Naibu Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akiongea na Mama Loisa Kamwaya (aliyevaa
kilemba) akiwa miongoni mwa Watanzania walioolewa na Wanamimbia waliokaa Wilaya
ya Kongwa mkoa wa Dodoma wakati wa kupingania uhuru wa nchi za Kusini mwa
Afrika. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Deogratius Ndejembi.
Na
Eleuteri Mangi, Kongwa
Serikali
inaendelea kubainisha maeneo yaliyotumiwa na wapingania uhuru wa nchi za Kusini
mwa Afrika ambayo yanasimamiwa kupitia Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika
iliyopo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Akiwa
katika ziara ya kikazi wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakati akitembelea maeneo ya historia ya
Ukombozi wa Afrika, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema
kuwa Serikali kupitia wizara hiyo inaandaa sheria ya kulinda na kuhifadhi
urithi wa ukombozi wa Afrika unaopatikana nchini.
“Lengo
kubwa ni kuhakikisha maeneo haya yanalindwa kisheria ili yaweze kutumika kama
vivutio vya utalii wa kiutamaduni pamoja na utalii wa kihistoria kwa sababu huu
ni urithi muhimu wa historia nzuri ya nchi yetu, haya ni maeneo yaliyotumika
kusaidia ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika” alisema Naibu Waziri Shonza.
Katika
kutekeleza Programu ya Uhifadhi na Uendelezaji wa historia ya Ukombozi wa
Afrika, Wizara inaendelea kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo, ukarabati wa
jengo lililokuwa la Kamati ya Ukombozi ya iliyokuwa Umoja wa Nchi Huru za
Afrika (OAU) ambayo kwa sasa ni Umoja wa Afrika (AU).
Kazi
nyingine ambazo Serikali imekamilisha ni uandaaji wa tovuti ya Programu,
ubainishaji wa maeneo yaliyotumika wakati wa harakati za ukombozi, utambuzi wa
nyaraka na vitu mbalimbali vinavyohusiana na harakati hizo pamoja na kufanya
mahojiano na watu walioshiriki au kushuhudia harakati za ukombozi wa Afrika
ambayo yamehifadhiwa kwa njia ya kidigitali.
Mji
wa Kongwa kihistoria ni kitovu cha harakati za Ukombozi wa Afrika kwani
harakati zote za mapambano ya kutafuta uhuru zilianzia Kongwa na baadaye
zikaendelea katika maeneo mengine nchini kama sehemu ya kupanua wigo wa
harakati hizo na huduma kwa Wapigania Uhuru.
Kwa
upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Deogratius Ndejembi amesema kuwa Kongwa ni eneo
kongwe lililotumiwa na Wapigania uhuru kutoka vyama mbalimbali vya Ukombozi
kutoka nchi za Kusini mwa Afrika.
Aidha,
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa eneo hilo lilitumika kwa ajili ya mafunzo kwa
wapigania uhuru ambapo kwa sasa lina vielelezo muhimu vya kihistoria vilivyopo
katika eneo hilo yakiwemo maeneo ya Handaki alilokuwa akilitumia Samora Mashel,
nyumba za Makazi kwa wapigania uhuru, majengo ya shule ya sekondari Kongwa, eneo
la Mafunzo ya kijeshi, kiwanja cha ndege na makaburi ya wapigania uhuru.
Maeneo
mengine ya kihistoria ni makaburi ya mashujaa wa harakati za ukombozi ambayo
jumla yake ni 11; makaburi matano ya wapigania uhuru kutoka Msumbiji, makaburi
matatu ya wapigania uhuru kutoka Afrika Kusini na makaburi matatu ya wapigania
uhuru kutoka Namibia.
Naibu
Waziri Shonza yupo katika ziara ya kikazi kutembelea maeneo ya ya historia ya ukombozi
wa Afrika katika mikoa ya Dodoma wilaya ya Kongwa, Morogoro wilaya Kilosa,
Manispaa ya Morogoro pamoja na Mkoa wa Pwani wilaya za Chalinze na
Bagamoyo.
No comments:
Post a Comment