Habari za Punde

Balozi Seif Azungumza na Ujumbe wa Madaktari Bingwa wa Moyo Kutoka Nchini Isreal

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.,Balozi Seif Ali Iddi akionyesha furaha yake kutokana na ujio wa Timu hiyo ya Madaktari Bingwa wa kuja kutoa huduma za Afya Visiwani Zanzibar.
Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya kuhudumia Maradhi ya Moyo kwa Watoto {SACH} kutoka Nchini Israel wakiwa makini kufuatilia nasaha za Balozi Seif Ali walipofanya mazungumzo yao.
Kiongozi wa Taasisi ya kuhudumia Maradhi ya Moyo kwa Watoto {SACH} Kutoka Nchini Israel Dr. Mara Chapira akielezea Mfumo wa majukumu yao katika kutoa huduma za Matibabua ya Moyo kwa Wagonjwa wa maradhi hayo.kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi walipofika Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya kuhudumia Maradhi ya Moyo kwa Watoto {SACH} kutoka Nchini Israel pamoja na Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis.OMPR. 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara inayosimamia Masuala ya Afya Zanzibar imeshajipanga kukabiliana na Virusi hatari vya Corona vinavyosababisha Homa Kali inayoambatana na Mafua vikiwa vimeibuka hivi karibuni Nchini Jamuhuri ya Watu wa China.
Hatua hiyo ya Serikali imechukuliwa kufuatia zaidi ya Mataifa Kumi Ulimwenguni kuthibitisha kutokea kwa kesi za maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo hadi sasa ni China pekee ndio iliyoripotiwa kupata wahanga wa maradhi hao.
Timu ya Wizara ya Afya Zanzibar ikiongozwa na Katibu Mkuu wake Bibi Asha Ali Abdulla ilitoaTaarifa hiyo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kumaliza mazungumzo yao na Madaktari Bingwa wa Taasisi ya kuhudumia Maradhi ya Moyo kwa Watoto {SACH} kutoka Nchini Israel.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Ali  Salum Ali alisema Kamati ya Majanga kupitia Kitengo Maalum kilichoanzishwa inamalizia matayarisho kujiandaa na kazi hiyo baada ya kupata nyenzo kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni {WHO}.
Dr. Ali alisema Wataalamu wa Shirika la Afya Ulimwenguni wameshatoa muongozo wa jinsi ya kukabiliana dhidi ya virusi hivyo hatari vya Corona kama vitaripotiwa Nchini ambavyo mafua ni miongoni mwa dalili kubwa ya Ugonjwa huo.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bibi Asha Ali Abdulla alisema kinachozingatiwa zaidi kwa wakati huu ni kwa Wataalamu wa Afya kujipanga katika kutoa Elimu itakayowasaidia Wananchi kujiweka tayari kukabiliana na Virusi vya  Corona.
Katibu Mkuu Asha alisema wakati jitihada hizo zikiendelea Taasisi, Mashirika, Jumuiya za Kiraia pamoja na Wadau wakubwa Wananchi wanapaswa kubeba jukumu katika kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira ndio jibu la kwanza la kujiepusha na maambukizi ya maradhi mbali mbali yanayoikumba Jamii.
Virusi vya Corona viligundulika kwa mara ya kwanza mwezi Septemba Mwaka 2012 huko Saudi Arabia katika nchi za Mashariki ya kati na kuendelea  kusambaa Ugonjwa huo katika nchi za Mashariki ya kati ikiwemo Jordan, Qatar, na Falme za Kiarabu (UAE).
Ndani ya Bara la Ulaya, Virusi vya Corona vimethibitishwa kutokea katika nchi za Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza na Barani Afrika katika nchi ya Tunisia ukiendelea kuwepo kwenye nchi hizo kwa kiwango kidogo kuanzia mwaka 2012 hadi Aprili 2015.                                                                
Ongezeko la Virusi vya Corona limejitokeza zaidi kuanzia tarehe Mwezi Mei, 2015 katika nchi ya Jamuhuri ya Korea na hadi Mwezi Juni, 2015, watu 167 walithibitishwa kukumbwa na Homa kali ya Virusi hivyo ambapo Watu  24 walipoteza maisha.
Akizungumza na Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya kuhudumia Maradhi ya Moyo kwa Watoto {SACH} kutoka Nchini Israel Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema mfumo wa Wataalamu hao kuja Nchini kutoa huduma za Matibabu ya Moyo unatoa fursa kwa wagonjwa wengi kupata huduma hiyo muhimu.
Balozi Seif alisema Wananchi wengi hasa wale wenye kipato cha chini wamefaidika na Mfumo huo kwa kupunguza gharama za Matibabu ya kuwapeleka Nje ya Nchi Wagonjwa wao tokea kuasisiwa kwa Mpango huo ulioanzishwa mwishoni mwa Miaka ya Tisini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushukuru Uongozi wa Taasisi ya kuhudumia Maradhi ya Moyo kwa Watoto {SACH} kutoka Nchini Israel kutokana na huduma inazotoa zinazoendelea kuleta faraja kwa Wananchi waliowengi Nchini.
Balozi Seif  alikumbusha umuhimu wa kuongeza ushirikiano kati ya Mabingwa hao wa Israel na Madaktari Wazalendo ili kufanikisha Kazi hiyo muhimu inayogusa Maradhi yanayohitaji umakini wa hali ya juu yakiwa pia na gharama kubwa.
Mapema Kiongozi wa Taasisi ya kuhudumia Maradhi ya Moyo kwa Watoto {SACH} Kutoka Nchini Israel Dr. Mara Chapira alisema Timu yake  inatarajiwa kuwafanyia Uchunguzi Watoto wapatao 400 katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambao wanasumbuliwa na Maradhi ya Moyo ndani ya Siku Tano za uwepo wao Zanzibar.
Dr. Chapira alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  kwamba wale Watoto watakaobainika kuwa na sababu za kufanyiwa huduma za Upasuaji utaratibu wa kuwasafirisha Nchini Israel utapangwa kama ilivyokuwa vipindi vilivyopita.
Kiongozi huyo wa Taasisi ya kuhudumia Maradhi ya Moyo kwa Watoto {SACH} kutoka Nchini Israel alithibitisha furaha yake kutokana na Ushirikiano unaopata Timu yake na kupelekea kujihisi kuwa kama wana Familia ya Zanzibar.
Mwishoni mwa Mwaka 2012 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alibahatika kuwatembelea Watoto wa Zanzibar waliliopata huduma za Upasuaji wa Maradhi ya Moyo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Sach iliyopo Mjini Tela Vive Nchini Israel.
Wasimamizi wa Wagonjwa hao kutoka Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja walielezea faraja yao kutokana na huduma walizopatiwa Wagonjwa wao baada ya kusumbuliuwa na maradhi ya Moyo wa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.