NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa ufafanuzi kwa wananchi juu ya mazoezi mawili tofauti yanayoendelea Nchini ya kuandikisha wapiga kura na kuwatahadharisha kwamba Kadi ya Mpiga Kura inayotolewa na Tume haitatumika kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwenzi ujao.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo (10.10.2019), Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Dkt. Wilson Mahera Charles amesema kwamba uandikishaji unaoendelea ambao ulianza tarehe 08, Oktoba 2019 unahusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 24 Novemba 2019 ambao hausimamiwi na Tume.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kuwataarifu wananchi kuwa uandikishaji unaofanyika kuanzia tarehe 08, Oktoba 2019 hadi tarehe 14, Oktoba 2019 na kusimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI) kupitia Halmashauri mbalimbali kote Nchini unahusika na uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 24 Novemba 2019. Mwananchi asipojiandikisha hataweza kupiga kura katika uchaguzi huo,” amesema Dkt. Mahera.
Aliongeza kwamba mwananchi ambaye hatajiandikisha kwenye uandikishaji unaofanywa na OR-TAMISEMI hatapata fursa ya kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba 24 mwaka huu, hata kama atakuwa na Kadi ya Mpiga Kura inayotolewa na Tume na kwamba uchaguzi huo hausimamiwi na Tume bali unasimamiwa na OR-TAMISEMI
Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye zoezi hilo la kujiandikisha ili wapaete fursa ya kuwachagua viongozi wa mitaa yao siku hiyo ya tarehe 24 Novembe 2019.
Aidha, Dkt. Mahera amesema kwamba Tume kwa mujibu wa Ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ina jukumu la kuandikisha Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara.
 “Uandikishaji huo (wa OR-TAMISEMI) ni tofauti na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaofanywa na Tume kwenye mikoa mbalimbali Nchini. Uboreshaji huu unahusu Uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani wa Tanzania Bara utakaofanyika mwakani 2020,” amesema.
Dkt. Mahera ameeleza kwamba zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linaendelea kwa sasa katika mikoa ya Tabora, Katavi na Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma ambako uboreshaji utafanyika kuanzia tarehe 14 Oktoba hadi tarehe 20 Oktoba mwaka huu.
Ameongeza kwamba zoezi hilo litaendelea kwenye mikoa ya Songwe, Dodoma na Singida kuanzia tarehe 26 Oktoba hadi tarehe 01 Novemba 2019.
“Wanaostahili kujiandikisha ni wale ambao wana miaka 18 na wale ambao watafikisha miaka 18 mwakani (2020) kabla ya uchaguzi, lakini pia zoezi linawahusu wale ambao kadi zao zimeharibika au zimepotea ili wapate fursa tena ya kuwepo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” alismema Dkt. Mahera.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.