Habari za Punde

Balozi Seif akagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa tangi la kuhifadhia maji safi na salama Kitope Mbaleni

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Tangi kubwa la kuhifadhia Maji safi na salama katika Kijiji cha Kitope Mbaleni.
  Baadhi ya Viongozi wa Kisiasa na Serikali wa Wiilaya ya Kaskazini “B” na Shehia ya Kitope wakisikiliza nasaha za Balozi Seif alizowapa wasimamizi wa Mradi wa Uenzi wa Tangi la Kuhifadhia Maji safi Kitope.
 Balozi Seif Ali Iddi akizishauri Kampuni na Taasisi za Kizalendo zinazopewa Miradi ya Maendeleo na Kiuchumi ni vyema zikazingatia kuheshimu Mikataba inayojenga uaminifu.
 Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Rajab Ali Rajab akitoa maelezo ya hatua alizochukuwa za kuhakikisha Mkandarasi wa Ujenzi wa Tangi la Kuhifadhia Maji Kitope Mbaleni.
 Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi akimtwisha Ndoo ya Maji Mkaazi wa Kijiji cha Mahonda Bibi Pili Mkuya Salum baada ya kuzindua Rasmi Kisima cha Maji safi na salama katika eneo hilo kilichojengwa na ufadhili wa Taasisi ya Misaada ya Hayrat Yardin.
Balozi Seif Kulia akizungumza na Wananchi wa Mahonda na kuushukuru Uongozi wa Taasisi ya Misaada ya Hayrat Yardin kwa kuiona changamoto iliyokuwa ikiwakabili Wananchi wa Mahonda ya ukosefu wa Huduma ya Maji Safi na salama.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Wahandisi wa Ujenzi Wazalendo lazima wajenge Heshima wakati wa kutekeleza Miradi wanayokabidhiwa katika misingi ya uaminifu kitendo kitachowajengea SIFA na hatimae kuaminika Zaidi.
Alisema wapo baadhi ya Wataalamu Wazalendo wenye  tabia chafu isiyokubalika ya kuwadanganya Viongozi pamoja na Taasisi zilizowakabidhi Miradi ya Ujenzi bila ya kujali kwamba wametia saini Mkataba unaowapa wajibu wa kuutekeleza kwa muda muwafaka.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Tangi kubwa la kuhifadhia Maji safi na salama katika Kijiji cha Kitope Mbaleni ambao ulichelewa kukamilika katika muda uliopangwa ambapo alilazimika kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” kuchukuwa hatua zinazostahiki dhidi ya Wahandisi wa Ujenzi wa Mradi huo.
Alisema Wahandisi Wazalendo ni vyema wakazingatia umuhimu na fursa wanazopewa na Serikali pamoja na Taasisi za Kijamii za kusimamia  Miradi ya Maendeleo na Kiuchumi kwa vile Taifa limeshaanza kuridhika na Taalum zao badala ya ile tabia ya  kuwakumbatia Wahandisi wa Kigeni
“ Baadhi ya Wakandarasi wetu wanatuangusha jambo ambalo haipendezi hata kidogo kwa vite Taifa tayari limeshajipanga  kuwatumia Wataalamu Wazawa katiak shughuli za Uhandisi badala ya wale waliozoeleka wa Kigeni wanaotumia gharama kubwa”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza na kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” kwa usimamizi mzuri wa Mradi huo uliokuwa ukisuasua katika utekelezaji wake.
Balozi Seif  alisema lengo la kuanzishwa kwa mradi huo uliopata nguvu za ufadhili ni kuwaondoshea usumbufu wa upatikanaji wa huduma za Maji safi na Salama Wananchi wanaozunguumka eneo hilo ambao wamekuwa wakitumia maji yasiyo salama kwa muda mrefu.
Akitoa Taarifa ya Mradi huo  Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Tanzania Youth Icon inayosimamia Ujenzi huo kwa ufadhili wa Taasisi moja ya Umoja wa Mataifa Bwana Abdullah Suleiman alisema jumla ya Shilingi Milioni 10,000,000 tayari zimeshalipwa katika Awamu ya pili ya Mradi huo.
Nd. Abdullah Suleiman alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba salio lililobaki litamalizwa mara tu pale Mradi huo muhimu kwa Maisha ya Wananchi utakapokamilika na kukabidhiwa Rasmi kwa Wahusika ambao ni Serikali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Rajab Ali Rajab alisema alilazimika kumpa agizo la kuripoti kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kaskazini “B” Asubuhi ya Ijumaa ya Tarehe17 Aprili Mwaka huu Mkurugenzi wa Kampuni ya Grative Tanzania Limited yenye Makao Makuu yake Dar es salaam kutoa maelezo ya kina kuhusiana na kuchelewa kumalizika kwa wakati Mradi huo.
Nd. Rajab alimueleza Balozi Seif kwamba Agizo hilo lilitanguliwa na lile alilompa Mhandisi wa usimamizi wa Ujenzi huo aliyepo Zanzibar la kumtaka asitoke nje ya Zanzibar na kuripoti kwa Mkuu wa Polisi Wilaya kila Jumatatu saa 3.00 asubuhi agizo analoendelea kulitekeleza hadi Mradi huo utakapokamilika Rasmi.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Kaskazini “B” alisema makubaliano ya kukamilika kwa Mradi huo kati ya Uongozi wa Serikali ya Wilaya hiyo na Uongozi wa Kampuni ya Grative Tanzania Limited yamefikiwa ambapo ifikapo Tarehe 25 Juni Mradi huo utakabidhiwa rasmi.
Nd. Rajab alifahamisha kwamba kukamilika kwa Mradi huo ambao kwa sasa uko katika hatua ya kumaliza Zege kwenye Tangi la juu la kuhifadhia Maji kutafuatia hatua ya Mamlaka ya Maji Zanzibar kumalizia miundombinu ya uingizaji wa huduma hiyo ili baadae iwafikie Wananchi waliokusudiwa.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alizindua Rasmi Kisima cha Maji Safi na salama kilichojengwa na Uongozi wa Jimbo la Mahonda kwa Ufadhili wa Taasisi ya Misaada ya Hayrat Yardin kilichopo Magharibi ya Skuli ya Mahonda.
Kisima hicho kilichoanza kujengwa mnamo Tarehe 9 Disemba 2019 hadi Tarehe 7 Januari 2020 kwa kuhudumia Zaidi ya Wananchi Mia Tatu wanaokizunguuka kimegharimu jumla ya Dola za Kimarekani Elfu Nne sawa na Shilingi za Kitanzania Zaidi ya Milioni Tisa.
Akizungumza na Wananchi wa eneo hilo Balozi Seif ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda aliwashukuru na kuwapongeza Viongozi na Watendaji wa Taasisi ya Misaada ya Hayrat  Yarnid kwa kuguswa na changamoto iliyokuwa ikiwakabili Wananchi wa Mahonda ya ukosefu wa hudum hiyo muhimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.