Habari za Punde

Majaliwa - Tutaendelea Kushirikiana na Madhehebu Yote Nchini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza  katika kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W,   Mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar es salaam, Februari 16, 2020. Wa pili kushoto ni  Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi Bin Ally. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza  katika kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W ,  Mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar es salaam, Februari 16, 2020. Wa pili kushoto ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na  Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar  Zuberi Bin Ally katika kumbukumbu ya kuzaliwa kwa  Mtume Mohammad S.A.W ,  Mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar es salaam
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Abubakar Zuberi Bin Ally (kulia) wakati aliposhiriki katika kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W. , Mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar es salaam, Februari 16, 2020. Wa pili kulia ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam, Al Hadi Musa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua na kuheshimu dini zote nchini,hivyo itaendelea kutoa ushirikiano kwa madhehebu yote katika kutunza na kulinda amani.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Februari 16, 2020) kwenye Kumbukumbu ya Mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam iliyoandaliwa na Nida Textile Mills (T) ltd, na kufanyika katika mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar-es-Salaam.

Amesema amani ndiyo msingi wa kila binadamu kufurahia maisha ya dunia na kufanya ibada zake kulingana na imani yake. “Kwa hiyo,tunapoazimisha mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam, tuna kila sababu ya kumuenzi kwa kufuata mafundisho yake.“ 

Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Serikali kwa upande wake inatambua na itaendelea kuthamini, mchango wa dini, taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali na hata mtu mmoja mmoja katika kutunza na kulinda amani ya nchi yetu. 

Hivyo, Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa dini zote na jamii kwa ujumla waendelee kuvumiliana na kustahamiliana hususan pale zinapotokea tofauti miongoni mwao, lengo likiwa ni kudumisha amani na ulivu uliopo nchini. 

“Kuvumiliana na kustahamiliana ndiko kulikotufanya tuendelee kuwa wamoja na kuitunza neema hii kubwa ya amani katika nchi yetu. Kila mmoja wetu anapaswa kutambua kuwa anao mchango mkubwa katika kutunza na kuimarika kwa amani ya nchi yetu.”

Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo ya Mazazi ya Mtume Muhammad (S. A. W), Waziri Mkuu amesema kwamba hiyo ni fursa muhimu kwa waislamu wote kuyasoma na kuyatafsiri kwa kivitendo maisha ya Bwana Mtume katika mfumo wao wa maisha ya kila siku ili kuyafanya maisha yao hapa duniani yawe bora zaidi.

“Tukio hili la leo ambalo nimefahamishwa kuwa linafanyika kwa mwaka wa 25 sasa, ni kielelezo cha umoja, mapenzi na undugu miongoni mwetu. Katika Quran Surah ya 49 (Al-Hujurat) ayah ya 10, Mwenyezi Mungu anatufahamisha kuwa ’hakika waumini ni ndugu.......’ Kwa msingi huo, tukiwa Waislamu suala la kuimarisha umoja, undugu na ushirikiano katika nyanja zote ni wajibu wa kila mmoja wetu.“

Kadhalika, Waziri Mkuu ameongeza kuwa Mtume Muhammad (S.A.W) naye katika kusisitiza suala hilo la umoja, kwenye hotuba yake ya kuaga alihimiza kuwa mtu yeyote yule hawezi kuwa bora dhidi ya mwingine kwa sababu tu ya rangi yake au kabila lake lakini kitu pekee kitakachompa yeye daraja hilo la kuwa bora ni kutenda haki na kumuogopa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Awali, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakari Bin Zuberi alisema katika kuadhimisha Mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) waislamu nchini wanapaswa waendelee kuwa watulivu na wasikivu wa kila jambo linalotolewa kwao na viongozi.

Maadhimisho hayo yamehudhuliwa na masheikh na viongozi wa Serikali kutoka maeneo mbalimbali nchini. Pia yamehudhuriwa na masheikh kutoka nchi za Paksani, Iraq na Misri ambao kwa ujumla wao wameisifu Serikali ya Tanzania kwa kudumisha amnai, utulivu pamoja na umoja.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, FEBRUARI 16, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.