Habari za Punde

Ufunguzi Majengo ya Madrasa na Dakhalia Bwejuu Mkoa Kusini Unguja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe kuzindua , Majengo Mawili ya Skuli ya Charity {Madrasa na Dakhalia Bwejuu katika shamra shamra za Sherehe za Maadhimisho ya kutimia Miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.


Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Watanzania wanapoadhimisha Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar lazima wale walioshuhudia wajikumbushe wakati kile  Kizazi Kipya kinapaswa kusoma Historia ili kujua vyema dhamira iliyopelekea kufanywa kwa Mapinduzi hayo.
Alisema Chama cha Afro Shirazy Party  {ASP} kilikuwa kikishinda kila mara kwenye chaguzi za vyama vingi wakati kikipigania kujikomboa kutoka katika makucha ya kidhalimu lakini ghilba na dhulma ndizo zilizokuwa zikitumiwa na mabeberu hao katika kuviza Demokrasia ya Wananchi waliowengi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Bwejuu mara baada ya kuzindua ,Majengo Mawili ya Skuli ya Charity {Madrasa na Dakhalia ikiwa ni shamra shamra za Sherehe za Maadhimisho ya kutimia Miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Alisema dhamira hiyo ndio iliyopelekea Wananchi wa Zanzibar chini ya Uongozi wa Jemedari wa Visiwani hivi Marehemu Mzee Abeid Aman Karume kuondoa mzizi wa fitina Januari 12 Mwaka 1964 ili kurejesha Heshima, Haki na Usawa kwa Wananchi walio wengi wa Visiwa vya Unguja na Pemba waliyoikosa kwa zaidi ya Karne Mbili nyuma.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wakati Watanzania wanaadhimisha Miaka hiyo 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar Watoto wa Visiwa hivi lazima wadhamirie kusoma kwa bidii kwa vile tayari wameshatengenezewa fursa na Mazingira ya kufanya hivyo.
Balozi Seif alieleza kwamba kazi inayowakabili kwa sasa Watoto wote ni kusoma kwa nguvu zao zote katika malengo ya kwenda sambamba na mabadiliko makubwa ya Sayansi na Teknolojia yaliyoikumba Dunia kwa wakati huu.
“ Serikali Kuu inaendelea kutengeneza fursa katika kila kada na kilichobakia ni juhudi za Wanafunzi wenyewe katika kufikia dhamira hiyo muhimu katika mustakabala wa maisha yao ya baadae”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitanabahisha kwamba uwezo wa Wanafunzi kufikia malengo hayo upo kwa vile mazingira ya kupata Taaluma katika ngazi mbali hadi Udaktari unapatikana hapa hapa Zanzibar ndani ya Vyuo Vikuu vilivyoanzishwa akiviainisha kuwa ni pamoja na SUZA na  ZU vilivyopo Tunguu pamoja na Sumeit cha Chukwani.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Elimu ni Silaha njema inayoweza kutumiwa wakati wowote ule licha ya upungufu wa Ajira iliyopo Nchini hivi sasa inayotokana na ongezeko kubwa la wasomi wanaomaliza Elimu ya Sekondari pamoja na Vyuo Vikuu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza na kuwashukuru Wananchi wa Bwejuu kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo kwenye Sekta ya Elimu kwa kuanzisha Mradi huo wa Skuli utakaosaidia jitihada za Serikali katika kusambaza Elimu kwa Watoto wa Visiwa vya Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi aliahidi kuunga mkono jitihada za Wananchi hao kwa kuchangia Charahani kwa Vile Skuli hiyo tayari  imeanzisha Madarasa ya Ushoni kwa kuwaandaa Vijana katika Miradi ya Ujasiri Amali au Kompyuta kulingana na Mahitaji halisi ya Skuli hiyo kwa Vifaa hivyo vya aina mbili.
Akitoa Taarifa ya Kitaalamu ya Mradi huo wa Kijamii Katibu Mkuu Wizara ya Eimu na Mafunzo ya  amali Zanzibar Dr. Idriss Muslim Hijja alisema zaidi ya Shilingi za Kitanzania Milioni Mia 682,000,000/- zimetumika kugharamia Mradi huo Mkubwa.
Dr. Idriss alisema Gharama hizo pamoja na mambo mengine zimeainisha katika upatikanaji wa Vitanda kwa Wanafunzi wanaojiandaa na Mitihani, Darasa la Kompyuta, Maktaba, Ofisi za Walimu ikiwemo pia ile ya Mkurugenzi wa Mradi huo.
Alisema inapendeza kutoa Skuli hiyo ya Charity yenye Madarasa Saba na Wanafunzi 449 inatumia mkondo Mmoja tu wa asubuhi kama zilivyo Skuli zote za Wilaya ya Kusini jambo ambalo litatoa fursa nzuri kwa Wanafunzi wake kupata muda mkubwa wa ziada wa kujisomea hasa pale wanapokaribia kufanya Mitihani.
Mapema akimkaribisha Mgeni Rasmi kawenye hafla hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma alisema Ujenzi wa Dakhalia  ni Moja ya Mikakati bora inayowajengea Wanafunzi kupata muda wa ziada wa kujisomea.
Waziri Riziki aliwapongeza Wananchi wa Bwejuu na wafadhili waliojitokeza kuasisi Mradi huo hasa Wananchi wa Oman wenye asili ya Zanzibar kutokana na jitihada zao zinazoendelea kusaidia Miradi ya Maendeleo ikiwemo Sekta ya Elimu, Afya pamoja na Vifaa vya Miundombinu ya Mawasiliano.
Mradi wa Skuli ya Charity Bwejuu ulioanzishwa na Wananchu wenyewe Mnamo Mwaka 2014 ukianza na Wanafunzi 25 ulilenga kuwarejesha masomoni Watoto walioacha Skuli, Myatima pamoja na Watoto wenye Mahitaji Maalum, ikiwemo pia Futari wakati wa Mwezi wa Ramadhani kmwa Wazee wasiojiweza.

Waziri wa Elimu Mh. Riziki Pembe akihakiki maandishi kwenye Bango la Uzinduzi wa Majengo ya Skuli ya Charity Bwejuu mara baada ya Balozi Seif kuzindua rasmi.
Balozi Seif na Viongozi wengine wa Serikali wakitembelea maeneo mbali mbali ya Skuli ya Kijamii ya Charity ya bwejuu baada ya kuzindua rasmi.
Balozi Seif akiangalia baadhi ya Nguo zilizoshonwa na Wanafunzi wa Darasa la Ushoni katika Skuliu ya Charity ya Bwejuu Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar pamona na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kukamilika kwa Hafla ya Uzinduzi wa Majengo Mawili ya Skuli ya Charity {Madrasa na Dakhalia Bwejuu.
Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Al- Hafi Hamid Kushoto akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mwishoni mwa uzinduzi wa Majengo Mawili ya Skuli ya Charity {Madrasa na Dakhalia huko Bwejuu.
Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.