Habari za Punde

Wanadiaspora wasisitiza hawaikosoi serikali bali wanashauri

Assalaam Aleikoum.

Habari zenu.

Kumezuka utamaduni wa baadhi ya ndugu zetu waliopo Zanzibar na Tanzania Bara kuwashtumu ndugu zao waliopo nje ughaibuni (diaspora) kuwa wanaingilia mambo ya ndani ya Zanzibar na Tanzania khasa wakati wa janga hili la COVID — 19 iwe katika kuishauri na/au kuikosoa serikali na jamii hata kuthubutu kuwaambia hawana haki hio kwa vile wameshajiripua, washakuwa Wasomali, Waburundi nakadhalika.

Ukweli ni kwamba, sote tuliopo ndani na tuliopo nje tunahitajika na tunahitajiana katika kuinusuru Zanzibar na  Tanzania na janga hili na maendeleo ya nchi zetu.

Wacha tushirikiane wakati huu kwa fikra, mikakati, hali na mali na Insha'Allah kwa pamoja tulitokomeze janga hili thaqili khalafu baadae tufanyiane kejeli, stihzai na kudharauliana.

Huu ni wakati wa kushirikiana na kuwa kitu kimoja kwa lengo moja tu la kunusuru nchi zetu ambazo sote (wa ndani na nje) tunazipenda tena sana.

Baada ya kusema hayo, naomba niweke kumbukumbu sahihi katika baadhi ya hoja zinazotolewa na baadhi ya ndugu zetu hao kwa kutoa maelezo na vielelezo kama ifuatayvo:

SI kila alieko nje kajiripua. Sambamba, hata kwa waliojiripua bado wao ni Wazanzibari na wao ni Watanzania kwa sababu dhana ya diaspora haijikiti katika dhana ya ‘kisheria’ bali ya ‘nasaba’ zaidi. Ndio maana nchi nyingi wanakubali raia wao ambao wameshapoteza uraia wa nchi yao kutambuliwa kama diaspora ilimradi tu mtu huyo awe anajinasibu na nchi yake. Na ndivyo walivyo Wazanzibari na Watanzania po pote walipo duniani ndio maana serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mfano kwa kutambuwa mchango wa diaspora katika kusaidia na kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo ilianzisha idara ya kuratibu maendeleo kwa Wazanzibari walipo nje ambao wamekuwa wadau wakubwa katika shughuli mbali mbali za ujenzi wa taifa na kutoa misaada katika sekta ya afya, elimu, uchumi na maendeleo yenye tija kwa nchi yetu ya asili yenye na maslahi mapana kwetu sote (waliopo ndani na nje).

Inasikitisha lakini haishangazi kuona wengine wanafika hadi kusema walioko nje ziacheni serikali zetu. Lakini ni serikali zipi hizo wanazotaka ziachwe wakati zenyewe kwa kutambua na kuthamini umuhimu na michango ya wana diaspora katika maendelo ndio maana serikali ya Jamhuri ya Muungano mwaka 2010 iliunda idara maalum katika wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa ili kuiteleleza kivitendo azma ya serikali kushirikiana na wana diaspora katika kuendeleza nchi yetu.

Na kwa umuhimu huo huo, mwaka huo huo 2010 na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo ilianzisha tena ndani ya ofisi ya Rais, idara maalum kutokana na umuhimu wa Wazanzibari wanaoishi nje katika kusaidia shughuli za maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo misaada ya kifedha na ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika masuala ya afya, elimu, nakadhalika. Sasa wasikilizwe wao au zisikiliswe serikali zenyewe zinazotambua na kuthamini mawazo na michango ya hali na mali ya wana diaspora?

Suala la kushiriki kwa hali, mali na mawazo wana diaspora katika kuimarisha nchi zao za asili limepewa umuhimu mkubwa na mataifa mbali mbali pamoja na jumuia za kimataifa. Takwimu zilizotolewa na umoja wa Mataifa inaonesha kuwa wana diaspora wamekuwa wakituma kiwango kikubwa cha fedha katika nchi zao za asili kwa kiasi cha dola zaidi ya bilioni 40 kwa mwaka — kiwango ambacho ni kikubwa kuliko kiwango cha misaada rasmi ya maendeleo. Nimetoa takwimu hizo ili tuone umuhimu wa kuwa na mipango madhubuti ya kuimarisha mashirikiano na kuwashirikisha kikamilifu wana diaspora katika mipango ya maendeleo nyumbani ikiwa ni pamoja na kuzikosoa na kuzishauri serikali juu ya njia sahihi katika masuala mbali mbali ya ustawi wa nchi likiwemo hili janga la COVID — 19.

Kwa upande mwengine takwimu za bank ya dunia ambazo zimechapishwa karibuni zinaonesha kuwa fedha (remittance) ambazo Wazanzibari pamoja na Watanzania waliopo nje wanazituma nyumbani ambazo ni sawa na export revenues ni zaidi ya dola milioni mia nne kwa mwaka — kiwango ambacho sio tu kinazidi mauzo ya Karafuu, Pamba, Kahawa na Tumbaku bali kinazidi hata ukiyachanganya mazao yote hayo kwa pamoja.

Mwisho ila sio mwisho kwa umuhimu, siku zote walio nje wamekuwa ni wenye kujivunia na kukumbuka nyumbani na kujaribu kusaidia kwa hali na mali na kwa ushauri ili kupafanya napo panoge kama nchi nyengine zilizoendelea ulimwenguni.

Sote tuliopo ndani na nje ni WAZALENDO wa Zanzibar na wa Tanzania. Kushauri njia sahihi za kukabiliana na COVID — 19 hakuna maana ya kutokuwa WAZALENDO. Pamoja na ukweli huo, ni vyema pia ifahamike kuwa uzalendo SI kwa serikali. Uzalendo ni kwa taifa maana serikali zinakuja na kuondoka, lakini taifa hubaki milele. Uaminifu na utiifu kwa nchi ni kila wakati. Lakini uaminifu na utiifu kwa serikali ni pale tu inapostahili kwa kufanya mambo kwa usahihi, kwa uwazi na kwa vipaombele.

Naomba kuwasilisha.

Mungu Ibariki Zanzibar!
Mungu Ibariki Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.