Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Ali Mohamed Shein, akiwahutubia Wananchi katika hafla ya Baraza la Eid Al Hajj lililofanyika Kitaifa Wilaya ya Kaskazini "B" Unguja katika Ukumbi wa Mitihani wa Skuli ya Sekondari ya Bumbwini leo.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein amewataka
wananchi waendelee kushirikiana ili wahakikishe kwamba uchaguzi Mkuu
utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu unafanyika kwa amani na utulivu.
Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake
aliyoitoa katika Baraza la Idd El Hajj lililofanyika huko katika skuli ya
Bumbwini, Wilaya ya Kaskazini “B”, Mkoa wa Kaskazini Unguja ambalo lilihudhuriwa
na viongozi mbali mbali pamoja na wananchi.
Alhaj Dk. Shein alisema kwa kufanyika kwa uchaguzi kwa
amani na utulivu kutaipelekea Serikali ya Awamu ya Nane itakapoingia madarakani
iweze kuyashughulikia maendeleo ya nchi kwa ufanisi zaidi.
Hivyo, aliwataka wananchi wahakikishe kwamba hatokei mtu au
kundi lolote litakalojaribu kuharibu amani hapa nchini, kupandikiza chuki,
uhasama na fitna miongoni mwa wananchi na ndani ya jamii yao.
Alhaj Dk. Shein aliwasihi viongozi wa vyama vyote vya siasa
na wagombea wao wakati ukifika wajinadi kwa wapiga kura kwa kutangaza Ilani,
Sera na Mipango ya vyama vyao.
Aliwasisitiza kuwa ni lazima wahubiri amani, umoja na
mshikamano kwa maneno na vitendo, wakijuwa kwamba lengo lao ni kujinadi ili
wachaguliwe kwa ajili ya kuiletea maendeleo nchi na kutoa huduma bora kwa
wananchi.
Aidha, Alhaj Dk. Shein aliwaeleza wananchi kwamba ni wajibu
wao kuzingatia, kuheshimu na kuzitii sheria na miongozo ya Uchaguzi inayotolewa
na Tume zote mbili za Uchaguzi ambazo ni (ZEC na NEC).
“Hivi sasa tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
katika mwezi wa Oktoba mwaka huu hivyo, tunapaswa tukumbuke kwamba msingi wa
mafanikio yote tuliyoyapata katika awamu zote ni juhudi zetu za pamoja katika
kufanya kazi, kuilinda amani na utulivu pamoja na kudumisha umoja na
mshikamano”,alisema Alhaj Dk. Shein.
Alieleza kuwa hadi sasa nchi iko shwari, harakati za
kisiasa, kiuchumi na kijamii zinaendelea vizuri na kueleza mategemeo yake kwamba
hali hiyo itadumu hadi siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Alisisitiza kuwa iwapo wananchi watafanya hivyo watatoa
fursa nzuri kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ya kuanza
utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo kwa wepesi, hamasa zaidi na ari kubwa
ili hatimae iweze kupata mafanikio makubwa zaidi.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa ili kudumisha
na kuuendeleza umoja ni lazima wananchi wajiepushe na tabia mbaya kama
kudharauliana,kusengenyana, kuhusudiana, kuhasimiana na kushwawishiana katika
kufanya hujuma dhini ya wananchi na Serikali na badaya yake wafanye mambo mema.
Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani zake za
dhati kwa wananchi wote wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
jumla kwa mapenzi makubwa waliyomuonesha na kwa kuiunga mkono Serikali katika
kuyatekeleza majukumu yake kwa vipindi vyote viwili vya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar, Awamu ya Saba.
Alhaj Dk. Shein alitoa shukurani hizo kutokana na kuwa
shughuli hiyo ya Baraza la Idd el Hajj iliyofanyika leo huko Bumbwini, Mwenyezi
Mungu akipenda itakuwa ni ya mwisho kwake kuhudhudhuria na kutoa hotuba akiwa
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
“Sote tunafahamu kwamba baada ya kufanyika uchaguzi Mkuu wa
mwaka huu wa 2020 na kupatikana Rais mwengine wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba
ya Zanzibar ya mwaka 1984 ndio itakuwa mwisho wa uongozi wangu sitoongeza hata
dakika moja seuze sekunde moja”alisema Alhaj Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa katika Ibada ya Hijja
mafunzo mengi yanapatikana ikiwemo usawa mbele ya sheria na umuhimu wake katika
kutekeleza na kufanikisha mambo mbali mbali katika maisha ya mwanaadamu.
