Habari za Punde

"SINA imani tena na nafikiri siwezi kuipata haki ya mwanangu" Simulizi la sha,mbulio la aibu kwa watoto




NA MWAJUMA JUMA



"SINA imani tena na nafikiri siwezi kuipata haki ya mwanangu"



Alisema Amina Rajab mama wa mtoto aliefanyiwa shambulio la aibu  alipokutana na mwandishi wa makala hii huko kijijini kwao Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja.



Mama huyo ambae sio jina lake halisi anasema kuwa ni miezi minne tokea mwanawe afanyiwe kitendo hicho lakini bado mtuhumiwa yupo ndani.



Anasema kuwa kitendo hicho kinamyima usingizi na kukata tamaa ya kuwa hakuna haki ambayo itapatikana kwa mwanawe.



"Sijui nifanye nini maana kusema kweli wakati mwengine mpaka nguvu zinaniishia hasa pale ninapomuona mshitakiwa akiranda mitaani", anasema mama huyo ambae mtoto wake ana umri wa miaka mitano.



Mama huyo alinyooshea kidole kituo Cha Polisi Cha Jambiani ambapo ndipo aliporipoti tukio hilo kwa kusema kuwa mpaka Sasa hakioneshi jitihada zozote za kufatilia tukio hilo.



"Kusema kweli nishachoka kuona kila siku wanakuja watu na kunihoji baadae sielewi kinachoendelea isipokuwa kujiongezea maumivu tu", anafahamisha.



Anasema kuwa kwa staili hii matukio  ya udhalilishaji hayatokwisha kutokana na kuwepo kwa uzembe mkubwa unaofanywa na baadhi ya vituo vya Polisi.



Anasema kuwa Sasa hivi ndio kuna janga la maradhi ya Covid 19 ndio watasema mikusanyiko haitakiwi lakini hapo mwanzo kulikuwa hakuna karantini yoyote na haikuwa kitu.



Anaeleza kuwa baadhi ya vituo vya Polisi vinaonekana kufanya uzembe wa makusudi aofanywa  BAADHI ya vituo vya Polisi  na kuchukuwa muda mrefu  wa kufatilia upelelezi wa kesi mbali mbali za udhalilishaji
zinazoripotiwa na wananchi na kusababisha wananchi kukosa Imani na utendaji kazi wa vituo hivyo.



Anasema kuwa  imekuwa ni muda mrefu Sasa kesi yake ipo kituoni huku  akipewa majibu kesi  hizo zinafuatiliwa majimbu ambayo ambayo hayaridhishi na hayatoi matumaini ya haki kupatikana.



Alisema kuwa kwa sasa amekosa Imani na Jeshi hilo na kuona kwamba Hana  haki ambayo itapatikana.



"Mimi kwa sasa sina imani na yoyote kwani naamini hakuna haki itakayotendeka ni bora tu nikae kwani mungu anatosha", alisema mama huyo.



Mbali na mama huyo pia mama Halima Mohammed mkaazi wa Hanyegwa nae sio jina halisi anasema kuwa majibu ambayo ameyapata kwa mtoto wake kutoka kituo Cha Polisi Chwaka ni ya kusikitisha.




Anasema kuwa amekuwa na kawaida ya kufatilia lakini Mara ya mwisho jibu ambalo alipewa ni kuwa mfanyaji wa tukio ni mtoto wa miaka 13 hivyo hawezi kushitakiwa kwa mujibu wa sheria.



Hata hivyo mama huyo anasema kuwa jibu hilo halikumridhisha na madai ya kuwa mfanyaji ana umri huo sio kweli bali ana miaka 15.



Tukio la mama huyo lilitendeka mwezi Novemba mwaka jana na mtoto huyo aliumia vibaya na kupelekea kulazwa katika hospitali ya mnazimmoja kwa muda wa siku tatu.



Kwa upande wake  Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi hilo Mkoa wa Kusini Unguja Ramadhan Khamis anasema kuwa matukio yote wameyafatilia ambapo kuhusutukio la Jambiani alisema kuwa Polisi bado inaendelea kumtafuta
mshitakiwa na atakapopatikana atachukuliwa hatua.



Hivyo anasema kuwa Jeshi lake linaendelea kumtafuta na Kama wananchi wanamuona mitaani wanapaswa kutoa ushirikiano na Polisi ili aweze kukamatwa.



Kuhusu tukio la Hanyegwa Mchana anasema kuwa Jalada la  kesi hiyo lilipelekwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka DPP na lilirejeshwa huku wakitakiwa jalada hilo lifungwe kwa kuwa mfanyaji kulingana na umri hawezi kishitakiwa.



Anasema mtoto ambae alifanya kosa hilo ana umri wa miaka 13 na kwa.mujibu wa sheria hawezi kushitakiwa.




Aidha kwa upande wake Mratibu wa wa wanawake na watoto kutoka Cheju Hidaya Ali Rajab anasema kuwa mshitakiwa ni mtoto wa miaka 15 na sio 13 na kinachofanyika hapo ni dhahiri kuwa kuna udanganyifu umefanyika.



Nae Naibu Sheha wa Jambiani Kijigija Upatu Haji anasema kuwa bado kinaonekana kuwepo na harufu ya rushwa vituoni kutokana na matukio hayo kuchukuwa muda mrefu kuweza kupatiwa ufumbuzi.



Anasema kuwa kwa mfano tukio la hivi karibuni hapa shehiyani kwao mtuhumiwa hadi Sasa hajakamatwa huku akionekana kuranda mitaani.



Hivyo anasema kuwa kuendelea kuwepo kwa hali hiyo kunapelekea kuongezeka kwa matukio hayo kwani watuhumiwa wataona hakuna wanachofanywa.



Anasema kuwa kwa mwaka 2020 ndani ya shehiya yake yametokea matukio matatu ambapo moja linamuhusu mtoto wa miaka mitano aliebakwa mara mbili na watu wawili tofauti na shauri moja lipo mahakama ya watoto
Vuga na jengine linafanyiwa utaratibu wa kufikishwa mahakamani.



Tukio moja ni la shambulio la aibu ambapo mtuhumiwa wake hajapatikana hadi sasa.



Kwa upande wa Chama Cha Waandishi wa wa Habari za wanawake TAMWA Zanzibar  wamesema kuwa Polisi imekuwa na utaratibu wake katika kufatilia kesi hizo ambao unachukuwa muda mrefu.



Afisa miradi wa chama hicho Asha Abdi Makame anasema kuwa utaratibu walionao si mbaya lakini unawakwaza wananchi na kukuatisha tamaa.



"Polisi wao wana utaratibu wao katika kufatilia kesi ambayo inaanza ngazi ya chini katika kituo husika mpaka kwa RCO sio mbaya ingawa unakwaza", anasema.



Hata hivyo anawataka wananchi ambao wao wanakesi vituo vya Polisi na washitakiwa hawajakamatwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili waweze kuwakamata badala ya kukaa na kulalamika pembeni.



Anasema kuwa kuna matukio mengi yamejitokeza ambayo washitakiwa hawajakamatwa  lakini mfano mzuri wa kesi ya dude aliweza kuweka mtego na mshitakiwa aliweza kukamatwa.



Hivyo na wao wajaribu kuiga mfano huo na kuweza kutoa ushirikiano kwa Polisi ili washitakiwa waweze kukamatwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.