Habari za Punde

Mwanafunzi Aliyedaiwa Kumpa Mimba Mwanafunzi Mwenzake Ahamishwa Skuli

NA MWAJUMA JUMA
UONGOZI wa skuli ya sekondari ya Paje wilaya ya Kusini Unguja umemuhamisha shuleni hapo mwanafunzi wa kiume ambae anadaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi mwenzake.

Hayo yamethibitishwa na mwalimu Mkuu wa skuli hiyo Issa Abdalla  Makame alipokuwa akizungumza na mwandishi wa.habari hizi ambae aliitaka kujuwa hatua walizochukuwa baada ya kutokea hali hiyo.

Alisema kuwa uongozi huo umechukuwa hatua hiyo kwa lengo la kutaka kuona matendo hayo hayajirejei shuleni hapo.

Alisema kuwa mwanafunzi huyo ambae jina lake limehifandhiwa anasoma darasa la 12 na tayari ameshapewa taarifa za kutafuta skuli nyengine ili kuendelea na masomo yake mara zitakapofunguliwa.

Kwa mujibu wa mwalimu Mkuu huyo alisema kuwa mwanafunzi huyo anadaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi mwenzake ambae anasoma Kidatu cha tatu shuleni hapo.

"Tulichokifanya baada ya kutokea hilo tulikutana na kukubaliana tumpe uhamisho na aende akamalizie katika skuli  nyengine kwani kuendelea kubakia hapa kutawafanya na wengine kuiga", alisema mwalimu mkuu huyo.

Alisema kuwa hili ni tukio la kwanza la wanafunzi kwa wanafunzi kupeana ujauzito lakini wameona ni bora kuchukuwa hatua haraka ili wengine wasiweze kuiga.

Mratibu wa wanawake wa shehiya ya Paje Asya Mussa Dai alisema kuwa uwamuzi waliouchukuwa sio mbaya na utatoa fundisho kwa wengine.

Hata hivyo kwa mujibu wa sheria ya elimu ya mwaka 1982 kifungu namba 20(4) kinatoa mamlaka kwa Wizara, Mwalimu Mkuu kumfukuza skuli baada ya mahakama kutoa hukumu na mwanafunzi kuthibitika kufanya kosa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.