Aliongeza kuwa miongoni mwa mafunzo makubwa yanayopatikana
katika utekelezaji wa ibada ya Hijja ni utii wa sheria pamoja na kuimarisha
umoja na mshikamano katika hali ya amani na utulivu kwani mambo hayo ndio
msingi mkubwa wa mafanikio.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa
viongozi na wananchi wa Bumbwini kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya
Kaskazini “B” pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa ujenzi wa
ukumbi uliofanyika Baraza hilo la Idd el Hajj.
Pia, aliuagiza Uongozi wa Wizara ya Elimu ushirikiane na
uongozi wa Wilaya ya Kaskazini “B” na Mkoa huo wa Kaskazini kwa ajili ya
kulikagua eneo linalokusudiwa kujengwa skuli ya Bumbwini Gongoni kwenye kijiji
kipya kwa ajili ya kutatua changamoto ya msongamano wa wanafunzi katika skuli
ya Bumbwini.
Hivyo, alisisitiza kwamba dhamira ya Serikali hivi sasa ni
kujenga Skuli za ghorofa ili kuwepo kwa matumizi bora ya ardhi hivyo, ni vyema
suala hilo likazingatiwa katika ujenzi wa skuli hio.
Pia, Alhaj Rais Dk. Shein alisema kuwa ikithibitika kwamba
eneo la karibu na Skuli ya Pangatupu linafaa kwa kuzingatia mipango miji na
vijiji iliyopo na maendeleo ya muda mrefu ya Mkoa huo, basi aliuagiza uongozi
wa Mkoa uanze mradi huo japo kwa kujenga jengo moja dogo kama ni kielelezo cha
utekelezaji wa dhamira hiyo.
Halikadhalika, alisema kuwa Mkoa wa Kaskazini Unguja hivi
sasa unaongoza hapa Zanzibar kwa kuwa na barabara mpya, nzuri na za kisasa
hivyo alitoa pongezi kwa wananchi waliokubali bila ya masharti kupitisha miradi
ya ujenzi wa barabara katika mikoa yote ya Unguja na Pemba.
Alhaj Dk. Shein pia, alieleza juu ya mpango wa ujenzi wa barabara ya Makoba
hadi Kiongwe pamoja na barabara ya Bumbwini hadi Mahonda na kueleza kuwa hiyo
ni ahadi ya Serikali na kwa vyovyote vile zitatekelezwa.
Kwa upande wa daraja la Mperura linalounganisha eneo la
Bumbwini Misufini na Pangatupu lililoporomoka alisema kuwa Serikali inaandaa
mipango ya kulifanyia matengenezo daraja hilo katika kipindi kifupi kijacho.
Katika hafla hiyo Alhaj Dk. Shein pia, aliwataka wananchi
waliohudhuria Baraza hilo kusimama kwa muda wa dakika moja kwa ajili ya
kumkumbuka Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa
aliyefariki usiku wa tarehe 23 Julai na kuzikwa nyumbani kwao Lupaso hapo juzi
tarehe 29 Julai, 2020.
Mapema Alhaj Dk. Shein alihudhuria sala la Idd el Hajj
iliyosaliwa katika uwanja wa mpira Misuka hapo Mahonda na baadae alisalimiana
na Masheikh katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo huko Kinduni.
Viongozi
mbali mbali walihudhuria katika Baraza hilo akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassam, Balozi Seif Ali Idd Makamo wa Pili
wa Rais, Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ambaye pia, ni Mgombea Urais wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM),
Wengine ni viongozi wa dini, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar
Othman Makungu, Mawaziri na Manaibu Mawaziri,Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya
Mzee, Wabunge, Wawakilishi Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa
yote ya Zanzibar, Mabalozi na viongozi wengine wa Serikali, viongozi wa vyama
vya siasa, wageni waalikwa na wananchi.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment